Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatima watia nia udiwani CCM kujulikana kesho

Muktasari:

  • Hatima ya wagombea udiwani wa CCM itajulikana Agosti 13, 2025, baada ya mchakato wa kura za maoni na vikao vya uteuzi. Ingawa kuongoza kwa kura si hakikisho la kuteuliwa, wengi wanatarajia walioongoza wapate kipaumbele.

Dar es Salaam. Hatima ya kina nani watakaopeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi za udiwani wa kata na viti maalumu inatarajiwa kujulikana kesho Jumatano, siku ambayo vikao vya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa wadhifa huo vinafika tamati.

Tamati ya vikao hivyo itafuatiwa na taarifa ya uteuzi itakayotolewa kesho, Agosti 13, 2025, ambapo jina la kada mmoja kati ya waliopigiwa kura za maoni Agosti 4, 2025, litatajwa kuwa mgombea wa udiwani kupitia chama hicho.

Kukaribia kwa siku hiyo kumeongeza wasiwasi zaidi kutoka kwa miongoni mwa watiania kwa kile wanachosema kutotabirika kwa mchakato husika, kunawapa tabu ya kujua ni nani kati yao atakayepewa nafasi.

Wapo wanaosema kwa kuwa waliingia kwenye kinyang’anyiro hicho na ufahamu wa ama kuteuliwa au kutoteuliwa, lolote litakalotokea wamejipanga kulipokea kwa mikono miwili na hawatajenga kinyongo dhidi ya vikao.

Ni nyakati za lala salama kwa upande mmoja, lakini kupanda na kushuka kwa presha za watiania kwa upande mwingine, hasa ukizingatia vikao hivyo vina mamlaka ya kuteuwa jina lolote kati ya watiania waliopigiwa kura za maoni.

Kuongoza kwa wingi wa kura si hakikisho la kuteuliwa kuwa mgombea kwa mujibu wa miongozo ya chama hicho tawala tangu uhuru mwaka 1961, ndiyo sababu presha zaidi inaendelea kufukuta miongoni mwa watiania na wapambe wao.

Hata hivyo, matokeo hayo ya udiwani ndiyo yanayotarajiwa kuchora ramani ya itakavyokuwa katika uteuzi wa wagombea wa ubunge na uwakilishi.

Kwa mujibu wa watiania wa udiwani, iwapo itaonekana walioongoza kwa kura ndio watakaoteuliwa katika udiwani, hata kwa upande wa ubunge nao watajipima kwa kuangalia kigezo cha kuongoza kwa wingi wa kura.

Uteuzi wa wagombea ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar utafanyika Agosti 22, 2025, na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mchakato wa kupatikana kwa wagombea wa udiwani ulianza na makada mbalimbali wa chama hicho kuchukua na kuzirudisha katika Ofisi za CCM Kata, kisha vikafuata vikao vya mchujo kuanzia kamati za siasa za kata, wilaya na mikoa.

Vikao hivyo vilipendekeza majina matatu kati ya watiania wote na yalirudishwa kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni, kabla ya baadaye Sekretarieti ya chama hicho kutangaza watiania wote warudishwe kupigiwa kura za maoni.

Agizo la kurudishwa kwa watiania wote lilikuja baada ya malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi, wakidai watiania wao wamekatwa na wengine walisema kuna hila zilizojificha nyuma ya uteuzi wa awali uliofanyika.

Malalamiko hayo yalijibiwa kwa Sekretarieti ya chama hicho kurudisha watiania wote wakapigiwe kura za maoni. Mchakato ambao kesho ndiyo unakwenda kutoa nafasi ya mwisho.

Katika mchakato huo, waliotiania kuomba ridhaa ya udiwani kwa chama hicho walikuwa zaidi ya 30,000, kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.

Akizungumza Agosti 9, 2025, wakati akitoka kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania nafasi ya urais wa Tanzania, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwataka wanachama kuwa wamoja baada ya mchakato wa uteuzi kukamilika.

“Kama ilivyo desturi yetu ya CCM, mchakato wa uteuzi unapoisha na makundi nayo yaishe na ushindani ndani ya chama nao uishe, tunarudi kuwa kitu kimoja ili tuingie kwenye uchaguzi tukiwa wamoja na mshikamano,” alisema.

Pia Rais Samia alisema ni muhimu kudumisha desturi hiyo na vilevile wajitokeze katika maeneo yao kuwaunga mkono wagombea wao wanapokwenda ofisi za INEC kuchukua fomu za kuwa wagombea.

“Hawa ni wagombea wa chama chetu na sote tupo kwenye timu moja, hivyo twendeni kwa umoja na mshikamano kama timu ili tuhakikishe ushindi wa kishindo kwa chama,” alisema Samia.

Uteuzi huo wa CCM unafanyika ikiwa imebaki siku moja, kwani kuanzia Agosti 14, INEC itafungua dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuwania udiwani na ubunge. Dirisha hilo litafungwa Agosti 27, ambapo utafanyika uteuzi wa wagombea.

Uchukuaji na urejeshaji fomu za urais tayari umeanza tangu Agosti 9 na utamalizika Agosti 27, utakapofanyika uteuzi. Zaidi ya vyama 10 mpaka sasa vimeshachukua fomu.

Kwa mujibu wa INEC, kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza kufanyika Agosti 28 hadi Oktoba 28, siku inayofuata Jumatano ya Oktoba 29, itakuwa ni wananchi kupiga kura.


Madiwani wastaafu

Diwani wa zamani wa Buza, James Mkude, amesema siku moja kabla ya uteuzi huwa ngumu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuelekea uchaguzi.

Mkude amesema taarifa ya kuteuliwa na chama ndiyo mara nyingi inapresha zaidi kwa mgombea kuliko kusubiri matokeo ya uchaguzi.

Hofu na wasiwasi, amesema, inatokana na ukweli kwamba suala la kuteuliwa halitabiriki, bali ni kudra za Mungu kupitia uamuzi wa vikao vya viongozi wa chama husika.

“Tofauti ya matokeo ya uchaguzi na uteuzi wa wagombea ni kwamba kwenye uteuzi hautabiriki, lakini uchaguzi kuna wakati unaweza kuwa na taarifa za mapema,” amesema.

Amesisitiza katika nyakati hizi, watiania hufanya kila wanachoona kitawasaidia kupunguza hofu kama maombi na wengine wanakwenda mbali zaidi hadi kulazimika kutumia dawa za usingizi.

“Kugombea ni haki yako, lakini kuteuliwa ni uamuzi na matakwa ya chama. Hiki ndicho kinacholeta hofu na wasiwasi zaidi kwa watiania,” amesema.

Wasiwasi zaidi, amesema, inatokana na kueleweka kuwa kuongoza kwa wingi wa kura sio miongoni mwa vigezo vya kuteuliwa.

Kwa upande wa diwani wa zamani wa Kurasini, Anord Peter, amesema wanaoteseka ni wale walioshindwa kuongoza kwa wingi wa kura katika mchakato huo.

Amesema katika mchakato wa mwaka huu, kuna uwezekano walioongoza kwa kura wakapewa nafasi zaidi.

“Uzuri wa mchakato huu ni kwamba wa awali umeshafanyika na walioongoza wanajulikana na jana Katibu Mkuu amesema walioongoza katika kura ndio wapewe kipaumbele,” amesema.

Kwa sababu hiyo, amesema walioongoza kwa kura hawawezi kuwa na wasiwasi kwa kuwa wanajua wapo karibu na uteuzi.

Kwa upande wa mtiania wa udiwani wa Makangarawe, Morris Kapinga, amesema unapokwenda kwenye mashindano kuna matokeo mawili ya kushinda au kushindwa.

Katika uhalisia huo, ameeleza mtiania anapaswa kujiandaa kabla ya uteuzi, atambue kwamba pengine atateuliwa au hatateuliwa kwa sababu uamuzi haupo mikononi mwake.

“Unapokwenda kugombea unatakiwa ujue mapema kwamba nafasi yako ipo mikononi mwa vikao. Kwa hiyo jiweke tayari kushinda na kushindwa. Ukiwa katika hali hiyo, hauwezi kupata shida,” amesema.

Ameeleza unapokwenda kuomba kuhudumu sio jambo la kulazimisha, ingawa ungependa uongoze, lakini mwisho wa siku ni vikao vinaamua nani apewe nafasi hiyo.