Mixx, Serikali ya Zanzibar kushirikiana kuleta mapinduzi ya kiditali kwa vyama vya ushirika
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hamza Hassan Juma akimkabidhi tunzo Mkurugenzi wa Uzingatiaji wa Sheria Mixx Tanzania Abdallah Nguba, wakati wa maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani 2026, huko katika kiwanja cha kufurahishia Watoto Tibirinzi Chake Chake.
Pemba. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya ushirika yataongeza uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika huduma za kifedha, kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Mixx by Yas na Idara ya Maendeleo ya Ushirika Zanzibar.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani, Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anayeshughulikia Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, alisema ushirikiano huo unaendana na dhamira ya Serikali ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali yatakayowezesha vyama vya ushirika kuwa na mifumo ya kisasa, salama na yenye tija.
"Mageuzi ya kidijitali katika sekta ya ushirika yataongeza uwazi, kuimarisha uwajibikaji na kuwapa wananchi huduma bora zaidi za kifedha. Ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo jumuishi na kujenga uchumi wa kisasa unaomgusa kila Mwananchi," alisema.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kunufaisha maelfu ya wanachama wa vyama vya ushirika, vikundi vya kijamii na wajasiriamali Zanzibar kwa kuwezesha usimamizi wa fedha kwa njia za kidijitali, kuongeza usalama wa miamala na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.
Mkurugenzi wa Uzingatiaji wa Sheria Mixx, Bw Abdallah Nguba alisema ushirikiano huo unaweka msingi wa mageuzi yatakayoboresha namna vyama vya ushirika vinavyosimamia fedha na kutoa huduma kwa wanachama wake kupitia teknolojia.
"Makubaliano haya yanaweka msingi wa mageuzi makubwa katika vyama vya ushirika kwa kuboresha usimamizi wa fedha, kuongeza uwazi na kurahisisha huduma kupitia teknolojia. Kupitia Mixx Kikoba, wanachama wataweza kuweka akiba, kuchangiana, kufanya malipo, kununua hisa, kupokea gawio na hata kuomba mikopo moja kwa moja kupitia simu zao," alisema.
Aliongeza kuwa vyama vya ushirika vinaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi kwa kuwaunganisha wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiriamali, huku teknolojia ikichochea uwajibikaji, kumbukumbu sahihi za kifedha na utoaji wa takwimu zitakazosaidia Serikali kupanga maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Makubaliano hayo pia yanatarajiwa kuharakisha urasimishaji wa vikundi na vyama vya ushirika, kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuongeza imani ya wanachama kupitia mifumo ya kidijitali iliyo salama na yenye uwazi.
Hatua hiyo inaendelea kuimarisha nafasi ya Mixx kama mshirika wa Serikali katika kukuza ujumuishwaji wa kifedha na kuharakisha uchumi wa kidijitali unaowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.