Dk Nchimbi aahidi kasi ya maendeleo, ahimiza uchapakazi
Muktasari:
- CCM imesema licha ya kujipanga kuwaletea maendeleo wananchi kwa kasi, nao wanapaswa kupenda kufanya kazi kwa bidii.
Bunda. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema licha ya kujipanga kuwaletea maendeleo wananchi kwa kasi, nao wanapaswa kupenda kufanya kazi kwa bidii.
Amesema CCM chini ya Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza miradi ya kimkakati, huku kipaumbele kikiwa ni utu wa wananchi wake.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumamosi, Agosti 30, 2025 kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu akiwa wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025. Uchaguzi utafanyika Jumatano Oktoba 29, kuwachagua madiwani, wabunge na Rais.
Dk Nchimbi akisalimia wananchi wa Bunda amesema amejiandaa vyema kumsaidia Samia kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi kubwa. Amewaomba wakaichague CCM Oktoba 29 kwa nafasi ya udiwani, ubunge na urais ili kuendeleza mipango waliyoiandaa.
"Mtu aliyefika Bunda miaka mitano nyuma hahitaji kuambiwa maendeleo bali yanaonekana. Kwa hiyo, wananchi nanyi muendelee kupenda kazi, inatupa heshima, kipato na kazi inakufanya kuhudumia familia," amesema.
Amesema, mgombea urais, Samia ameahidi ndani ya siku 100 atatengeneza mfumo wa kuwabana viongozi wazembe, wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo
Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akihutubia wananchi wa Bunda Mjini alipoanza ziara ya mikutano ya kampeni mkoani Mara leo Agosti 30, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
"Mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na watendaji wengine ambao watashindwa kutatua kero za wananchi, kusimamia majukumu yao ipasavyo watawajibishwa," amesema.
Amesema mfumo wa kidijitali utawawezesha wananchi kufikisha kero zao na Rais Samia ataziona na atajua imetatuliwa au la na wazembe atawashughulikia.
Awali, akisalimia wananchi wa Kisesa, wilayani Magu, Dk Nchimbi amewaahidi uboreshaji wa huduma za afya kwa kutolewa za kibingwa na kuongeza upatikanaji wa majisafi.
"Yale maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano, yatapatikana zaidi na zaidi na Mwanza historia imeonyesha kama hawataki, hawataki na kama wanataka, wanataka," amesema.
Amesema, Kisesa huduma za afya zimeimarika, shule za msingi zimeongezwa madarasa, maabara imejengwa, huduma ya majisafi na salama imeongezeka kutoka asilimia 44 hadi 73.
Dk Nchimbi amesema, wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo Agosti 28, 2025 mgombea urais wa CCM, Samia aliahidi mambo mbalimbali kuyafanya ndani ya siku 100 na katika hilo ajira 12,000 zitatolewa ndani ya muda huo. Kati ya ajira hizo mpya 5,000 za kada ya afya na 7,000 za walimu wa sayansi na hisabati.
Kauli ya Gavu, Msigwa
Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Issa Gavu Ussi akisalimia wananchi wa Bunda amesema: "Tumejipanga kushinda na ushindi huo utatokana na umoja na mshikamano wa wananchi wetu, utatokana na umoja na mshikamano wa wana-CCM."
Gavu amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM ili wakaendelee walipoishia.
Kwa upande wake, kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema kinachofanyika ni utaratibu wa kila miaka mitano kupata viongozi wapya na sasa umefika na viongozi sahihi wanatoka CCM.
Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini 2010-2020 kupitia Chadema amesema ndoto za waasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume kuiona nchi ikipiga hatua za maendeleo.
Amesema Mwalimu Nyerere alipigania uhuru kwa kumwondoa mkoloni ili kuondokana na umasikini, ujinga na maradhi na vitu hivyo vinaendelezwa vyema na Chama cha Mapinduzi.
Amewaomba wananchi wa Bunga Mjini kumchagua Ester Bulaya kuwa mbunge wao kwani uwezo huo anao na wa kutosha.
Bulaya amekuwa mbunge wa viti maalumu kupitia CCM 2010-2015. Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chadema 2015-2020. Mwaka 2020 alikuwa mbunge wa viti maalumu na amerejea tena CCM na amepitishwa kuwania ubunge kupitia chama hicho.