Dk Nchimbi awataja Mwalimu Nyerere, Mzee Kawawa kuhusu uzalendo
Muktasari:
- Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Makamu wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa ni miongoni mwa wapigania uhuru wa Tanganyika sasa Tanzania ambao wanakumbukwa kwa uzalendo na utumishi uliotukuka. Dk Nchimbi amewakumbuka na kueleza alichoelezwa nao.
Liwale. Dk Emmanuel Nchimbi amesimulia nasaha alizopewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Waziri Mkuu mstaafu, Rashid Mfaume Kawawa enzi za uhai wa viongozi hao.
Dk Nchimbi amesema, mwaka 1998 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mwalimu Nyerere alimweleza aende akajifunze uzalendo na Mzee Kawawa.
Mwalimu Nyerere alilitumikia Taifa kwa nafasi mbalimbali ikiwemo Rais na alifariki dunia Oktoba 14, 1999, London, nchini Uingereza alikokwenda kwa matibabu. Mwili wake ulirejeshwa nchini na kuzikwa kwake, Butiama, Mkoa wa Mara.
Kawawa naye alitumikia Taifa hadi nafasi ya Makamu wa Rais, alifariki dunia Desemba 31, 2009, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. Mwili wake, ulizikwa katika makazi yake, Kijiji cha Madale, eneo la Wazo Hill, Dar es Salaam.
Dk Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza wa urais wa CCM ametoa simulizi juu ya Mzee Kawawa na Nyerere leo Ijumaa, Oktoba 3, 2025 katika mkutano wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa Ujenzi, Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi.
Liwale ndiko chimbuko la Hayati Kawawa ambaye enzi za utumishi wake aliitwa jina la ‘Simba wa Vita’ kwa sababu alikuwa haogopi kutekeleza uamuzi mzito.
Dk Nchimbi ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM ameanza kumadi Ilani ya chama hicho ya mwaka 2025/2030 mbele ya umati wa wananchi akiwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo.
"Mmoja wa waasisi wa chama chetu, Rashid Mfaume Kawawa alitoka hapa. Katika viongozi waliopata kutokea, waliolitumikia taifa ni Mfaume Kawawa," amesema Dk Nchimbi.
"Nilipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama chetu, kikao cha kwanza kabisa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alisema kama unataka kujifunza uzalendo kwa nchi yako kaa karibu na Mzee Kawawa," amesema Dk Nchimbi.
Amesema katika kipindi chote alipokuwa mwenyekiti wa UVCCM: "Hakuna mwezi ulipita sijaenda kuongea na Mzee Kawawa, kujifunza uzalendo na utumishi kwa nchi yangu."
Ameendelea kumwelezea Mzee Kawawa kwamba: "Desemba 2009, katika siku moja wapo nilipokwenda kumsalimia hospitalini, nilipoondoka nikaitwa tena na kurudi ndani."
Amesema aliporudi, kulikuwa na watoto wake, Vita Kawawa na Zainabu Kawawa pamoja na mlinzi wake na akasema, amemwita amweleze: "Mimi sitatoka hapa, sitarajii kupona, lakini hakikisheni chama chetu kinakuwa cha watu, hakikisheni chama chetu kinaendelea kuwatetea Watanzania wenye shida, chama chetu kiwe kimbilio la wanyonge."
Dk Nchimbi amesema wiki hiyo hakuisha, Mzee Kawawa alifariki dunia.
"Tunaendelea kuyaishi maneno yake, kama chama tunasema katika Wazee waliolitumikia Taifa ni Rashid Mfaume Kawawa," amesema.
Mgombea ubunge wa viti maalum, Zainabu Kawawa akizungumza kwa ufupi katika mkutano huo amesema,
Mgombea wa Makamu wa Rais anatuelezea historia ya Mzee Kawawa na yeye (Zainabu) kama angepata nafasi, angeweza kusimulia jinsi baba yake alivyosoma umbali mrefu kwa kutembelea kwa miguu enzi hizo akiwa Liwale.
Kitakachofanyika
Dk Nchimbi amewaomba wananchi wa Liwale kujitokeza kwa wingi Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kumchagua mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani ili waendelee kuwatumikia.
Amesema mambo mengi yamefanyika miaka mitano iliyopita kwenye eneo kila sekta ikiwemo ya afya, elimu, kilimo, ufugaji na ujenzi wa barabara: "Na miaka mitano ijayo kasi itakuwa kubwa zaidi kama mtatuchagua."
Mgombea mwenza huyo amesema, miaka mitano ijayo wanakwenda kujenga skimu mpya za umwagiliaji tano, kufanya ukarabati wa skimu zote zilizopo sasa hivi ili ziwe bora zaidi.
"Tumedhamiria kuendelea kuhakikisha wakulima wote wanaendelea kupata ruzuku ya mbolea, mbegu na madawa. Kujenga majosho mapya matatu, machinjio ya kisasa na malambo ya kuongeshea mifugo yetu yataanzishwa," amesema.
Huduma za afya amesema, wataendelea kuzisogeza karibu zaidi na wananchi ambapo watajenga vituo vya afya vitatu na zahanati tatu.
Dk Nchimbi ameahidi iwapo wataingia madarakani ujenzi wa shule mbili za msingi na moja ya sekondari huku madarasa 250 yatajengwa kwenye shule za zamani za msingi na sekondari ili kupunguza msongamano darasani.
"Tunatambua makazi ya watumishi ni changamoto, tutajenga nyumba 25 za walimu na nyumba tano za watumishi wa kada ya afya," amesema Dk Nchimbi huku akiwasisitiza kujitokeza kwa wingi Oktoba 29.
Maji ni ahadi na changamoto inayotolewa kila sehemu anapopita na Liwale, Dk Nchimbi amesema:"
Tutaboresha miradi ya maji ili kuhakikisha inashughulikiwa na wananchi wapate maji."
Ujenzi wa barabara amesema, watasimamia vyema ilani ya uchaguzi huku akitaka baadhi ya barabara ambazo zitajengwa ni ya
Mji Liwale kwa kiwango cha lami na Nangurukuru- Liwale kilomita 230 kwa kiwango cha changarawe.
Zingine ni ya Posta, Raha Leo, Sanamu na Namponda pamoja na sehemu korofi Mpiga Miti ili kurahisisha shughuli za usafirishaji na usafiri kwa wananchi.
Akimkaribisha Dk Nchimbi kuzungumza, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Lindi, Alhaj Hassan Jarufu, amesema wanashukuru kwa Serikali ya chama hicho kutoa ruzuku ya pembejeo ya kilimo hususani korosho na kuomba iendelee zaidi.
"Dk Nchimbi ni zao la UVCCM, amekulia ndani ya Chama cha Mapinduzi, anakijua chama na anaijua nchi, atakuwa msaidizi mzuri wa Rais Samia na hapa Lindi ni nyumbani karibu sana," amesema Jarufu.
Awali, Mgombea ubunge wa Liwale, Mshamu Munde amesema kuna changamoto ya maji ambapo kwa mjini upatikanaji ni asilimia 56 na kuna mradi mkubwa wa Turuki unaokwenda kumaliza tatizo hilo.
Munde amesema kuna miradi minane ya maji na uchimbaji visima vinane ambavyo navyo vikikamilika itaongeza upatikanaji wa maji.
"Hatukuwa na vituo vya afya vya kutosha, katika kipindi cha Rais Samia tumejenga vituo vitatu na Hospitali ya wilaya," amesema Munde.
Amesema katika vijiji 76 vyote vimeunganishwa na umeme huku akiomba barabara kutengenezwa ili zipitike wakati wote.