Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Osha yapata bodi mpya, Waziri atoa maelekezo mazito

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Osha.

Muktasari:

  • Bodi hiyo imetakiwa kuzingatia weledi, uwazi na uwajibikaji, kusimamia sera na mwelekeo wa taasisi ili kuendeleza mafanikio ya kulinda wafanyakazi.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Deus Sangu, ameizindua Bodi mpya ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), huku akiitaka kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kusimamia usalama na afya za wafanyakazi nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi ya saba ya Osha, Sangu amesema taasisi hiyo imekuwa miongoni mwa taasisi inafanya vizuri katika kutekeleza wajibu wake wa kulinda nguvu kazi ya Taifa kupitia usimamizi wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura Na. 297 Toleo la mwaka 2023.

Amesema Osha imekuwa mstari wa mbele kutoa miongozo na ushauri kwa waajiri na wamiliki wa sehemu za kazi kuhusu namna bora ya kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha afya za wafanyakazi.

“Osha ni miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri kwa sasa, hususan katika kutoa miongozo na ushauri kwa wamiliki wa sehemu za kazi juu ya uboreshaji wa mazingira yao na kuimarisha afya za wafanyakazi,” amesema Sangu.

Ameongeza kuwa juhudi za Osha zimeanza kuonekana wazi katika maeneo mbalimbali ya kazi, akitolea mfano taasisi za fedha na mashirika mengine ambayo yameanzisha programu za mazoezi kwa wafanyakazi wake.

“Wengi wetu tumeshuhudia siku za hivi karibuni mabenki na taasisi nyingine zikiendesha programu za mazoezi zinazolenga kuimarisha afya za wafanyakazi pamoja na kuongeza ari ya kazi. Haya ni matokeo ya ushauri wa wataalamu wa Osha baada ya tafiti zao kubaini changamoto za magonjwa yasiyoambukiza kwa wafanyakazi wengi,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akitoa ufafanuzi kuhusu vitendea kazi vilivyotolewa kwa wajumbe wapya wa Bodi ya Saba ya OSHA wakati wa hafla ya uzinduzi. Vitendea kazi hivyo ni pamoja na Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa taasisi, kitabu cha sheria pamoja na vifaa kinga (PPEs).

Sangu amesema bodi hiyo mpya imeanza kazi katika kipindi muhimu, wakati taifa likielekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Ilani ya Chama Tawala pamoja na Mpango Mkakati mpya wa Osha unaotarajiwa kuanza Julai mwaka huu.

Ameitaka bodi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia weledi, uwazi na maadili ya utumishi wa umma, huku akisisitiza wajikite zaidi katika kusimamia sera, maono na mwelekeo wa taasisi badala ya shughuli za kila siku ambazo ni wajibu wa menejimenti.


Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa bodi hiyo, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ushauri ya Osha, Makwaia Makani, amesema wamepokea jukumu hilo kwa uzito mkubwa na wako tayari kushirikiana na menejimenti kuisogeza mbele taasisi hiyo.

“Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru kwa imani uliyoonesha kwetu. Tunakuahidi tutafanya kazi kwa mshikamano, uwazi na uwajibikaji mkubwa ili kuhakikisha Osha inazidi kufikia mafanikio makubwa zaidi,” amesema Makani.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Osha Khadija Mwenda, amesema menejimenti ya taasisi hiyo imepokea kwa furaha kuanza kwa bodi mpya baada ya iliyopita kumaliza muda wake wa kisheria.

“Osha ina menejimenti imara inayofanya kazi kwa weledi na kujituma. Tupo tayari kupokea ushauri na maelekezo ya bodi mpya na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuijenga taasisi yetu,” amesema.

Wajumbe wa Bodi ya Saba ya Ushauri ya Osha ni Makwaia Makani ambaye ni Mwenyekiti, pamoja na Rehema Ludanga, Renatus Mbamilo, Mercy Sila na Lilian Francis.