Jesca Magufuli, Bulembo na wengine moshi mweupe viti maalumu UVCCM
Muktasari:
Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) anayemaliza muda wake, Ng'wasi Kamani ameongoza katika kinyang'anyiro cha kuwania tena nafasi hiyo kwa kupata kura 409.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) anayemaliza muda wake, Ng'wasi Kamani ameongoza katika kinyang'anyiro cha kuwania tena nafasi hiyo kwa kupata kura 409.
Katika uchaguzi huo ulioanza jana asubuhi na kumalizika usiku wa manane kuamkia leo Jumamosi, Agosti 2, Ng'wasi amefuatiwa na Jesca Magufuli, mtoto wa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli aliyepata kura 391.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo akipata kura 320, Lulu Mwacha 316, Juliana Masaburi kura 282 na Timida Fyandomo 280.
Kwa upande wa Zanzibar, aliyeongoza ni Mwanaenzi Hassan Suluhu aliyepata kura 399, Latifah Juakali 357 na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah Issa aliyepata 354 na Amina Mzee kura 151.
Matokeo hayo ni hatua moja mbele kwa makada hao wa CCM, kushinda nafasi ya ubunge wa viti maalumu na kinachosubiriwa ni vikao vya uamuzi vya chama hicho kuwateua na kuwathibitisha.
Mbali na viti maalumu bara na Zanzibar, kwa upande wa nafasi za uwakilishi, walioongoza ni Salha Mwinjuna 255, akifuatiwa na Huzaina Mubarak aliyepata kura 233.
Jumuiya Wazazi
Katika kinyang'anyiro hicho kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Catherine Joachim ameongoza Tanzania Bara kwa kupata kura 597 akifuatiwa na mpinzani wake wa karibu Khadija Taya aliyepata 94.
Khadija maarufu Keysha ni Mbunge wa viti maalumu kupitia watu wenye ulemavu anayemaliza muda wake na msanii.
Kwa upande na nafasi ya viti maalumu wazazi Zanzibar aliyeshinda ni Najma Murtaza Giga aliyepata kura 591 kati ya kura 710 zilizopigwa na kuwabwaga wapinzani wake sita waliokuwa wanagombea nafasi hiyo.
Kuhusu nafasi ya uwakilishi Zanzibar walioshinda ni Aza January Joseph aliyepata kura 350 akifuatiwa na Salama Abbas Juma aliyepata kura 330 na kuwabwaga wenzao sita.
Mkutano wa jumuiya hiyo, umefanyika Agosti 1, chini ya usimamizi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, aliyesema hayo ni matokeo ya awali bado kuna uamuzi wa mwisho kutoka vikao vya chama hicho.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UVCCM wakiendelea kusubiri Matokeo ya Kura za Maoni kuwachagua Wabunge wa Viti Maalum katika ukumbi wa Jiji, Mtumba - Dodoma usiku huu Ijumaa 01 Agosti, 2025. Picha UVCCM
Katika uchaguzi huo, uliotamatika usiku wa manane, mgombea mmoja wa nafasi ya ubunge Tanzania Bara, Dk Onael Chamshana hakutokea kuomba kura, hivyo idadi ya wagombea wa nafasi hiyo ilipungua kutoka 19 hadi 18.