Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mto Gide, ajira kilio cha wajumbe Ubungo

Muktasari:

Wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam wamehoji watiania ya ubunge kuhusu changamoto za Mto Gide.

Dar es Salaam. Athari za Mto Gide kwa makazi ya binadamu, uhaba wa ajira na masoko ni miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), dhidi ya watiania wa udiwani na ubunge waliokwenda kujitambulisha kuelekea kura za maoni Agosti 4, 2025.

Kwa mujibu wa hoja za wajumbe hao, hizo ndizo changamoto zinazowakabili wakazi wa Jimbo la Ubungo, linalowaniwa na Profesa Kitila Mkumbo anayetetea nafasi yake, Elizabeth Jackson, Andrew Kulwa, Seif Chekanae na Dk John Kahemele.

Wajumbe wametoa hoja kuhusu Mto Gide ikiwa ni miezi miwili imepita tangu Mwananchi lilipochapisha ripoti maalumu kuhusu kutanuka kwa mito ikiwamo Gide, kunavyoathiri makazi ya wananchi wa Ubungo na maeneo ya jirani.

Katika ripoti hiyo iliyochapishwa Juni 15 na 16, mwaka huu, Mwananchi lilieleza mkakati wa Serikali wa kujenga kingo za mto huo, kama hatua ya kudumu kukomesha mmomonyoko wa udongo, unaosababisha kutanuka kwa mto husika na hatimaye kuathiri makazi.

Hatua ya watiania kujitambulisha kwa wajumbe, itafuatiwa na mchakato wa kura za maoni zitakazopigwa Agosti 4 na ndizo zitakazoamua mtiania atakayepitishwa na vikao vya juu vya chama hicho, kugombea ubunge.

Hoja hizo ziliibuliwa jana Agosti 1, 2025 katika ziara ya watiania wa ubunge na udiwani wa CCM, kujitambulisha kwa wajumbe wa kata za Ubungo.

Wakiwa Kata ya Kimara, wajumbe walihoji kwa nini kingo za Mto Gide hazijajengwa licha ya kuwa ni miongoni mwa ahadi kuu za Profesa Kitila katika kipindi cha uongozi wake jimboni humo.

Akijibu hoja hiyo, Profesa Kitila ameeleza tayari alichukua hatua kwa kutumia Sh5 milioni kutoka mfuko wa maendeleo ya jimbo kwa kila kata inayopakana na mto huo, ikiwemo Kimara.

Amesema fedha hizo zilielekezwa katika juhudi za muda mfupi kupunguza athari za mto huo wakati Serikali ikiendelea na taratibu za utekelezaji wa mradi mkubwa wa kudhibiti mafuriko.

Profesa Kitila ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, amesisitiza akipewa ridhaa tena, atalifuatilia kwa ukaribu zaidi suala hilo hadi lifikie mwisho.

Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa Soko la Midizini, amesema atalijenga ili kuwaokoa wanawake kwenda umbali mrefu kutafuta bidhaa na kwamba ataanzisha elimu ya ujasiriamali na mifuko ya vijana ili wapate mikopo.

Elizabeth yeye amesema endapo watampa ridhaa atahakikisha anaboresha miundombinu ili kupunguza mafuriko na ajira kwa vijana.

Amesema miradi inayokuja Ubungo itaanza kuwanufaisha na atashughulikia mikopo kwa wanawake.

Alipoulizwa kuhusu huduma za afya, ameahidi atapigania kupatikana kwa hospitali kwa ajili ya wakazi wa Manzese.

Dk Kahemela amesema magumu yanayoikumba Ubungo ni mengi, likiwamo suala la ukosefu wa maji na elimu duni.

"Tuna uwezo wa kuijenga Ubungo yetu kwa sababu nipo muda mrefu jimboni hapa, hivyo nazifahamu changamoto zetu nichagueni ili nikawatatulie," amesema.

Pia alizungumzia suala la kuzuiwa maiti mochwari kutokana na watu kukosa fedha, akisema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza hakuna maiti ya mtu kuzuiwa. Amesema mwenye changamoto anapaswa kwenda ofisi za ustawi wa jamii ili mwili utolewe pasipo malipo.

Chekanae amesema kwa sasa Serikali inahitaji vijana, hivyo kwa umri wake, atajituma na hatakuwa na visingizio katika kuyatafuta maendeleo kwa ajili ya jamii.

"Jimbo la Ubungo linahitaji mchapakazi, mimi ndiye ninayefaa kuja kutatua shida za jimbo hili, nitakuwa karibu na kina mama kuhusu mikopo inayowaumiza," amesema.