Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NEMC yafunga viwanda viwili Mkuranga kwa kuhatarisha afya za wananchi

Muktasari:

  • Ukaguzi uliofanywa na NEMC umebaini uwepo wa moshi mzito, harufu kali na utiririshaji wa maji taka kwenye mazingira, huku moja ya viwanda vikidaiwa kukosa Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira na kuzuia wakaguzi kutekeleza majukumu yao.

Mkuranga. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limevifungia viwanda viwili katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani baada ya kubaini shughuli zake zinahatarisha afya za wananchi na kuchafua mazingira kutokana na kutofuata sheria na taratibu za mazingira.

Viwanda vilivyofungiwa ni SAN SHAN kinachojihusisha na uchakataji wa mafuta machafu (waste oil) na BAI-LY PAPER CO. LTD kinachozalisha karatasi za chooni ‘toilet paper’.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ukaguzi wa mazingira uliofanywa na timu ya NEMC ikiongozwa na Meneja wa Utekelezaji wa Sheria wa baraza hilo, Mhandisi Luhuvilo Mwamila.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Mwamila amesema kiwanda cha SAN SHAN kimekuwa kikizalisha moshi mzito na harufu kali kutokana na kukosa mfumo wa kudhibiti hewa chafuzi, hali inayohatarisha afya za wakazi wa maeneo yanayokizunguka.

Amesema pamoja na tatizo la hewa chafu, kiwanda hicho kimekuwa kikitiririsha maji taka yenye mafuta machafu kwenye mazingira, jambo lililosababisha uchafuzi mkubwa wa maeneo ya jirani.

“Tumebaini kuwa shughuli za kiwanda hiki zinaendelea bila kuwa na mifumo stahiki ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Hali hii siyo tu kwamba inaharibu mazingira, bali pia inaweka afya za wananchi katika hatari,” amesema Mhandisi Mwamila.

Aidha, amesema uchunguzi wa NEMC umebaini kuwa kiwanda hicho hakina Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM), huku mwekezaji wake akidaiwa kuwazuia mara kadhaa wakaguzi wa mazingira kutekeleza majukumu yao.

Kwa upande wa kiwanda cha BAI-LY PAPER CO. LTD, NEMC ilibaini kuwa kilikuwa kikitiririsha maji taka moja kwa moja kwenye mazingira, jambo lililosababisha uchafuzi unaoweza kuathiri afya za wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo.

Kutokana na ukiukwaji huo, NEMC ilishirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha ukaguzi na utekelezaji wa hatua za kuvifungia viwanda hivyo hadi vitakapotekeleza matakwa ya kisheria na kimazingira.

Mwamila amevitaka viwanda vyote nchini kuhakikisha vinafanya tathmini za athari kwa mazingira kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji, kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kushirikiana na wakaguzi ili kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.

Amesema NEMC itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji haziathiri ustawi wa wananchi na mazingira kwa ujumla.