Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi aahidi kuifungua Ludewa, kilio cha barabara chatolewa

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewaahidi kuifungua kiuchumi Ludewa, Mkoa wa Njombe iwapo kitaibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Ludewa. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe iwapo wananchi watawachagua viongozi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya, kuwainua wakulima na wafugaji, kuanzishwa vizimba 50 vya ufugaji samaki pamoja na kujengwa barabara kwa kiwango cha lami na changarawe ni miongoni mwa ahadi za CCM kwa wananchi wa Ludewa.

Dk Nchimbi ametoa ahadi hizo leo Jumatatu, Septemba 22, 2025 katika mkutano wa kwanza wa kampeni za uchaguzi mkuu mkoani Njombe uliofanyika Uwanja wa Mpira wa Halmashauri ya Ludewa, akitokea mkoani Ruvuma.

Ahadi kwa wana Ludewa

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi ameeleza kitakachofanywa na chama hicho katika miaka mitano ijayo ikiwamo kuboresha zaidi Hospitali ya Wilaya ya Ludewa:"Nia ya CCM wananchi wasitoke wilaya moja kwenda nyingine kupata huduma. Yaani raia wa Ludewa wapate huduma Ludewa."

"Tutajenga vituo vipya vya afya 14, zahanati mpya nne. Tunataka kuboresha zaidi huduma za afya kwa wananchi wetu," amesema.

Eneo la elimu, Dk Nchimbi ameahidi Serikali ya CCM itajenga shule za msingi mpya tano zinazoendana na mahitaji na wakati, shule za sekondari sita na katika shule za zamani wakipata ridhaa watajenga   madarasa mapya 344.

Maabara 12 katika shule za sekondari zitajengwa pamoja na hosteli mpya 14 za wasichana ili kuwapunguzia adha.

Katika miaka mitano mingine, vizimba vipya 50 vya ufugaji samaki vitaanzishwa, kuongeza boti za doria Ziwa Nyasa na kila wilaya nchini tutaanzisha viwanda kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Eneo la maji, amesema miradi mipya itaanzishwa ili kuhakikisha matanki na mabomba kwenye kata zote 17 yanajengwa ili kufikia lengo la upatikanaji wa maji vijijini inakuwa asilimia 90 na mijini zaidi ya asilimia 95.

Huduma ya nishati ya umeme Ludewa, Katibu Mkuu huyo wa zamani wa CCM amesema vijiji vyote vimeunganishwa na vitongoji kama vipo havijafikiwa, vitaunganishwa.

Dk Nchimbi amesema, kwenye ufugaji hawajawasahau wana Ludewa kwani: "Majosho mapya matano na machinjio ya kisasa mbili yataanzishwa. Pia, tutaongeza idadi ya wataalamu wa mifugo.

Kuhusu eneo la barabara ambalo liligusiwa na mgombea ubunge wa Ludewa, Joseph Kamonga, Dk Nchimbi ameanza kulizungumzia akisema:"Mbunge wenu ameongea kwa msisitizo sana habari ya barabara na miundombinu."

"Mngekuwa na mbunge mbovumbovu na madiwani wabovuwabovu haya maendeleo yasingekuwepo. Anajua matatizo ya wananchi wake kwa wakati gani," amesema mbunge huyo wa zamani wa Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma.

Dk Nchimbi amesema miaka mitano iliyopita, Rais Samia amefanya kazi kubwa na ya mfano, ameelekeza nguvu zake kutatua matatizo ya na kuinua huduma za Watanzania na kasi hiyo itaongezeka mara dufu.

Dk Nchimbi amesema CCM imetambua changamoto ya miundombinu ya barabara Ludewa na ndiyo maana kwenye ilani ya uchaguzi 2025/2030 wameeleza jinsi watakavyozijenga kwa kiwango cha lami na changarawe ili kuifungua Ludewa kiuchumi na kijamii.

Miongoni mwa barabara hizo ni ya Mwambao wa Ziwa Nyasa yenye zaidi ya kilomita 100, barabara za ndani ya wilaya hiyo na zinazounganisha na wilaya zingine zitajengwa.

Alichokisema Kamoga

Kabla ya Dk Nchimbi kuzungumza, alimtambulisha Joseph Kamonga, mgombea ubunge wa Ludewa akisema anafaa kuwatumikia tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo hivyo wananchi wampe kura nyingi.

Kisha, Dk Nchimbi akampa fursa kuzungumza na wapiga kura wake ambapo amesema zaidi ya Sh318 bilioni zilipelekwa jimboni mwake na kufanikisha ujenzi wa shule za sekondari saba ikiwemo ya mafunzo kwa vitendo. Sh7 bilioni zimetumika kujenga vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (Veta).

Kamonga ambaye anatetea nafasi hiyo amesema Hospitali ya wilaya ya Ludewa imejengwa ikiwemo wodi ya kina mama, vituo vya afya vinne na zahanati 22.

Amesema changamoto kubwa ni barabara: "Mheshimiwa mgombea mwenza, eneo la barabara lipewe uzito, tunaomba sana lipewe kipaumbele." Kauli hiyo iliibua shangwe mkutanoni hapo.

 Kilio kingine amesema, katika ziwa Nyasa:"Tunaomba MV Songea ifufuliwe kwani ile meli inahimili mawimbi. Yakifanyika haya mambo yatakuwa mazuri zaidi. Tunashukuru minara zaidi 19 ya mawasiliano imejengwa."

'Hatuwadai, Oktoba 29...

Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga, maarufu Jah People amesema mambo yaliyofanyika Jimbo la Ludewa ni makubwa na mazuri:"Yaani hayajapata kutokea haki ya Mungu."

Jah People amesema mkoani Njombe, wilaya inayolima kwa wingi chakula ni Ludewa:"Sasa mahindi wamepata mengi na ombi la wakulima ni Serikali kununua mahindi nayo ikakubali. Sasa tunataka nini kama siyo Oktoba tunatiki tu."

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu na mratibu wa kampeni hizo kanda ya nyanda za juu, Salum Asas amesema mkoa wa Njombe uko vizuri, wanahakikisha amani na utulivu utashamiri na watajitokeza kukipigia kura. Naye mratibu mwenzake wa kanda ya nyanda za juu, Leonard  Qwihaya ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu amesema: "Hapa Ludewa watu hawana mashaka na CCM, hapa Ludewa tuna barabara Afrika Mashariki hakuna mfano wake, hapa Ludewa hakuna changamoto yoyote na Oktoba 29 ni kazi moja tu kutiki.

Mgombea Ubunge wa Viti Maalum, Balozi Pindi Chana amewaomba wananchi wa Ludewa kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kumchagua Samia awe Rais, Kamoga kuwa mbunge na madiwani.

Balozi Chana ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii amesema:"Sisi wana Ludewa tumefanyiwa mengi sana, tulikuwa tunatembelea umbali mrefu kwa miguu lakini sasa hali imekuwa tofauti. Maji yanatoa. Hospitali yetu imejenga 1986 na imewekwa ICU kina mama wanajifungua vizuri, Mheshimiwa Dk Nchimbi hatuwadai, mnatudai sisi."

Mbunge mwingine wa Viti Maalum , Receba Semwa amesema kwa niaba ya wanawake wote wa Ludewa kuna miradi ya Sh13.5 bilioni ya maji ambayo inamaliza tatizo la maji.