Dk Nchimbi: Ndege ya mizigo yachochea biashara ya maua, mbogamboga Kaskazini
Muktasari:
- Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ikiwemo maua na mbogamboga kwenda ughaibuni iwapo wananchi watakichagua katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Moshi. Mgombea mwenza wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dk Emmanuel Nchimbi, amesema uwekezaji wa Serikali katika usafiri wa anga umechochea biashara ya maua na mbogamboga kutoka Kanda ya Kaskazini, hali inayosaidia kukuza uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Jumamosi Septemba 13, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi, Dk Nchimbi amesema hatua ya Serikali kununua ndege mpya tano, ikiwemo ya mizigo, imefungua fursa kubwa kwa wakulima wa Kilimanjaro na Arusha kupeleka bidhaa zao moja kwa moja kwenye masoko ya kimataifa.
“Biashara za kuuza maua na mbogamboga haziwezi kufanyika bila ndege. Ndege ya mizigo tuliyonunua imekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa kanda ya kaskazini kwani sasa bidhaa zao zinawafikia wateja Ulaya na Mashariki ya Kati kwa wakati,” amesema.
Amebainisha kuwa sekta ya utalii nayo imechangia kukuza uchumi kwa kasi, akisema idadi ya watalii imeongezeka kutoka 650,000 miaka mitano iliyopita hadi kufikia 5000,000 mwaka huu, licha ya changamoto za janga la Uviko-19 lililopunguza idadi yao hadi 200,000.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na mikakati ya Serikali, ikiwemo filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeitangaza Tanzania duniani na kuongeza hamasa kwa watalii kufika nchini.
Aidha, amesema uwekezaji wa Sh4.2 bilioni kuboresha mazingira ya Mlima Kilimanjaro umesaidia kuongeza mvuto wa kitalii na hivyo kuchochea biashara ndogondogo zinazohusiana na utalii, ikiwemo upatikanaji wa masoko mapya kwa wakulima wa mazao ya bustani.
Amefafanua kuwa mapato ya utalii yamepanda kutoka Sh700 milioni hadi kufikia Sh4 bilioni katika kipindi cha miaka minne pekee kwa eneo la Kanda ya Kaskazini, hali inayothibitisha mchango wa moja kwa moja wa sekta hiyo kwenye uchumi wa wananchi.
“Tunamshukuru Rais wetu kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuimarisha diplomasia ya uchumi akiwa kama mwanadiplomasia namba moja wa nchi yetu. Kupitia jitihada hizo tumeimarisha biashara si tu ndani ya mipaka yetu, bali pia na jirani zetu hususan Kenya, ambapo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro imeongoza kufanya nao biashara,” amesema Nchimbi.
Naye mgombea ubunge wa Moshi Vijijini, Morris Mak amesema wakazi wa jimbo hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa za barabara, ambazo zimeathiri maisha yao kwa muda mrefu.
Akizungumza katika mkutano huo, Makoi amebainisha kuwa barabara ya Kibosho Shine imeharibika baada ya mkandarasi aliyepewa kazi ya upanuzi kukata mazao ya wananchi na kubomoa majengo kisha kuondoka eneo la kazi, huku haijulikani kama atarudi kukamilisha mradi huo.
“Ninaamini kupitia uongozi tutamuomba mkandarasi aendelee na kazi ili barabara hii ikamilike kabla ya Oktoba,” amesema.
Ameongeza kuwa barabara nyingine muhimu kama Mabogini-Fongageti, kilometa 31, ambayo inaunganisha Moshi Vijijini na Vunjo, iliahidiwa na Naibu Waziri wa Tamisemi wiki mbili zilizopita kwamba itajengwa kwa Sh7.5 bilioni kwa mtindo wa bottom net. Hata hivyo, hadi sasa wananchi hawajapata maelezo ya kinachoendelea.
“Pia tunazo barabara za Kiboriloni-Kidia, Sango-Kimochi na Mamboleo-Shimbwe ambazo zote zimeidhinishwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) na tayari wamefanya upembuzi pamoja na mahesabu ya gharama ya Sh29.7 bilioni. Tunaomba kwa sababu wewe ni Mwanakilimanjaro, utatusaidia kusukuma mradi huu ili barabara hizi ziweze kujengwa haraka,” amesema Makoi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema changamoto ya kupata hadhi ya Moshi kuwa jiji ni jambo linalowasumbua.
"Hapa Moshi kuna jambo ambalo linatusumbua mara nyingi na bila shaka mgombea wetu Ibrahim Shayo atafanya, mwaka 2015 tuliomba tupate jiji tukashindwa, 2020 tukaahidiwa tukipata mbunge wa CCM tutapata jiji, mheshimiwa bado tunaendelea kungoja na kukumbusha habari ya jiji," amesema.