Dk Nchimbi aahidi mazingira bora ya ufugaji, kukuza utalii
Muktasari:
- Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kitakavyosimamia ipasavyo sekta ya utalii na kuweka mazingira rafiki kwa wafugaji baada ya kuingia madarakani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Longido. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema sekta ya utalii na ufugaji ni maeneo ambayo chama hicho kitaendelea kuyapa kipaumbele ili kukuza uchumi wa kudumisha amani.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Ijumaa, Septemba 12, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika uwanja wa mpira wa Longido mkoani Arusha.
Alipowasili kwenye uwanja huo, kabla ya kupanda jukwaani, amesimikwa kuwa Laigwanani.
Katika mkutano huo, amemwombea kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani huku Frederick Lowassa, James Ole Millya na Christopher Ole Sendeka wakipandishwa jukwaani kuzungumza.
Dk Nchimbi amesema kati ya makabila yote nchini ni Wamasai pekee wameendeleza utamaduni wao jambo ambalo ni zuri, na asilimia 91 wanajishughulisha na ufugaji hivyo lazima walipe kipaumbele.
"Moja ya kipaumbele ni kujali mazingira ya wafugaji. Katika miaka mitano iliyopita tumeshughulika na ufugaji, uchimbaji madini, utalii na mengine mengi mnayojionea," amesema Dk Nchimbi.
Huku akishangiliwa, Dk Nchimbi amesema: "Rais Samia amehangaika na matatizo ya wananchi, kutega sikio. Hatuna Rais mbishi, mwongo tuna Rais anayesikiliza. Ndiyo maana nchi nzima anapoona kuna tatizo anakwenda mwenyewe ama anatuma mtu wa karibu kabisa na uamuzi anaoufanya anashirikisha."
Amesema, wanaendelea kuwategemea wakulima na wafugaji na kupitia utalii umeimarisha utalii na miaka mitano, wakati wa Uviko-19 utalii ulishuka kwa karibu asilimia 80 na ndiyo maana alianzisha ‘Filamu ya The Royal Tour’.
"Kumekuwa na ongezeko la watalii zaidi ya milioni 4.9 na hii imefanywa na Rais wetu. Kiwanja kipya cha ndege kimejengwa cha kisasa Arusha ili kuimarisha utalii," amesema.
Mgombea mwenza huyo amesema katika kuimarisha ufugaji: "Yamejengwa majosho mapya 16 ya kuogeshea mifugo yetu, dawa na chanjo za mifugo zimetolewa. Serikali imetoa chanjo zaidi ya 500,000 ili mifugo yetu iwe salama na kuzaliana vizuri."
Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi amesema Serikali imejenga shule za msingi na sekondari na miaka mitano mingine watajenga zingine.
Pia, amesema kati ya vitongoji 112, 34 vimeunganishwa na umeme na vilivyobaki vinakwenda kuunganishwa.
"Tunataka watoto wa Kimasai wasome na shule 16 zitajengwa. Madarasa 88 yataongezwa. Hakikisheni watoto wanakwenda shule," amesema Dk Nchimbi.
Awali, Katibu wa Oganizesheni ya chama hicho, Issa Gavu Ussi amesema Ilani ya uchaguzi 2025/2030 imeweka utaratibu utakaotumika kutenga ardhi kwa ajili ya wafugaji na wakulima, akisema hilo litafanyika iwapo watakichagua tena chama hicho.
Alichokisema Frederick Lowassa
Aliyekuwa mbunge wa Monduli, Frederick Lowassa amesema; "Mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya Chama cha Mapinduzi umekwisha, mchakato umekwisha Longido na mchakato umekwisha Monduli," amesema Frederick.
Frederick ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Lowasaa amesema wanachama walitumia nafasi yao ya kuchagua na kuchaguliwa na vikao vikafanya uteuzi:"Sasa Monduli ni kazi moja tu kutafuta kura za Mama Samia, wabunge na madiwani."
Katika kura za maoni, Frederick aliongoza lakini Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia ilimteua, Izack Copriano maarufu Kadogoo kuwa mgombea ubunge wa Monduli.
Sendeka, Millya...
Moja ya maeneo yaliyokuwa na mvutano kwenye mbio za ubunge ni Simanjiro. Ole Sendeka na Ole Millya ni miongoni waliochukua fomu. Jina la Sendeka halikurudi. Millya akapitishwa kuwania ubunge.
Katika mkutano wa leo, Ole Millya na Sendeka wakapewa fursa ya kuzungumza na wote walikuwa walishangiliwa wakati wanazungumza kwa kuchanganya lugha za Kiswahili na Kimasai.
Millya ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, amesema Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), umekuwa chachu ya kuzalisha viongozi mbalimbali ndani ya chama na Serikali akiwemo Dk Nchimbi.
Ole Millya amesema Dk Nchimbi akiwa Mwenyekiti wa UVCCM aliwezesha kuwapika vijana mbalimbali ambao baadhi ni mawaziri:"Na mimi nimepata kwenye mikono yako. Kwa kweli Mama Samia amepata mtu sahihi wa kumsaidia."
Aidha, amesema uteuzi ndani ya chama umemalizika na wagombea wamepatikana akiwemo yeye huku akimshukuru Christopher Ole Sendeka ambaye alikuwa mbunge wa Simanjiro 2015-2020 na alipojitosa kutetea nafasi hiyo vikao viliengua jina lake kwenda hatua ya kura za maoni.
"CCM ilivyofanya uteuzi, tunaipenda na tunaheshimu. Kule Simanjiro Mzee wangu Ole Sendeka amepanda majukwaani kuninadi mimi, CCM na kuomba kura za Mama Samia, asante sana," amesema Ole Millya.
Ole Millya amesema chini ya Rais Samia na Mwenyekiti wa CCM yeye amefanikiwa kuwa:"Mbunge wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza kutoka kwenye jamii ya wafugaji. Hii ni heshima kubwa kwetu na ninawaomba Oktoba 29, tuichague CCM, tuwachague wabunge wa CCM
na madiwani."
Kwa upande wake, Ole Sendeka amesema; "Nasimama mbele yako (Dk Nchimbi) ukiwa umepata nafasi kubwa ya mgombea mwenza, kwamba nakwenda kushuhudia tunda la CCM kuanzia chipukizi hadi kuwa makamu wa Rais."
"Awamu ya sita inakwenda kuongozwa na watu ambao hatuna shaka nao (Samia na Dk Nchimbi), wanaweza kuhimili uongozi bora ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume," amesema.
Kuhusu mchakato wa uteuzi, Ole Sendeka amesema yeye ni mzoefu amekuwa akipata nafasi ya kugombea na kukosa, huku akisema hiyo ni sehemu ya siasa na atahakikisha anapambana awezavyo kutafuta kura za Rais Samia, wabunge na madiwani wa CCM.
Katika maelezo yake kwenye mkutano huo, Dk Nchimbi amesema amefurahi kuona wawili hao wanashirikiana akisema: "Nimefurahi sana mnavyoshirikiana, ni makada wa CCM wa mfano sana."
Endelea kufuatilia Mwananchi