NFRA yasisitiza uwajibikaji, ufanisi katika hifadhi ya chakula
Muktasari:
- Kwa mujibu wa NFRA, mifumo imara ya hifadhi ya chakula ni nguzo muhimu ya usalama wa chakula nchini, kwani huwezesha upatikanaji wa chakula kwa wakati, hupunguza athari za mishtuko ya uzalishaji na kusaidia kudumisha utulivu wa bei za nafaka sokoni.
Dodoma. Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya wamekutana jijini Dodoma kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wakala huo, wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi na kuongeza ufanisi wa utendaji ili kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Kikao hicho maalum kimelenga kupokea na kuchambua hatua zilizofikiwa katika shughuli za hifadhi ya chakula, pamoja na mikakati ya kuboresha mifumo ya akiba ya chakula ili kuhakikisha upatikanaji wake wakati wote, hususan katika kipindi ambacho nchi inaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na mzunguko usiotabirika wa uzalishaji wa mazao.
Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi, Balozi John Ulanga amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma ili NFRA iweze kutekeleza wajibu wake wa kulinda usalama wa chakula kwa Watanzania.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya hifadhi ya chakula zinasimamiwa kwa ufanisi na uwazi, ili akiba ya taifa iwe salama na ya kutosha kukidhi mahitaji wakati wa dharura,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi hiyo, Andrew Komba amesema kikao hicho kimejadili kwa kina utekelezaji wa shughuli za wakala huo, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika kusimamia hifadhi ya chakula nchini.
Wajumbe wengine walioshiriki kikao hicho ni Anthony Mtaka ambaye ni mkuu wa mkoa wa Njombe, Chabu Mishwaro, Tumaini Mbano, Obadia Kameya na Robinson Meitinyiku.
Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imeendelea kuimarisha maghala ya hifadhi ya chakula na kuongeza uwezo wa akiba ya taifa, hatua inayolenga kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha kwa matumizi ya ndani na msaada wa kibinadamu wakati wa majanga au uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa NFRA, mifumo imara ya hifadhi ya chakula ni nguzo muhimu ya usalama wa chakula nchini, kwani huwezesha upatikanaji wa chakula kwa wakati, hupunguza athari za mishtuko ya uzalishaji na kusaidia kudumisha utulivu wa bei za nafaka sokoni.