Jamii yahimizwa kuandika wosia kupunguza migogoro ya mirathi
Baadhi ya wanawake wajane na viongozi wa chama cha wajane Tanzania (TAWIA) wakiwa katika moja ya ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kuanza safari ya kupandisha bendera kuelekea mlima Kilimanjaro.
Muktasari:
- Migogoro mingi ya mirathi inayojitokeza katika familia mbalimbali hapa nchini inaelezwa kusababishwa na kutokuwepo kwa wosia ulioandikwa, hali inayochangia kutokea kwa migongano na kutokuelewana miongoni mwa warithi baada ya kifo cha mhusika.
Moshi. Jamii imetakiwa kuacha dhana potofu kuhusu kuandika wosia na badala yake kutambua kama nyenzo muhimu ya kuzuia migogoro ya mirathi na kulinda haki za familia inayoachwa baada ya kifo cha mzazi au mlezi kutokea.
Wito huo umetolewa leo mkoani Kilimanjaro na viongozi mbalimbali walioshiriki uzinduzi wa safari ya kupeleka ujumbe wa umuhimu wa kuandika wosia katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Safari ambayo imehusisha wanawake wajane iliyobeba kauli mbiu isemayo, "Andika Wosia Kuepuka Migogoro ya Mirathi."Ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni.
Akizungumza Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Nchini (TAWIA), Rose Sarwatt amesema kwa zaidi ya miaka 10 wamekutana na changamoto nyingi zinazotokana na migogoro ya mirathi ambayo amesema ingeweza kuepukika kwa kuandika wosia.
“Wosia si uchuro, ni ishara ya kuijali na kuipenda familia yako. Changamoto kubwa ambayo hujitokeza kwenye jamii zetu ni pale mwanaume anapofariki.Mara nyingi mjane hukumbana na vikwazo vingi ikiwemo kunyimwa haki zake na kudhibitiwa katika maamuzi ya maisha yake na kusababisha migogoro isiyo ya lazima,"amesema Sarwatt.
Aidha, amesema TAWIA imekuwa ikishughulikia migogoro ya mirathi kwa miaka mingi na hadi sasa imefanikiwa kusaidia kutatua zaidi ya kesi 24,000 zinazohusu mirathi na haki za wajane hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine, Sarwatt amesema lengo la kupeleka ujumbe huo katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ni kuhamasisha jamii kuelewa kuwa changamoto za mirathi zinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa iwapo wananchi watajengewa uelewa wa kuandika wosia kwa usahihi.
Akizungumza Mjumbe wa Bodi ya Chama hicho, ambaye pia ni Wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia, amesema migogoro mingi ya mirathi inayoshuhudiwa nchini inatokana na wananchi kutokuandika wosia au kuandika wosia usiozingatia matakwa ya sheria.
Alisema wosia ni tamko la mwisho la mtu kuhusu namna anavyotaka mambo yake yaendeshwe baada ya kifo chake, ikiwemo mahali pa kuzikwa, mgawanyo wa mali na mtu atakayesimamia mirathi yake.
“Chanzo kikubwa cha migogoro ya mirathi ni kutokuwepo kwa wosia au kuwepo kwa wosia ulioandikwa kimakosa. Matokeo yake, mahakama zimekuwa zikibatilisha baadhi ya wosia kutokana na kutokidhi matakwa ya kisheria,” amesema Sungusia.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema katika mkoa huo amekuwa akisuluhisha migogoro mingi ya mirathi ikiwemo wajane kudhukumiwa mali na ndugu wa marehemu baada ya waume zao kufariki dunia huku akisema suluhusho la migogoro hiyo ni kuandika wosia ili kuiacha familia katika mikono salama.
Aidha Babu alikemea jamii kuacha tabia ya kudhulumu mali za wajane akisema ni vitendo kandamizi vinavyopaswa kukataliwa na jamii kwa kuwa mali nyingi hutafutwa kwa ushirikiano wa wanandoa.
"Jamii inayowajali wajane ni jamii inayojenga msingi imara wa haki, utu na maendeleo endelevu, wosia si uchuro, hakuna anayejua siku yake ya kuondoka duniani. Ni muhimu kuandika wosia ili kulinda familia na kuondoa migogoro isiyo ya lazima,” amesema RC Babu.