Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ridhiwani awataka Wahitimu Kuchangamkia Ajira 45,000 za Serikali

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akihutubia wahitimu wakati wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Mtwara Mikindani.

Muktasari:

  • Ridhiwani Kikwete amewataka wahitimu nchini kujiandaa kuomba ajira 45,000 za Serikali zitakazotangazwa serikalini hivi karibuni, huku akisisitiza umuhimu wa wahitimu kuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mtwara. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka wahitimu nchini kujiandaa na kuchangamkia nafasi 45,000 za ajira zinazotarajiwa kutangazwa hivi karibuni katika kada mbalimbali za serikalini.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 43 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara, Juni 13, 2026 Ridhiwani amesema Serikali imepanga kujaza nafasi hizo katika mwaka wa fedha 2026/27 kufuatia kibali kilichotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kupunguza upungufu wa watumishi katika taasisi mbalimbali za umma.

Amesema ajira hizo zitahusisha sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, kilimo, uvuvi, uhandisi na huduma nyingine za umma, huku akiwahimiza vijana wenye sifa kufuatilia matangazo rasmi ya ajira na kuwasilisha maombi yao kupitia mifumo inayotambuliwa na Serikali mara tu nafasi hizo zitakapotangazwa.

“Vijana wenye sifa wanapaswa kufuatilia matangazo rasmi ya ajira na kuwasilisha maombi yao kupitia mifumo inayotambuliwa na Serikali mara tu nafasi hizo zitakapotangazwa,” amesema Ridhiwani.

Viongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakiongozwa na mgeni rasmi Ridhiwani Kikwete wakielekea ukumbini kwa ajili ya Mahafali ya 43 ya chuo hicho yaliyofanyika Mtwara.

Amesisitiza umuhimu wa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini kujiandaa kufanyakazi zitakazosaidia kutatua changamoto na kuleta tija kwa jamii na Taifa.

Aidha, amewapongeza wahitimu 1,926 waliohitimu katika ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada ya Kwanza kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu uliowasaidia kufikia mafanikio hayo.

Amesema Tanzania inapoelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inahitaji wataalamu wenye maarifa na umahiri wa kutekeleza maeneo mbalimbali ya kimkakati.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi amesema vyuo vya elimu ya juu vinapaswa kuhakikisha vinazalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira ili waweze kushindana na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakifuatilia mahafali ya 43 ya chuo hicho yaliyofanyika Mtwara Mikindani.

“Ni muhimu kwa vyuo vya elimu ya juu kuhakikisha vinazalisha wahitimu wenye uwezo unaoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira na maendeleo ya nchi,” amesema Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Utumishi

Naye Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho amesema mazingira ya sasa ya utumishi wa umma yanahitaji matumizi ya teknolojia za kidijitali, akili mnemba(AI) na mifumo ya kufanya maamuzi inayozingatia ushahidi wa kisayansi ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Kutokana na mahitaji hayo, amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimeboresha na kuandaa mitaala inayozingatia matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.