Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kairuki aahidi kuboresha barabara, huduma ya maji Kibamba

Muktasari:

  • Nitatumia uzoefu wangu wa ndani ya bunge na mitandao yangu ya kimataifa kuhakikisha Kibamba inapata uwekezaji na miradi ya maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki, amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kushughulikia changamoto sugu zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo, hususan katika sekta za maji, barabara, afya, na ajira kwa vijana.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika leo Jumapili, Septemba 7, 2025, katika Stendi ya Mbezi Magufuli, jijini Dar es Salaam, Kairuki amesema licha ya maendeleo yaliyopatikana, Kibamba bado haijafikia kiwango kinachotarajiwa kutokana na miundombinu duni na huduma zisizoendelevu.

“Jimbo la Kibamba linaendelea kuongezeka idadi ya watu kila siku, lakini bado huduma za jamii hazitoshi. Barabara nyingi ni za vumbi, baadhi ya maeneo hayana maji safi na salama, na huduma za afya ni za kiwango cha chini,” amesema Kairuki.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, ameahidi kuboresha barabara zote kuu na za mitaa kwa kiwango cha lami, kusambaza huduma ya maji kupitia miradi ikiwemo tanki la Bangulo, pamoja na kuboresha na kujenga vituo vipya vya afya.

Kuhusu maendeleo ya kiuchumi, hasa kwa wafanyabiashara wadogo, Kairuki ameahidi kuboresha mazingira ya biashara kwenye maeneo ya stendi ili kuwawezesha kinamama kuuza bidhaa zao kwa urahisi.

Pia amesema atahakikisha mabasi makubwa yanashusha abiria katika Stendi ya Mbezi, jambo litakaloongeza shughuli za kibiashara na kipato kwa wananchi.

Akizungumzia ajira kwa vijana, Kairuki ameahidi kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji, kuanzisha mafunzo ya teknolojia ya habari na ubunifu, pamoja na kukuza vipaji kupitia mashindano ya michezo ya Kairuki Cup.

Aidha, amesema atashirikiana na vyombo husika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.

“Vijana wetu wanahitaji mwelekeo sahihi. Nitahakikisha tunaanzisha vyuo vya ubunifu, tunawawezesha kielimu na kiuchumi, na wale wenye vipaji tutawasimamia hadi wafikie mafanikio. Sambamba na hilo, nitasimamia mpango wa lishe shuleni ili watoto wetu wawe na afya bora,” amesema.

Kuhusu ardhi, Kairuki amesema atahakikisha maeneo ya wazi yaliyovamiwa yanarejeshwa serikalini na kutumika kwa manufaa ya jamii, ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati, na maeneo ya michezo.

Ameongeza kuwa atatumia uzoefu wake ndani ya Bunge pamoja na mitandao yake ya kitaifa na kimataifa kuvutia uwekezaji na miradi ya maendeleo Kibamba. “Hakuna mlango wa serikali nitakaoshindwa kuufungua kwa ajili ya Kibamba,” amesisitiza.

Akihamasisha wananchi, Kairuki amewataka wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, kushiriki uchaguzi mkuu na kumchagua Rais, wabunge, na madiwani wa CCM ili kudumisha mshikamano na maendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo, Logatus Mbowe, amesema Kairuki ana rekodi nzuri ya utendaji serikalini, hivyo akawaomba wananchi kumpa kura nyingi ili aweze kuwatumikia kwa ufanisi.

“Tunamfahamu mgombea wetu. Ni mchapakazi na msikivu. Wananchi wa Kibamba wasisite kumpa kura,” amesema Mbowe mbele ya mamia ya wafuasi wa chama hicho.

Aliyekuwa Mbunge wa Kibamba, Abasi Mtemvu, naye amemnadi Kairuki akisema CCM imefanya uamuzi sahihi kumpitisha kuwa mgombea wa jimbo hilo.

“Kairuki ana uwezo, ni mzoefu na ni chaguo bora kwa Kibamba. Tumuunge mkono kwa nguvu zote na tumchague kwa kura nyingi ifikapo Oktoba 29,” amesema Mtemvu.

Kampeni hizo zimehitimishwa kwa hotuba ya mgombea udiwani wa Kata ya Mbezi, Pius Nyantori, ambaye pia ameahidi kushughulikia changamoto za maji, barabara, na ajira kwa vijana endapo atachaguliwa kuongoza kata hiyo.