Mbeya: Dk Tulia ahamasisha wananchi kulinda kura na kuichagua CCM
Spika wa Bunge na mgombea ubunge wa Jimbo jipya la Uyole, Dk Tulia Ackson (kushoto), akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Busokelo, George Mwalwiba, katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Septemba 6, 2025, Shule ya Lwangwa, Rungwe.
Muktasari:
- Kauli hiyo ameitoa leo Jumamosi Septemba 6,2025 wakati akizindua kampeni na kumnadi mgombea ubunge jimbo la Busokelo Wilaya ya Rungwe mkoani hapa, George Mwalwiba.
Mbeya. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk Tulia Ackson amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Rungwe kuhakikisha wanalinda kura na kuwachagua wagombea wa CCM katika nafasi za urais, ubunge na udiwani, ili chama hicho kiweze kuunda Serikali na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dk Tulia ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo jipya la Uyole, ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Septemba 6, 2025, alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi na kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Busokelo, George Mwalwiba, katika Wilaya ya Rungwe.
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni, Dk Tulia amesema wananchi wa Rungwe wanayo dhamana kubwa ya kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuichagua CCM katika ngazi zote za uongozi.
“Ni muhimu tukalinda kura zetu na kuhakikisha tunachagua wagombea wa CCM kuanzia urais, ubunge hadi udiwani. Kwa kufanya hivyo, tunatoa nafasi kwa chama chenye dira na ilani yenye majibu ya changamoto za wananchi kuendelea kuongoza nchi,” amesema Dk Tulia.
Aidha, amepongeza maendeleo yaliyofikiwa katika Mkoa wa Mbeya, ikiwemo sekta za elimu, afya, maji na barabara, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya usimamizi madhubuti wa Serikali ya CCM.
Dk Tulia amewataka wananchi kutofanya maamuzi ya majaribio wakati wa uchaguzi, bali wachague viongozi wenye uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.
" Ifikapo Oktoba 29, 2025 wananchi mkatie tiki wagombea wa CCM ili kuwawezesha kuunda Serikali ambayo itaenda kukamilisha kazi iliyo anzishwa katika suala zima la kuleta maendeleo ya kweli," amesema.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeleta maendeleo na kuboresha huduma katika sekta ya afya, elimu, barabara na maji hususani mradi mkubwa wa kimkakati wa chanzo cha maji kutoka Mto Kiwira wenye thamani ya zaidi ya Sh119 bilioni.
"Wananchi wa Busokelo Serikali ya awamu wa sita imefanya kazi kubwa na nzuri chini ya Rais Samia Suluhu Hassan hususani sekta mbalimbali za afya ,elimu na miundombinu ya barabara na maji ," amesema.
Dk Tulia amesema kuwa uwekezaji huo unapaswa kuungwa mkono na wananchi kwa kuwapigia kura wagombea wa nafasi mbalimbali kutoka CCM.
Ahadi za mgombea
Akizungumza na wananachi waliojitokeze kwenye uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Lwangwa Halmashauri ya Busokelo, Mwalwiba ameomba ushirikiano na wananchi ili aweze kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Kwanza nashukuru sana kwa wananchi kwa kuniamini sambamba na Chama cha Mapinduzi, nitakwenda kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa vitendo katika kuleta maendeleo kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi ikiwepo elimu,afya na nyinginezo," amesema.
Mkazi wa Kandete, Frank Daudi amesema kimsingi wana imani na mgombea ubunge jimbo la Busokelo kikubwa wanahitaji maendeleo ya kweli katika nyanja mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita.