Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chongolo: Miradi ya umwagiliaji Lindi, Mtwara ikamilike kwa wakati

Muktasari:

  • Ahadi hiyo imetolewa wakati wa ziara ya kukagua mradi wa umwagiliaji unaotekelezwa eneo la Ndanda wilayani Masasi, mkoani Mtwara.

Masasi. Serikali imehakikishia wakulima wa Mkoa wa Mtwara kuwa miradi yote ya umwagiliaji inayoendelea kutekelezwa itakamilika kwa wakati na kuleta tija iliyokusudiwa, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa wananchi na kuongeza uhakika wa chakula.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa umwagiliaji unaotekelezwa eneo la Ndanda wilayani Masasi, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake katika taasisi na miradi iliyo chini ya wizara hiyo.

Akizungumza katika mradi huo, Chongolo amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilika na kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, huku akisisitiza kuwa umwagiliaji ni nguzo muhimu katika kufanikisha kilimo cha uhakika bila kutegemea mvua.

Mradi wa Ndanda unahusisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji pamoja na uchimbaji wa mifereji mirefu, na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 700 kutoka vijiji saba utakapokamilika.

Chongolo amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa bwawa hilo, akieleza kuwa mradi huo utatoa fursa kwa wakulima kulima mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga, mpunga, mahindi na mazao mengine, hali itakayoongeza kipato.

Ameongeza kuwa licha ya Mtwara kujulikana zaidi kwa kilimo cha korosho, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imeamua kuanzisha miradi ya umwagiliaji katika mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha uzalishaji wa mazao mchanganyiko na kupunguza utegemezi wa mazao kutoka mikoa mingine.

Chongolo pia ameitaka tume hiyo kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali, inaonekana na wakulima wananufaika kwa kupata uzalishaji unaokidhi viwango vinavyotakiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa amesema Serikali imewekeza na itaendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya umwagiliaji ili wananchi wa Lindi na Mtwara waweze kufanya kilimo cha uhakika kwa misimu yote bila kutegemea mvua.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack amewataka wananchi kushirikiana na tume katika kulinda miundombinu na rasilimali zilizowekezwa na Serikali, akisisitiza kuwa wao ndio wanufaika wakuu wa miradi hiyo.

Akitoa taarifa ya mradi, mhandisi Macklera Mrutu kutoka NIRC amesema jumla ya miradi 26 ya umwagiliaji inatekelezwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa gharama ya Sh23.7 bilioni. Amesema hadi sasa miradi miwili imeanza kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa na mifereji mikuu na ya kati, itakayohudumia zaidi ya hekta 300, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 27.

Mkulima Pili Nampokela ameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo wa umwagiliaji, akisema utawawezesha kulima mara tatu hadi nne kwa mwaka, kuongeza ajira, kuimarisha usalama wa chakula na kupunguza utegemezi wa mazao kutoka mikoa mingine.