Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu: Nikitinga Ikulu hakuna kuvaa suti

Muktasari:

  • Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ni siku ambayo Watanzania watapiga kura kuwachagua madiwani, wabunge na Rais. Mtiania wa nafasi ya urais wa Chaumma, Salum Mwalimu amebainisha kile ambacho atakwenda kukifanya iwapo ataibuka mshindi.

Iringa. Mwalimu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chaumma, ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 19, 2025 alipozungumza na wananchi waliojitokeza kumsikiliza na kumdhamini stendi ya zamani Iringa Mjini.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, kifungu cha 33 (1) kinaeleza: Ili kuweza kuteuliwa kuwa mgombea halali wa kiti cha Rais, mtu anapaswa kudhaminiwa kwa maandishi na wadhamini walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa madhumuni ya uchaguzi chini ya sheria hii wasiopungua 200 kwa kila mkoa, angalau kwa mikoa 10 ya Jamhuri ya Muungano, kati ya hiyo angalau mikoa miwili kutoka Zanzibar.

Mwalimu amesema atakuwa rais anayevaa nguo za kazi zikiwemo jinsi, kapelo na tisheti badala ya kuvaa mavazi ya kiheshimiwa na kutulia Ikulu.

"Nichagueni kijana wa kazi, sitavaa suti, nitapiga kapelo, jinsi na tisheti, mtaa kwa mtaa kuchapa kazi," amesema.

Huku akishangiliwa, Mwalimu amesema; "Nitavaa suti siku ninaapishwa na siku ninapokea marais wenzangu ili nchi yetu isionekane ya watu wa hovyo," ameongeza.

Mwanasiasa huyo amesema Serikali yake kama atashinda urais ataunda Serikali ya wachapa kazi na kuondoa uzembe serikalini ili kujenga utumishi makini.

Akiwaomba wakazi wa Iringa kumdhamini ili apate uteuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mtiania mwenza wake wa urais, Devotha Minja amewataka kuenzi juhudi za Mtemi wa zamani wa mkoa huo, Mkwawa kwa kuondoa utawala wa CCM madarakani ili wapate maendeleo.

"Ndugu zangu wana Iringa nyie ni watu wa mapambano tangu enzi za Mkwawa, muenzini Mkwawa kwa kuondoa CCM madarakani mtuchague sisi tuwaletee maendeleo," amesema Minja ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chaumma-Bara.

Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu hizo ulifunguliwa na INEC Agosti 9 na utafungwa Agosti 27, 2025 siku ambayo utafanyika uteuzi wa waliokidhi.

Kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28 ni kipindi cha kampeni na Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ni shughuli ya upigaji kura.