Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma yaahidi Kinondoni isiyo na michango shuleni

Mgombea ubunge jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chaumma, Moza Ally akiwahutubia wananchi katika viwanja vya Buibui Mwananyamala, Dar es Salaam leo Septemba 20, 2025. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mgombea huyo amewataka wananchi kutumia kura zao kwa busara ili kuleta mabadiliko ya kweli, kwani chama hicho kimejipanga kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanakuwa ya vitendo.

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Moza Ally, ameahidi kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa jimbo hilo endapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia bungeni.

Akizungumza leo, Septemba 20, 2025, katika uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika katika Viwanja vya Buibui, Mwananyamala, Moza ameeleza kwa uwazi ajenda yake kuu ya maendeleo kwa Jimbo la Kinondoni, akibainisha mambo matano ya kipaumbele yatakayotekelezwa mara tu atakapochaguliwa.

Amesisitiza kuwa kila hoja aliyoibua inalenga kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi wa Kinondoni, huku akitoa wito wa mabadiliko yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja.

“Elimu ndiyo msingi wa maendeleo, hakuna shule itakayobaki bila madarasa, madawati au vifaa vya kutosha kwa walimu na wanafunzi. Watoto wetu wanastahili kusomea katika mazingira bora,” amesema Moza.

Kuhusu ajira na uwezeshaji, Moza amesema vijana na wanawake wanahitaji fursa za kujitegemea.

“Vijana na wanawake wanastahili fursa za kujitegemea, tutaunda vituo vya mafunzo ya ufundi, biashara na ujasiriamali vitakavyowawezesha kupata ajira na kujitegemea badala ya kutegemea ajira serikalini pekee,” amesema.

Pia, mgombea huyo amegusia kero ya wazazi kuendelea kubebeshwa mzigo wa michango shuleni, akisisitiza kuwa elimu inapaswa kubaki bure kwa vitendo na si maneno tu.

“Wazazi wanabebeshwa mzigo wa michango kila siku, elimu inapaswa kubaki bure kwa vitendo na si maneno tu. Hili litashughulikiwa mara moja,” amesema Moza.

Moza pia amezungumzia sekta ya afya na changamoto ya kuzuiliwa kwa maiti hospitalini kutokana na madeni ya matibabu.

“Ni jambo la udhalilishaji kuona familia zikiteseka na maumivu ya kuondokewa na ndugu na kushindwa kumzika kwa wakati kwa sababu ya deni. Tutahakikisha suala hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” amesema.

Pia, maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii ni kipaumbele kingine cha mgombea huyo.

“Kinondoni lazima ibadilike. Tutahakikisha barabara, mitaro ya maji ya mvua na usafi wa mazingira vinaboreshwa ili wananchi wasibakie kuteseka kila siku,” amesema.

Akihitimisha hotuba yake, amewataka wananchi kutumia kura zao kwa busara ili kuleta mabadiliko ya kweli, kwani chama chao kimejipanga kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanakuwa ya vitendo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chaumma Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, amesema Moza ni mtu anayetafuta majibu ya matatizo ya wananchi kwa vitendo na si kiongozi wa kushabikia hoja bila kufikiria athari zake.

Amewaeleza wananchi wa Kinondoni kuwa wanapaswa kumpa kura mgombea ubunge wa chama hicho kwa kuwa ni kiongozi shupavu na mpenda watu atakayewatetea bungeni.

Kilewo amesema wampe nafasi ili wampime kwa vitendo, endapo atatekeleza, waendelee naye akishindwa, wamtafute mwingine lakini kwa sasa wamuamini na kumpa kura.

“Mtumeni mtu wa hoja, anayejua matatizo yenu na anayejua namna ya kuyatetea, si mtu wa kushangilia na kushika cheo. Hivyo, mnapaswa kumpa Moza muda wa miaka mitano na baadaye mumchukulie hatua kwa matendo yake,” amesema Kilewo.

Pia, Kilewo amesema Moza ni kiongozi atakayewakutanisha wananchi wote wa Kinondoni bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila, huku chama kikiwa karibu naye kuhakikisha anatimiza wajibu wake.