DCEA yawatia mbaroni watuhumiwa 117 wa dawa za kulevya
Kamishna Msaidizi wa DCEA Kanda ya Kusini, John Katabi, akitoa taarifa ya mafanikio ya operesheni za kupambana na dawa za kulevya.
Muktasari:
- DCEA Kanda ya Kusini imekamata kilo 1,776 za bangi na gramu 250 za heroini katika operesheni zilizotekelezwa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, huku watuhumiwa 117 wakikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mtwara. Katika jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kusini imefanikiwa kukamata kilogramu 1,776 za bangi na gramu 250 za heroini katika operesheni mbalimbali zilizotekelezwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Operesheni hizo zilizofanyika kati ya Mei 2025 na Mei 2026 kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, pia zimewezesha kuteketezwa kwa hekari 156 za mashamba ya bangi.
Hayo yameelezwa Julai 3, 2026 na Kamishna Msaidizi wa DCEA, John Katabi, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya kwa Kanda ya Kusini, na kuongeza kuwa watuhumiwa 117 walikamatwa katika operesheni hizo, wakiwemo wanaume 107 na wanawake 10.
Katabi amesema watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani, ambapo kesi 68 zimekwishatolewa hukumu na watu 52 kupatikana na hatia, huku kesi 49 zikiendelea kusikilizwa.
Amesema mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kukabiliana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa kila kiasi cha dawa kinachokamatwa ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ya vijana na kulinda mustakabali wa jamii.
Mbali na operesheni hizo, DCEA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, ambapo wananchi zaidi ya milioni 2.5 wamefikiwa kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, taasisi za elimu, nyumba za ibada, masoko na mikusanyiko mingine ya kijamii.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amesema dawa za kulevya ni adui mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa zinaondoa nguvu kazi ya taifa, hususan vijana ambao wanapaswa kuwa wazalishaji, wabunifu na nguzo ya maendeleo ya jamii.
Mku wa wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, akihutubia hadhira katika maadhimisho ya kupinga dawa za kulevya.
Ameeleza kuwa familia nyingi zimepoteza mali na kuingia katika madeni kutokana na kuwahudumia waathirika wa dawa za kulevya, hali inayochochea umaskini, utegemezi na kuvuruga ustawi wa kijamii.
Kwa upande wa taifa, amesema matumizi ya dawa za kulevya hupunguza uzalishaji, huongeza gharama za matibabu na uhalifu, huku Serikali ikilazimika kutumia rasilimali nyingi katika udhibiti, ukamataji, matibabu na utengamao wa waathirika.
“Hivyo, kila mmoja wetu ana wajibu wa kusema hapana kwa dawa za kulevya ili kulinda uchumi wa familia zetu na taifa letu,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya haviwezi kuachiwa Serikali pekee, bali vinahitaji ushiriki wa wazazi, walezi, walimu, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali za Mitaa, vijana na jamii kwa ujumla.
Hamisi Saidi akisimulia safari yake ya kuachana na matumizi ya dawa za kulevya na kurejea katika maisha yenye tija.
Kwa upande wake, Hamisi Saidi, mmoja wa waliowahi kuwa waathirika wa dawa za kulevya, ameishukuru Serikali kwa kumpatia msaada uliomwezesha kuachana na matumizi hayo na kurejea katika maisha ya kawaida.
Amesema elimu, ushauri nasaha na huduma za utengamao alizopata zilimsaidia kutambua madhara ya dawa za kulevya na kumpa nguvu ya kuanza upya maisha yake.
“Nilikuwa nimepoteza matumaini na mwelekeo wa maisha, lakini kupitia msaada nilioupata nimeweza kuacha matumizi ya dawa za kulevya, kurejea kufanya kazi na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii" amesema