Mkakati wa CUF kukabili rushwa kwa watumishi wa umma
Mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF) , Gombo Samandito Gombo
Muktasari:
Chama cha Wananchi (CUF) kimeahidi kuwajengea nyumba watumishi wote wa umma ikiwa ni njia ya kukabiliana na rushwa kutokana na ugumu wa maisha.
Kahama. Chama cha Wananchi (CUF) kimeahidi kitakapopata ridhaa ya kuongoza dola, kitahakikisha kila mtumishi wa umma anajengewa nyumba ya kisasa.
Hatua hiyo imeelezwa inalenga kukabiliana na rushwa iliyoota mizizi kwenye taasisi za umma kutokana na maisha magumu ya watumishi, hivyo kushawishika kuomba na kupokea rushwa.
Ahadi hiyo imetolewa leo Septemba 5, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Gombo Samandito Gombo, kwenye mkutano wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 uliofanyika Kata ya Malunga, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Amesema: "Sisi CUF tutaboresha huduma za wafanyakazi kwa sababu wanatusaidia kufanya kazi zetu na kuwahudumia wananchi wetu, lakini hali zao ni ngumu, ndiyo maana wanakula rushwa kwa sababu ya njaa."
"Kwa hiyo wafanyakazi tutawaboreshea masilahi yao. Tutahakikisha watumishi wote wa umma wanapata nyumba za kuishi, mtu akiajiriwa tu anapewa kiwanja, anajengewa na nyumba ili aishi vizuri tupunguze njaa," amesema.
Gombo amesema chama hicho kitakapoingia tu Ikulu kitahakikisha kila mzee wa miaka 60 na kuendelea anapatiwa fedha ya kujikimu kila mwezi.
Amesema hata kama hakuwa mtumishi wa Serikali atapatiwa fedha kwa kuwa aliitumikia nchi hata kupitia kilimo au ufugaji, akieleza rasilimali zilizopo nchini zinatosha kila mmoja kuishi kwa furaha.
"Ukichagua Samandito, wazee wote wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea watapatiwa pesa ya kujikimu kila mwezi. Hata kama hakuwa mtumishi, kupitia kilimo chake aliitumikia nchi, kwa hiyo kilichopo Tanzania tutagawana wote,” amesema n a kuongeza kuwa atapambana na mafisadi.
Miundombinu ya barabara
Gombo amesema CUF ikiingia madarakani itahakikisha barabara zote za Manispaa ya Kahama zinakuwa na lami kutokana na wilaya hiyo kuwa na mapato makubwa kuliko wilaya zote za mkoa huo.
Amewataka wananchi kujitokeza kupiga kura na kukichagua chama hicho ili kiweze kuibadilisha Kahama kupitia mapato yaliyopo.
"Mkituchagua hizi barabara tutazijenga kwa kiwango cha lami kwa sababu pesa ipo. Ninyi jitokezeni mkapige kura na kuchagua CUF ili tuyafanye haya yote, mkituchagua kwa kura nyingi hawataiba," amesema na kuongeza:
"Kuwa tu Kahama tayari wewe ni tajiri, hapa mna kila kitu ila maendeleo ndiyo hamna. Kahama inakusanya mapato kuliko Shinyanga, hapa kuna mpunga, mna madini, mna tumbaku, mna pamba lakini bado mnaishi kwa shida."
Sekta ya afya
Katika sekta ya afya amesema: "Mkinichagua mimi kila mwananchi atatibiwa bure kwenye hospitali zote nchini, nitafuta bima za afya kwa sababu haziwasaidii."
"Mtu ana bima lakini akifika hospitali hapati dawa, sasa hizi bima nitazifuta kabisa na mtaishi vizuri," amesema.
Kuhusu ajira ameahidi kuajiri vijana wote wa Kitanzania kwani bado kwenye kada mbalimbali kuna upungufu wa watumishi.
"Kwa vijana wetu ambao ni Taifa la leo tutahakikisha wanapata ajira. Tutawaajiri vijana wetu wote kwa sababu pesa zipo. Ukienda shuleni watumishi ni wachache, ukienda hospitalini madaktari ni wachache, halafu mtaani wapo wanatembea hawajaajiriwa," amesema na kuongeza:
"Shida ni matumizi mabaya ya pesa, Tanzania hatuna shida ya pesa, ifike mahali wananchi na ninyi mjionee. Kwa Samandito hakuna kukosa ajira, tutazisimamia pesa zetu vizuri, tuhakikishe kwamba zinakuja kwenu kutoa ajira kwa vijana ili muishi vizuri.”
Awali, mgombea udiwani wa kata ya Malunga kupitia CUF, Anastazia James aliwaomba wananchi kura akiahidi kuboresha hali ya kata hiyo inayokabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo ubovu wa miundombinu ya barabara.
"Mnanijua, nimewahi kuwa mwenyekiti wenu, kazi zangu mnazijua, mkinichagua nakwenda kuibadilisha Malunga yetu, hili vumbi lote litaisha," ameahidi.