Kupuuzwa mila na desturi kwatajwa kuchochea mmomonyoko wa maadili
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba Asili, Tiba Mbadala na Wakunga Mkoa wa Pwani, Chifu Salimu Mashimba amesema kupungua kwa matumizi ya mila na desturi za Kitanzania kumechangia mmomonyoko wa maadili.
Kibaha. Kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili, watoto kutowaheshimu wazazi na viongozi, migogoro ya kifamilia, talaka, matumizi ya dawa za kulevya na kupungua kwa mshikamano wa jamii ni miongoni mwa changamoto zinazotajwa kuchangiwa na kupuuzwa kwa mila na desturi za Kitanzania.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba Asili, Tiba Mbadala na Wakunga Mkoa wa Pwani, Chifu Salimu Mashimba, wakati akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla ya kutundika bendera ya Amani kwenye Kituo cha Tiba Asili cha Dk. Kobelo John kilichopo Visiga, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Mashimba amesema kwa miaka mingi mila na desturi zilikuwa nguzo ya malezi, heshima na mshikamano wa jamii, lakini kadiri zilivyozidi kupuuzwa ndivyo jamii ilivyoanza kushuhudia mmomonyoko wa maadili unaowaathiri zaidi vijana.
"Tunashuhudia watoto kutowaheshimu wazazi na wazee, migogoro ya kifamilia kuongezeka, vijana kujiingiza katika vitendo visivyokubalika na ndoa nyingi kuvunjika mapema. Haya yote yanatokana na kuacha misingi mizuri ya mila na desturi zetu," amesema Mashimba.
Amesema kurejesha maadili kunahitaji ushirikiano wa wazazi, wazee wa kimila, viongozi wa dini, serikali na jamii kwa ujumla, huku akisisitiza wazee kuwafundisha watoto historia, tamaduni na mila zenye kujenga utu, heshima na uzalendo.
"Wazee tusikimbie wajibu wetu. Tuwafundishe watoto wetu mila na desturi zenye kujenga maadili, kuwaheshimu wengine na kuipenda jamii yao. Tukifanya hivyo tutajenga kizazi chenye hofu ya Mungu, heshima na amani," amesema.
Akizungumzia tukio la kutundika Bendera ya Amani, Mashimba amesema hatua hiyo ni ishara ya kuhimiza umoja, mshikamano, maadili mema na matumizi sahihi ya tiba asili kwa kuzingatia sheria, kanuni na miiko ya taaluma hiyo.
Kwa upande wake, Dk. Kobelo John amesema waganga wa tiba asili wanapaswa kuwa sehemu ya kujenga amani badala ya kuwa chanzo cha migogoro katika jamii.
Amekemea baadhi ya waganga wanaotumia ramli chonganishi kuwagombanisha watu, kuvunja ndoa, kuchochea migogoro ya kifamilia na kuwatengenezea wananchi hofu kwa maslahi binafsi.
"Tiba asili ni urithi wenye thamani kubwa. Haipaswi kutumiwa kueneza chuki, kulipiza visasi wala kuwachonganisha watu. Mganga wa kweli anatibu, anashauri, anapatanisha na kuijenga jamii yenye amani. Taaluma hii iheshimiwe kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria za nchi," amesema Kobelo.
Naye Mbonde Mohamed amesema kuporomoka kwa mila na desturi kumeathiri hata taasisi ya ndoa kwa kuwa vijana wengi hawaandaliwi tena kabla ya kuingia kwenye maisha ya ndoa.
Amesema zamani wazee walitoa mafunzo ya malezi na ndoa yaliyowajengea vijana uvumilivu, heshima, uwajibikaji na namna ya kutatua migogoro, hali iliyochangia ndoa nyingi kudumu kwa miaka mingi.
"Siku hizi vijana wengi wanafahamiana kwa muda mfupi na kuamua kuishi pamoja bila maandalizi wala ushauri wa wazee. Matokeo yake migogoro imekuwa mingi na talaka zimeongezeka. Tukirejesha mafunzo ya mila na desturi zenye kujenga maadili, tutasaidia kurejesha uimara wa familia na amani ya jamii," amesema Mbonde.
Katika hafla hiyo, viongozi wa tiba asili na wananchi walisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhifadhi mila na desturi zenye manufaa kwa jamii, wakieleza kuwa ndizo msingi wa malezi bora, amani, mshikamano na maendeleo endelevu.