Prime
Kilichojificha nyuma mchakato ubunge Kongwa kurudiwa
Muktasari:
- Kabla ya kufariki dunia, mbunge huyo wa zamani wa Kongwa, alikuwa anaongoza katika matokeo ya awali kwa kupata kura 5,692, akifuatiwa na Isaya Mngurumi (2,602).
Dar/Dodoma. Hatua ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza kurudiwa upya mchakato wa kuwania ubunge katika Jimbo la Kongwa umehusishwa na mambo mawili kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa.
Mambo hayo ni pamoja na kuongeza demokrasia kwa watiania wa jimbo hilo na kuridhisha wale wa upande uliokuwa ukimuunga mkono marehemu Job Ndugai, kuhakikisha mchakato huo unaanza upya.
Ndugai aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, alifariki dunia Agosti 6,2025 akipatiwa matibabu jijini Dodoma.
Kabla ya kufariki dunia, Ndugai aliyekuwa akiwania nafasi ya ubunge wa jimbo hilo kwa mara nyingine, alikuwa ameshinda kura ya maoni baada ya kupata kura 5,692, akifuatiwa na Isaya Mngurumi aliyepata kura 2,602.
Aliyeshika nafasi ya tatu alikuwa Deus Seif (1,260), Dk Samora Mshang’a (544), Dk Simon Ngatunga (517), Elias Mdao (435), Philip Chiwanga (558), Paschal Mahinyila (331), Balozi Emmanuel Mbennah (232) na Ngaya Mazanda aliyepata kura 195.
Hata hivyo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 12, 2025, amesema mchakato wa kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo utafanyika kwa siku moja ambayo ni leo pekee.
Mkaugala amesema gharama za fomu ni kama ilivyokuwa awali, watiania watalazimika kulipia Sh500,000 na si vinginevyo.
Wachambuzi wanena…
Baadhi ya wachambuzi waliozungumza na Mwananchi wameonyesha kushtushwa na uamuzi huo wa CCM wakisema walidhani chama hicho kingeendeleza mchakato huo kwa watiania waliofuata baada ya Ndugai.
“Nilijua CCM ingeendelea na watiania waliobaki, kama vile ilivyokuwa kwa wabunge wa viti maalumu kama ikitokea amekufa basi wanaendelea majina yaliyopo kwenye orodha. Lakini kuurudia upya (mchakato) hali inaleta sintofahamu na kuna wingu zito nyuma yake.”
“Ingetokea Ndugai amefariki dunia baada ya uteuzi wa INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), hapo CCM ingerudia upya. Lakini kwa hiki kilichotokea ni bora wangeendelea na watiania waliobaki,” amesema Ramadhan Manyeko.
Kwa mujibu wa Manyeko, kilichopo nyuma ya pazia CCM kuurudia upya mchakato huo ni kutaka kuwaridhisha makada waliokuwa wanamuunga mkono Ndugai kwa kuhakikisha jambo hilo linaanza tena hatua ya awali.
“Wakati wa kampeni za kata kwa kata za kuomba kura wajumbe, Ndugai alikuwa anazomewa au kuulizwa maswali ambayo kwa namna moja au mwenyewe (Ndugai) alisema watu hao wamepangwa au kutumwa na washindani wake,” amesema.
Hivyo, amesema ili kuwaridhisha watu hao, CCM kimeamua kuanza upya mchakato kwa lengo la kuweka mambo sawa, kuliko kuendeleza pale walipoishia wanadhani huenda kungezua maneno tena.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema CCM ilitakiwa kuendeleza pale walipoishia mchakato huo badala kuurejea upya, kwa sababu kuna watu watalazimika kulipia upya Sh500,000 za fomu.
“Ninaona mambo mawili, mchakato huu kurudiwa, mosi watiania wa awali wataingia hasara ya kuingia mfukoni kutoa Sh500,000 za fomu. Pili kutakuwa na kuongeza kwa demokrasia kwa watiania wapya watakaoamua kuwania jimbo hilo.”
“Kuna watu, enzi za uhai wa Ndugai hawakuweza kuchukua fomu kwa kumhofia au kumheshimu spika huyo wa zamani, sasa kurejea upya kwa mchakato kutawaamsha kuchukua fomu za ubunge,” amesema Dk Mbunda.
Alichokisema Mkaugala
Kwa mujibu wa katibu huyo wa CCM, kura kwa utaratibu wa wajumbe ngazi ya kata zimepigwa leo kama ilivyofanyika Agosti 4, 2025 na baadaye vikao vya kawaida vitaendelea.
“Ni kweli tunatoa fomu kwa siku moja ya leo (Agosti 12,2025) baada ya hapa tunaendelea na taratibu za kawaida ambapo Jumapili ya Agosti 17,2025 wajumbe watapiga kura za maoni,” amesema Mkaugala.
Hata hivyo, Mkaugala hakuweka wazi kama kutakuwa na kampeni za kuzunguka kwa wajumbe kwa ajili ya kuwanadi wagombea kama awali akisema wanachama wasubiri wataelezwa utaratibu.
Wilaya ya Kongwa ilizaliwa kutoka Wilaya ya Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma na kwa sasa inaundwa na wilaya 22.
Sifa pekee inayoitambulisha wilaya hiyo, ni soko kuu la mazao ya mahindi la Kibaigwa, makumbusho ya wapigania uhuru, ikiwemo handaki kubwa la Samora Machel (rais wa zamani wa Msumbiji) na wingi wa matrekta unaotajwa unazidi maeneo mengi nchini.
Miongoni mwa waliochukua fomu ambao walikuwepo awali ni Deus Seif ambaye alishika nafasi ya tatu katika matokeo ya jumla na Elias Mdao ambaye alikuwa mtu wa sita kati ya majina 10 ambayo yalipigiwa kura.
Seif amesema ameitikia wito wa chama huku akisisitiza kuwa wajumbe ndiyo wenye kushinda ama kushindwa lakini kwake inampa huzuni kwa msiba wa aliyekuwa mgombea mwenzao.
"Kweli nilishika nafasi ya tatu lakini wajumbe ndio wameshinda maana ndiyo wenye kutupima kwenye mizani, lakini binafsi kifo cha mwenzetu kimeniumiza sana," amesema Seif.
Kwa upande wake Elias Mdao amekiri kuchukua fomu na kurudisha akisema amefanya hivyo kwa sababu ya nia njema ya kuwatumikia wananchi.
Kuhusu gharama amekiri kuwa haina shida huku akisema kama kada, amekuwa akichangia fedha nyingi kuliko hizo katika ujenzi wa chama chake cha mapinduzi.