Mkenda Cup yawasha moto Rombo, timu 118 kushiriki
Rombo. Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro inatarajiwa kushuhudia ushindani mkubwa wa soka mwaka huu baada ya jumla ya timu 118 kuthibitisha ushiriki wao katika mashindano ya Mkenda Cup, ambayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana na kuwafungulia milango ya ajira kupitia michezo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkenda cup awamu ya nne, uliofanyika katika uwanja wa Rongai, kata ya Motamburu Kitendeni, Matibu wa mashindano hayo, Themistocles Isdori Masae, amesema Mkenda Cup imeendelea kuthibitisha umuhimu wake kwa jamii kwa kuwaunganisha vijana na kuwapa fursa ya kuonyesha vipaji vyao mbele ya wadau wa michezo.
Amesema mafanikio ya mashindano hayo yanaonekana kupitia idadi ya wachezaji waliopata nafasi ya kucheza katika ngazi za juu za soka baada ya kuonekana kupitia Mkenda Cup.
“Mashindano haya yamekuwa daraja la mafanikio kwa vijana wengi. Kupitia Mkenda Cup tumepata mchezaji wa kimataifa Suleiman Mwalimu, ambaye alianza kucheza katika timu ya Kelamfua Mokaka. Pia tumepata Chobwedo ambaye kwa sasa anacheza katika timu ya TRA inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara,” amesema Isdori.
Ameongeza kuwa mashindano hayo pia yamemlea beki Nzonzi, ambaye baada ya kuonyesha kiwango bora kwa miaka mitatu mfululizo alifanikiwa kusajiliwa na Coastal Union ya Tanga.
“Ukiangalia mafanikio haya, ni wazi kuwa Mkenda Cup si mashindano ya kawaida. Ni sehemu ambayo vijana wanapata fursa ya kuonekana na kufikia ndoto zao za kucheza soka la ushindani,” amesema.
Masae amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na udhamini wa Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, ambaye ameendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo wilayani humo.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Profesa Mkenda kwa kuendelea kuwezesha mashindano haya. Kupitia mchango wake, vijana wengi wamepata jukwaa la kuonyesha vipaji vyao na kujenga maisha yao kupitia michezo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, amesema mashindano hayo yanaonyesha mabadiliko makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya michezo wilayani humo.
Amesema ushiriki wa timu 118 ni ishara ya mwamko mkubwa wa vijana katika kutumia michezo kama njia ya kujiletea maendeleo na kuimarisha mshikamano wa jamii.
“Rombo ya sasa si ile iliyokuwa ikizungumzwa zamani. Mwaka huu tutashuhudia timu 118 zikipiga vumbi katika mashindano haya. Hii ni fursa ya vijana kujenga afya zao, kuimarisha umoja na kutafuta ajira kupitia michezo,” amesema Mwangwala.
Ameongeza kuwa mashindano ya ndani kama Mkenda Cup ndiyo yanayoendelea kuzalisha wachezaji wanaofika katika timu za Ligi Kuu na hata ngazi za kimataifa.
Akizungumza kuhusu mashindano hayo, Mbunge wa Rombo na mdhamini wa Mkenda Cup, Profesa Adolf Mkenda, aliishukuru bodi ya michezo pamoja na wajumbe wote wanaoshiriki katika maandalizi na uendeshaji wa mashindano hayo.
Profesa Mkenda alisema mafanikio ya Mkenda Cup yametokana na ushirikiano wa viongozi wa michezo, wadau na wananchi ambao wameendelea kuyaunga mkono tangu yalipoanzishwa.
“Tunashukuru sana bodi ya michezo pamoja na wajumbe wake wote kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha mashindano haya yanafanyika kwa mafanikio. Mchango wao umekuwa muhimu katika kukuza michezo na kuibua vipaji vya vijana wetu,” alisema.
Aliwataka vijana wanaoshiriki mashindano hayo kuendelea kuonyesha nidhamu, kujituma na kutumia fursa hiyo kujijengea mustakabali mzuri kupitia michezo.
“Vijana wa Rombo wapo vizuri sana. Ninawatakia kila la heri katika mashindano haya na ninaamini wataendelea kuonyesha uwezo mkubwa unaoweza kuwafungulia milango ya mafanikio katika ngazi mbalimbali za michezo,” alisema Profesa Mkenda.
Naye mchezaji wa Rongai FC, Fadhili Amiri, amesema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea vijana kujiamini na kuwapa nafasi ya kuonekana na timu mbalimbali.
“Mkenda Cup sasa ipo katika msimu wake wa nne na imekuwa msaada mkubwa kwetu vijana. Tumekuwa tukipata nafasi ya kuonyesha vipaji vyetu na kutafuta fursa za kucheza katika timu nyingine ndani na nje ya nchi,” amesema.
Amesema matarajio yake ni kuona mashindano hayo yanaendelea kukua zaidi ili vijana wengi wa Rombo na maeneo mengine wapate nafasi ya kutimiza ndoto zao kupitia michezo.
Kwa miaka minne sasa, Mkenda Cup imeendelea kujijengea sifa kama moja ya mashindano makubwa ya ngazi ya jamii mkoani Kilimanjaro, huku wadau wakiamini kuwa yana mchango mkubwa katika kuibua vipaji na kuimarisha maendeleo ya michezo nchini.