Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lango la Mamire lafungua fursa ya uwekezaji Babati

Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Dk Beatrice Kessy, akizungumza na waandishi wa habari katika lango jipya la kuingia Hifadhi ya Taifa Tarangire,leo Alhamisi Aprili 23,2026, lililopo wilayani Babati mkoa wa Manyara.

Muktasari:

  • Lango hilo lililozinduliwa rasmi na kuanza kutumika leo Alhamisi Aprili 23, 2026 linakuwa lango la tano la kuingia katika Hifadhi ya Taifa Tarangire ambapo fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo usafirishaji, huduma za vyakula na uanzishaji wa makazi.

Babati. Fursa mpya za uwekezaji wa utalii na shughuli zingine za kiuchumi zimefunguliwa kufuatia kuanza kutumika kwa lango la kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire la Mamire.

Lango hilo linafanya jumla ya malango ya kuingia hifadhini humo kufikia matano, huku fursa mbalimbali ikiwemo usafirishaji, uanzishaji wa malazi na huduma za vyakula zikitarajiwa kufanyika katika maeneo ya karibu.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 23, 2026 na, Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk Tutindaga George, baada ya kufunguliwa rasmi kwa lango hilo lililoanza kutumika leo.

Amesema kukamilika kwa lango hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kupanua wigo wa utalii na kuunganisha vivutio vya kanda ya kati na kaskazini.

Dk Tutindaga amealika wadau ikiwemo wawekezaji wa sekta ya utalii katika huduma za vyakula, usafirishaji na uanzishaji wa malazi ili kukuza uchumi wao.

"Niwaombe wadau wa utalii hii ni fursa yetu sasa tutumie geti kuhakikisha tunaenda kuibua fursa mpya katika mnyororo wa thamani wa sekta hii ya utalii kwani kuna fursa kwenye usafirishaji,uanzishaji wa malazi na huduma za chakula," amesema.

Amesema lango hilo litakuwa kiunganishi muhimu kwa watalii wanaotoka mikoa ya Dodoma, Singida na hata Morogoro pamoja na Dar es Salaam, ambapo sasa wanaweza kufikia hifadhi hiyo kwa urahisi zaidi bila kulazimika kupitia Minjingu kama ilivyokuwa awali.

"Linaenda kufungua fursa kubwa za kiutalii na kiuchumi na watalii wataweza kuunganisha safari zao kutoka mikoa ya Kanda ya Kati au Dar es Salaam, akifika Dodoma kwa reli ya SGR, ataweza kuja moja kwa moja hifadhini kupitia geti hili lililopo Babati," amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Dk Beatrice Kessy, amesema lango hilo lililopo umbali wa kilomita 26 kutoka mji wa Babati, limeanza rasmi kutoa huduma za vibali kwa wageni wanaoingia hifadhini kuanzia leo.

Amesema hatua hiyo ni chachu ya kukuza utalii katika ukanda huo, huku akibainisha kuwa huduma kusogezwa karibu kutapunguza gharama na muda wa safari kwa watalii.

“Lango hili litachochea uwekezaji mkubwa ndani na nje ya hifadhi. Wawekezaji watakapowekeza, wananchi watanufaika kwa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pamoja na fursa za biashara na utalii wa kitamaduni,” amesema Dk Kessy

Aliongeza kuwa tayari ajira za awali zimeanza kutolewa kwa wananchi wa eneo hilo na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kadri siku zinavyokwenda ambapo hadi sasa ajira tano zimetolewa.

"Lango hili litakuwa chachu ya kukuza utalii katika ukanda huu na tunakaribisha wadau wote wa utalii waweze kulitumia lakini mbali na kukuza utalii itatoa mchango mkubwa kwenye uchumi na wawekezaji wengi wakiendelea kuvutiwa kuwekeza itasaidia kukuza uchumi kupitia ajira zitakazotolewa,"amesema

Msimamizi wa mradi huo, Ofisa Uhifadhi daraja la pili, Goodluck Busumbilo, amesema ujenzi wa lango hilo umegharimu zaidi ya Sh 3.9 bilioni na umekamilika kwa asilimia 100.

Amesema umekamilika ukiwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo eneo la maegesho ya magari 100, nyumba tano za watumishi, vyoo vya kisasa pamoja na eneo la mapumziko kwa wageni (vimbweta).

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mamire, Augustino Sosiya, ameeema wananchi tayari wameanza kunufaika na uwepo wa lango hilo, huku akitaja ajira tano za awali zilizotolewa kwa vijana wa eneo hilo.

Amesema pia uwepo wa lango hilo umeboresha miundombinu ya barabara na kufungua fursa za masoko ya mazao na uwekezaji katika sekta ya utalii.

“Tunawaalika wawekezaji kuja kuwekeza katika eneo hili kwa kuwa lina fursa nyingi, ikiwemo ardhi ya kutosha kwa shughuli za utalii na biashara nyingine,” amesema Sosiya.