Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwinyi: Hii ni historia, haijawahi kutokea

Muktasari:

  • Watu hao wamefutarishwa katika Uwanja wa Amani Complex Mkoa wa Mjini Magharibi na kuwahusisha watu tofauti bila kujali itikadi zao

Unguja. Wakati Zanzibar ikifutarisha watu zaidi ya 25,000 kwa wakati mmoja, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema tukio hilo ni la kihistoria kwani halijawahi kutokea.

Watu hao wamefutarishwa Machi 7, 2026 katika Uwanja wa Amani Complex Unguja Zanzibar.

Akizungumza katika futari hiyo, Rais Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema amefurahishwa kuona jambo hilo linafanyika katika hali hiyo.

"Tumezoea kufutarisha kila mkoa kwa wakati wake, lakini nilipoletewa taarifa hii nilisema lifanyike ni jambo jema sana kwani halijawahikufanyika na hii ni historia," amesema Dk Mwinyi

Amesema utaratibu huo ni vyema ukaendelezwa kwani unaunganisha watu wengi kwa wakati mmoja.

Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmaoud Mahmoud amesema kufutarisha pamoja kunaongeza upendo, kuondosha chuki na kuongeza mshikamano na huruma miongoni mwa wanajamii.

"Hata kwenye maandiko vitabu vitakatifu inaelezwa wazi kufutarisha ni jambo la hekima anayefutarisha na anayefunga wote wapo sawasawa," amesema

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Akif amesema tukio hili linaonesha dunia  dhahiri kwamba Zanzibar kuna amani, upendo na utulivu katika kuwaunganisha watu wote pamoja.

Amesema kamisheni wamekuwa wakiandaa matukio mengi katika kutangaza utalii lakini walikuwa hawajafikia katika hatua hii.

"Inaonesha wazi namna ambavyo tunaweza kupiga hatua kubwa, zaidi ya miaka 30 tumeshiriki katika matukio makubwa duniani lakini hili tulikuwa hatujafikia," amesema

Awali Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Ramadhan Bukini amesema wamefurarisha takribani watu 25,000 kutoka maeneo yote ya Zanzibar bila kujali itikadi na dini za watu

"Hapa wamekuja watu wote hata wakristu wapo, hili ni jambo la kusifia na kuonesha mshikamano wetu katika kuendeleza umoja wa Wazanzibar," amesema