Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa Hatifungani ya Kijani kuondoa adha ya maji Tanga

Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Pradeep Kurukulasuriya (katikati), akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Huduma za Maji Taka wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (UWASA), Mhandisi Salum Ngumbi (kushoto), na viongozi wengine wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Kukusanya Maji wa Mabayani unaofadhiliwa kupitia Hatifungani ya Kijani ya UNCDF mkoani Tanga.

Muktasari:

  • Mradi wa Hatifungani ya Kijani unaotekelezwa na UWASA Tanga kwa ufadhili wa UNCDF unatarajiwa kupunguza changamoto ya maji mkoani Tanga kwa kuongeza uzalishaji kutoka mita za ujazo 42,000 hadi 60,000 kwa siku.

Tanga. Wakazi wa Mkoa wa Tanga wanatarajiwa kupata nafuu ya huduma ya maji baada ya utekelezaji wa Mradi wa Hatifungani ya Kijani unaolenga kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Mradi huo unaotekelezwa katika eneo la Mowe kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (UWASA), unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 42,000 hadi mita za ujazo 60,000 kwa siku.

Ongezeko hilo linatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji inayowakabili baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Tanga, pamoja na kuboresha huduma ya maji safi na salama katika Wilaya za Tanga, Pangani na Muheza.

Akizungumza wakati wa ziara yake mjini Tanga, Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF), Pradeep Kurukulasuriya, amesema mafanikio yanayoonekana katika utekelezaji wa mradi huo yanaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.

Akiwa katika Bwawa la Mabayani, chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa Jiji la Tanga, Kurukulasuriya amesema UNCDF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufadhili miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi.

“Mradi huu unalenga kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo mbalimbali. Tunaendelea kushirikiana na Serikali kutokana na maendeleo mazuri yanayoonekana katika utekelezaji wa miradi hii,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Huduma za Majitaka wa UWASA, Mhandisi Salum Ngumbi, amesema mradi huo umefikia asilimia 60 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

Amesema kukamilika kwa mradi kutakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa maji na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa maeneo yatakayofikiwa na huduma hiyo.

Mradi wa Hatifungani ya Kijani unafadhiliwa na UNCDF ukiwa sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya maji na kuongeza uwezo wa uzalishaji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi.