Mpina anavyopita kwenye kivuli cha Magufuli mbio za urais
Muktasari:
- Luhaga Mpina aliwahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya awamu ya tano chini ya hayati Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021. Hata katika moja ya hotuba zake Magufuli aliwahi kumsifu Mpina kwa kile alichosema anakubali uchapakazi wake.
Kisesa. Mtiania wa urais kupitia ACT Wazalendo, Luhaga Mpina amesema kabla ya kuamua kuhusu nia ya kuwania urais wa Tanzania, alikwenda katika kaburi la Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli kuomba baraka zake.
Sambamba na hilo, katika mkutano wake wa kuomba wadhamini ili awanie nafasi hiyo, Mpina amemtaja zaidi ya mara nne hayati Magufuli, akimsifu kwa utendaji uliowezesha kuongeza bei ya pamba, huku akiahidi kuyaenenda matendo hayo kwa maslahi ya umma.
Mpina aliwahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya awamu ya tano chini ya hayati Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021. Hata katika moja ya hotuba zake Magufuli aliwahi kumsifu Mpina kwa kile alichosema anakubali uchapakazi wake.
Wananchi wa Jimbo la Kisesa wakishiriki mkutano wa mapokezi ya mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, uliofanyika leo Jumamosi Agosti 16, 2025 jimboni humo.
"Nilimpa uwaziri ili akatekeleze sheria ya uvuvi. Mmeniletea mchapakazi, anatekeleza sheria," alisema hayati Magufuli Septemba 10, 2018 akiwa Meatu kwa ziara yake ya kikazi.
Mpina aliyekuwa Mbunge wa Kisesa kwa miaka 20 kupitia CCM, Agosti 5, 2025 alijiunga na ACT Wazalendo na baadaye kupitishwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mpina ameyasema hayo leo, Jumamosi Agosti 16, 2025 alipozungumza katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Mwandoya, Kisesa mkoani Simiyu, alipokwenda kuomba udhamini baada ya kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Katika hotuba hiyo ya takriban dakika 40, mwanasiasa huyo amemtaja hayati Magufuli zaidi ya mara nne, akisifu utendaji wake uliokuza bei ya pamba na hadi kufikia zaidi ya Sh2,000, hivyo atakaporidhaa atalifanya hilo.
"Magufuli alipandisha bei ya pamba hadi ikafika zaidi ya 2,000 Leo hii imeporomoka. Nitakapokamilisha masharti ya kisheria ya INEC na kuteuliwa kugombea urais, nitayasema zaidi nitakavyofanya kukuza Bei hii," amesema.
Mara ya pili, amemtaja Magufuli kuwa miongoni mwa viongozi aliokwenda kutembelea makaburi yao ili apate baraka zake kabla ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuomba wadhifa wa urais kupitia ACT Wazalendo.
Katika hoja hiyo, amesema mbali na kaburi la Magufuli pia ametembelea kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
"Nilipoona mambo yanaharibika kwa muda tofauti, nilitembelea kaburi la Baba wa Taifa kuomba baraka, kaburi la Mzee Karume, kaburi la Magufuli kuomba baraka, pia walikozaliwa wazazi wangu.
"Ili sasa baadaye pale palipo na chuki na palipojaa dharau papate heshima. Tunataka mapinduzi makubwa ya maendeleo," amesema.
Mpina amemtaja pia hayati Magufuli wakati akiimba wimbo kwa lugha ya kisukuma katikati ya hotuba yake, akisema, "Nyagotuta Magufuli," ikimaanisha tumvute Magufuli.
Ukiacha kumtaja kiongozi huyo mkuu wa nchi wa zamani, mwenendo wa hotuba za Mpina umejikita katika falsafa na misimamo inayofanana na ile ya hayati Magufuli, huku akichanganya kiswahili na kisukuma katikati ya hotuba hiyo.
Katika mazungumzo na Mwananchi, Magesa Muze mmoja wa wakazi wa Kisesa, amesema anapomuona Mpina anamfananisha na hayati Magufuli kutokana na misimamo yake.
"Huyu ni Magufuli wetu, unaona anaongea kama Magufuli, ana misimamo hapendi dhuluma kwa watu wake," amesema mwananchi huyo.
Mbali na hilo, katikati ya hotuba yake, Mpina amesema wanadhani anatania kuomba nafasi hiyo hawamjui vizuri.
"Wengine wanasema huyu hamna lolote anaigiza, nataka niseme hawanijui vizuri. Mimi nitazindua kampeni saa 6:01 usiku na nitaongea na vyombo vya habari kwa hotuba ya saa 6 za mipango ya kulibadilisha Taifa," amesema.
"Tumewaambia watu wa INEC, siku za kampeni ni chache sisi tunaweza kufanya kampeni ndani ya siku 180 usiku na mchana kwa hiyo, hatutachoka.
"Tutaingia pale Ikulu hata jasho hamna. Hata wa kupambana naye hatujamuona. Waliposikia ACT Wazalendo wamewachagua kina Mpina wameanza kuchangishana fedha," amesema.
Amesema watakwenda katika mikoa yote kuomba ridhaa za wananchi ili kukamilisha matakwa ya kisheria.
"Tumekuja mtudhamini ili tukidhi matakwa ya INEC ambayo kila mgombea wa urais na makamu wake anapaswa kupata ili ateuliwe kuwa mgombea," amesema.
Awali, akimzungumzia Mpina, Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema wamefahamiama na Mpina kwa zaidi ya miaka 20.
Amesema aliyekuwa Spika wa Bunge wa wakati huo, Samwel Sitta aliwaweka katika Kamati ya Fedha na Uchumi na huo ndio uliokuwa mwanzo wa mahusiano yao ya kazi bungeni.
Amesema walifanya kazi kwa karibu, ingawa alikuwa Mbunge wa CCM alipohitaji msaada wa kuungwa mkono bungeni kwenye mambo yenye maslahi kwa Taifa Mpina alimuunga mkono.
Mwaka 2002 katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoonyesha ubadhilifu mkubwa serikalini, amesema walianzisha kampeni ya kukusanya kura 70 ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ili awajibike Mpina alikuwa mmoja wa waliounga mkono hilo.
"Hakusita hakuogopa, alikuwa anasimamia maslahi ya nchi yake," amesema Zitto.
Mtiania wa urais visiwani Zanzibar kupitia chama hicho, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema kujaa kwa uwanja huo ni kiashiria kwamba mkutano mkuu ulifanya uamuzi sahihi wa kuwateuwa Luhaga Mpina na mgombea mwenza, Fatma Abdulhabib Ferej.
Amesema Mpina alikuwa akitumika vibaya na sasa Watanzania wataanza kumjua kwa asili yake.
"Kwa sababu Watanzania watakwenda kushuhudia nini ambacho Luhaga Mpina atakwenda kukisimamia katika kuwakomboa," amesema.