Kanisa la Mlima wa Moto kuombea taifa siku nane
Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni B, Assemblies of God, Samwel Hillary (katikati) akizungumzia kongamano la kuliombea taifa kwa siku nane litakalofanyika nchini.
Muktasari:
- Kongamno hilo la maombi litakwenda sambamba na tamasha la kuimba na kuabudu likiwahusisha waimbaji mbalimbali wa kitaifa na kimatifa.
Dar es Salaam. Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni B, Assemblies of God, limeandaa kongamano la maombi ya siku nane kuliombea taifa, likitoa wito wa kudumisha amani, maadili na mshikamano wa kitaifa katika kipindi kinachohitaji umoja.
Maombi hayo yatafanyika kuanzia Januari 25 hadi Februari 1, 2026 katika kanisa hilo jijini Dar es Salaam, yakiongozwa na Askofu, Danstan Maboya na Askofu Rose Mgetta.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 19, 2026, Mchungaji wa kanisa hilo, Samwel Hillary, amesema lengo la kongamano hilo ni kuliombea taifa na viongozi wake ulinzi wa Mungu, pamoja na ustawi wa wananchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiroho.
Amesema kanisa lina wajibu wa kusimama na kuliombea taifa bila kujali tofauti za kisiasa, kikabila au kidini.
“Ni kongamano la kuanza mwaka na Bwana. Tuna wajibu wa kuliombea taifa tukiwa na kaulimbiu ya ‘kuchimbua visima’, kwani kuna visima vya amani, furaha na maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya kongamano hilo, Godfrey Kazinja, amesema maombi hayo yanakuja wakati ambapo maadili katika jamii yameporomoka.
“Tuna wajibu kama kanisa kuliombea taifa letu ili kuenenda katika njia zinazompendeza Mungu na kunusuru vizazi vijavyo. Tunaamini kila Mtanzania akianza na Bwana, amani na uchumi vitastawi,” amesema.
Naye mjumbe wa kamati ya maandalizi, Sarah Daniel, amesema kongamano hilo litaenda sambamba na tamasha la kuimba na kuabudu litakalowahusisha waimbaji mbalimbali wa kitaifa na kimataifa kwa lengo la kunogesha maombi hayo.