Mansour Group kuimarisha biashara, uchukuzi kikanda
Muktasari:
- Ongezeko la miradi ya miundombinu kama barabara, reli, bandari na nishati limeifanya nchi hiyo kuwa lango muhimu la biashara katika ukanda mzima
Dar es Salaam. Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati, baada ya kampuni ya kimataifa ya Mansour Group kutangaza kuanzisha mradi mpya wa magari ya kibiashara nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya logistics na biashara ya kikanda.
Mradi huo mpya unakuja katika kipindi ambacho Tanzania inazidi kuwa lango kuu ya biashara inayounganisha masoko ya Bahari ya Hindi na nchi zisizo na bandari kama Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ongezeko la miradi ya miundombinu kama barabara, reli, bandari na nishati limeifanya nchi hiyo kuwa lango muhimu la biashara katika ukanda mzima.
Mansour Group, ambayo ina uwekezaji katika zaidi ya nchi 100 duniani, imesema mradi huo utalenga kusaidia sekta zinazochochea uchumi kama usafirishaji, madini, ujenzi, kilimo na logistics, ambazo kwa sasa zinaongezeka kwa kasi kutokana na mahitaji ya ndani na ya kikanda.
Kupitia uwepo wake wa awali nchini kupitia kampuni kama Mantrac Tanzania na Mansour Automotive Tanzania, kundi hilo tayari limekuwa sehemu ya mnyororo wa maendeleo ya kiuchumi kwa kutoa huduma za vifaa na mashine zinazotumika katika sekta za uzalishaji na miundombinu.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mansour Trucks Tanzania, Anurup Chatterjee, amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika ukuaji wa biashara ya kikanda kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea katika miundombinu.
“Mradi huu unalenga kuimarisha ufanisi wa sekta ya usafirishaji na logistics, ili kuwezesha biashara kusafirishwa kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi ndani ya Tanzania na katika masoko ya kikanda,” amesema Chatterjee.
Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi zinazounganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati, hali inayofanya mahitaji ya suluhisho za kisasa za usafirishaji kuongezeka kwa kasi.
Wachambuzi wa uchumi wanasema uwekezaji huo unaongeza ushindani wa Tanzania katika ukanda, hasa katika sekta ya logistics ambayo ni mhimili muhimu wa biashara ya kikanda. Wamesema pia hatua hiyo inaashiria imani ya wawekezaji wa kimataifa katika mazingira ya biashara nchini.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuchochea zaidi uzalishaji wa ajira, uhamishaji wa teknolojia na kuongeza ujuzi kwa Watanzania, huku ukisaidia sekta binafsi kukua na kushindana katika soko la kikanda.
Uzinduzi rasmi wa mradi huo unatarajiwa kufanyika Juni 19, 2026, ukitarajiwa kuibua matumaini mapya ya Tanzania kuendelea kujikita kama kitovu cha biashara, viwanda na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati.