Halotel yawekeza zaidi ya Sh2.7 trilioni Tanzania
Muktasari:
- Kampuni ya mawasiliano ya Halotel imesema imewekeza zaidi ya Dola 1 bilioni za Marekani (Sh2.7 trilioni) nchini Tanzania tangu kuanza shughuli zake, huku ikiendelea kuwekeza zaidi ya Dola milioni 100 (takribani Sh270 bilioni) kila mwaka.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Halotel imesema imewekeza zaidi ya Dola 1 bilioni za Marekani (Sh2.7 trilioni) nchini Tanzania tangu kuanza shughuli zake, huku ikiendelea kuwekeza zaidi ya Dola milioni 100 (takribani Sh270 bilioni) kila mwaka.
Hili linafanyika ili kuhakikisha miundombinu iliyopo inaimarishwa na iweze kutoa huduma za uhakika kwa wananchi, hususan za kidijitali.
Akizungumza wakati wa kufungua banda lao katika Maonyesho ya Sabasaba, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Halotel, Tran Dung amesema sehemu kubwa ya uwekezaji huo imeelekezwa katika ujenzi wa minara ya mawasiliano na upanuzi wa mtandao ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Maonyesho haya ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yalianza rasmi Juni 28 mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika Julai 13 mwaka huu.
Hilo limefanyika pia ili kuunga mkono ajenda ya taifa ya mabadiliko ya kidijitali.
“Tunaendelea kuwekeza si kwa ajili ya biashara pekee, bali pia kujenga miundombinu. Kila mwaka tunawekeza zaidi ya Dola milioni 100 katika soko la Tanzania kwa kujenga minara zaidi na kupanua huduma zetu ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi,” amesema.
Mbali na uwekezaji katika mtandao, kampuni hiyo imetangaza maboresho ya huduma ya HaloPesa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya huduma hiyo nchini.
Amesema katika kufanikisha hilo imezindua toleo jipya la programu ya HaloPesa lenye mfumo mpya utakaowawezesha wateja kupata huduma kwa urahisi zaidi pamoja na huduma za ziada, ikiwemo mikopo na malipo ya bili za umeme na maji kupitia simu.
“Maboresho hayo yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu katika shughuli za kila siku,” amesema.
Hili linafanyika wakati ambao Serikali imepanga kuanza malipo ya kidijitali katika baadhi ya huduma Julai Mosi mwaka huu.
Akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 bungeni, Waziri wa Fedha, Dk Khamis Mussa Omar, alisema mageuzi hayo yanalenga kuimarisha ajenda ya mabadiliko ya kidijitali nchini, kuongeza ufanisi wa miamala, kudhibiti uhalifu wa kifedha, kuimarisha uwazi na kupunguza gharama za kushughulikia fedha taslimu.
"Maboresho yanayofanyika katika mifumo ya malipo yatachangia jitihada za Serikali za kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika uchumi kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuzuia shughuli za kihalifu pamoja na gharama zisizo za lazima," alisema.
Kwa mujibu wa Serikali, malipo ya kidijitali yatakuwa ya lazima katika sekta mbalimbali, ikiwamo usafiri wa umma kama mabasi ya mwendokasi, vivuko, reli, usafiri wa anga na huduma za usafiri kwa kutumia programu za kidijitali.
Akizungumzia ushiriki wao katika maonyesho ya Sabasaba, amesema unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wateja.
“Kupitia Sabasaba tunapata nafasi ya kuzungumza ana kwa ana na wateja wetu, kuelewa mahitaji yao na kupata maoni yatakayosaidia kuboresha huduma zetu na kuendelea kuleta ubunifu unaokidhi matarajio yao,” amesema.
Amesema pamoja na kutoa huduma za mawasiliano, kampuni hiyo pia inalenga kuboresha maisha ya Watanzania kupitia uwekezaji katika teknolojia, huduma za kifedha za kidijitali na upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa Halotel, Abdallah Salum, amesema maonyesho ya Sabasaba ni fursa ya kukutana na wateja, kusikiliza maoni yao na kuboresha huduma.
“Mwaka huu HaloPesa inatimiza miaka 10 na imeboreshwa kwa huduma zaidi za kifedha za kidijitali ili kuimarisha matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu,” amesema.