Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpogolo: ushirikiano ni silaha kukijanisha Dar

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (aliyevaa suti nyeusi) akikagua na kujionea mabanda mbalimbali yenye teknolojia ya nishati safi ya kupikia kwenye maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Viwanja vya Mnazimmoja Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Amesema utendaji wa taasisi hizo kwa kila moja kufanya kazi kivyake, ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umekuwa ukichangia kupungua kwa ufanisi katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Dar es Salaam. Taasisi zinazohusika na masuala ya mazingira nchini zimetakiwa kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za mazingira zinazingatiwa kwa lengo la kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya taifa.

Pia imeelezwa  utendaji wa taasisi hizo kwa kila moja kufanya kazi kivyake, ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umekuwa ukichangia kupungua kwa ufanisi katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja,  kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Mpogolo alisema ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa wadau wa mazingira ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika na kukutanisha taasisi mbalimbali katika mkoa huo chini ya kaulimbiu isemayo 'Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

“Ni lazima tujenge mshikamano kati ya taasisi zote zinazohusika na mazingira ili kufanikisha azma ya kuifanya Dar es Salaam kuwa ya kijani. Nawasihi tusimamie agenda hii kwa pamoja ili tuwe na nguvu ya pamoja na kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Mpogolo.

Amesema pamoja na ushirikiano wa taasisi, jamii inapaswa kuendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira ili kujenga utamaduni wa utunzaji wa mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Pia amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam kuandaa na kutekeleza mikakati rafiki ya mazingira itakayosaidia kuongeza kasi ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za mazingira.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Durdin Bilali ‘Shetta’, amesema wananchi wote wana wajibu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa kuwa maendeleo endelevu hayawezi kutenganishwa na mazingira bora.

“Maendeleo ya kweli hayawezi kutenganishwa na uhifadhi wa mazingira kwa sababu mazingira bora ndiyo msingi wa ustawi wa maisha ya wananchi na maendeleo ya jamii kwa ujumla,” amesema.

Amewataka wananchi kuwa mabalozi wa mazingira kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi, upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.

Meneja wa NEMC Wilaya ya Ilala, Zainabu Kuhanwa, amesema taasisi hiyo imeungana na Watanzania wengine kuadhimisha siku hiyo kwa kutambua kuwa maendeleo endelevu na uchumi imara vinategemea uhifadhi wa mazingira.

“Kwa miaka 40 tangu kuanzishwa kwa NEMC, tumekuwa tukipanda miti kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira. Mazingira ni uhai wetu, hivyo ni muhimu kuendelea kuyatunza na kuyakijanisha ili yaendelee kutulinda na kutuwezesha kuishi katika mazingira salama,” amesema.

Naye Mhifadhi Mwandamizi wa TFS Wilaya ya Ilala, Albert Masao, amesema wakala huo unaendelea kuzalisha miche ya miti kwa wingi na kuisambaza kwa wananchi ili kuhamasisha upandaji miti na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wa ukusanyaji taka ngumu Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajenjere, Mathew Andrew, amesema mazingira safi ni msingi wa maendeleo ya taifa na urithi muhimu kwa vizazi vijavyo.

“Mazingira si suala la taka pekee, bali yanahusisha afya ya wananchi na uhai wa taifa. Mji safi huvutia uwekezaji, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya wananchi wanaodharau kazi inayofanywa na wahudumu wa usimamizi wa taka wanapoona magari ya kubeba taka yakipita barabarani,” amesema.

Amesema nyuma ya huduma hizo kuna maelfu ya wananchi wanaotegemea sekta ya usimamizi wa taka kujipatia kipato, huku vijana wengi wakinufaika kupitia ajira zinazotokana na shughuli za ukusanyaji na uchakataji wa taka.

Andrew amesisitiza kuwa jamii inapaswa kutambua kuwa taka ni rasilimali yenye thamani ya kiuchumi na chanzo cha ajira nyingi iwapo itasimamiwa ipasavyo.

Pia ameiomba Serikali kuendelea kuipa sekta hiyo kipaumbele kwa mtazamo wa kimkakati katika kukuza uchumi, ikiwemo kuwapatia wakandarasi mikataba yenye uhakika itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.