Perterms yaibuka mshindi jukwaa la kimataifa la utawala bora
Mtendaji Mkuu wa Perterms Consultancy Limited, Shakibu Mussa Nsekela.
Dar es Salaam. Katika hatua inayoonesha kuongezeka kwa mchango wa wataalamu wa Kitanzania katika majukwaa ya kimataifa, kampuni ya Perterms Consultancy Limited imetangazwa mshindi wa Mpango wa Share My Story Initiative ulioandaliwa na Taasisi ya Basel Institute on Governance kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Sita wa Hatua za Pamoja (Collective Action).
Mpango huo ulilenga kutoa jukwaa kwa wataalamu na taasisi mbalimbali duniani kubadilishana uzoefu kuhusu namna ushirikiano wa wadau unavyoweza kuimarisha uwajibikaji, usimamizi wa hatari na uadilifu katika biashara na taasisi.
Ushindi huo wa Perterms umeelezwa kuwa si tu mafanikio kwa kampuni hiyo, bali pia ni ishara ya kuongezeka kwa mchango wa Tanzania katika mijadala ya kimataifa kuhusu utawala bora na ujenzi wa mifumo imara ya taasisi na biashara.
Perterms Consultancy Limited ni kampuni ya Kitanzania ya ushauri inayobobea katika utawala bora, usimamizi wa hatari, uzingatiaji wa sheria na kanuni, uchunguzi wa udanganyifu, uangalizi wa kina wa taasisi na miradi pamoja na urejeshaji wa mali.
Kampuni hiyo husaidia taasisi za sekta ya umma na sekta binafsi kuimarisha uwajibikaji, kudhibiti hatari na kuboresha utendaji kupitia suluhisho za kitaalamu zinazotegemea ushahidi wa kiutafiti na uzoefu wa vitendo.
Perterms imejijengea uzoefu kupitia ushirikiano na taasisi za sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wawekezaji katika kuimarisha mifumo ya utawala, kuongeza uwazi katika maamuzi ya biashara na kuimarisha uwezo wa taasisi kutambua na kudhibiti hatari kabla hazijaleta madhara makubwa.
Kampuni hiyo imesema ushindi huo umetokana na mchango wake wa muda mrefu katika kusaidia taasisi kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na kuongeza uwazi katika maamuzi ya kibiashara, hatua inayosaidia kupunguza hatari na kuongeza uendelevu wa taasisi.
Aidha, imeelezwa kuwa dhana ya Collective Actionimeendelea kuwa msingi muhimu duniani, ikisisitiza kuwa changamoto za kisasa katika biashara na maendeleo haziwezi kutatuliwa na taasisi moja pekee, bali zinahitaji ushirikiano wa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wadau wengine.
Katika mazingira ya sasa ya biashara yanayobadilika kwa kasi, maeneo ya Utawala Bora, Usimamizi wa Hatari na Uzingatiaji (GRC) yameendelea kuwa muhimu katika kuvutia uwekezaji na kujenga imani ya wadau.
Perterms imeeleza kuwa itaendelea kuchangia katika kukuza taaluma ya usimamizi wa hatari na utawala bora nchini Tanzania na nje ya mipaka yake, ikisisitiza kuwa uwekezaji katika mifumo hiyo si gharama, bali ni mkakati muhimu wa maendeleo na uendelevu wa taasisi na uchumi kwa ujumla.