Russia yadai kulipiza kisasi Kyiv, mashambulizi yaua karibu 30
Kyiv. Russia imesema mashambulizi makubwa ya anga iliyoyafanya dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, yalikuwa ya kulipiza kisasi, yakilenga viwanda vya kijeshi na miundombinu inayohusiana na sekta ya ulinzi.
Mashambulizi hayo yaliyofanyika alfajiri ya Alhamisi yamesababisha vifo vya takribani watu 30, kujeruhi wengine 91 na kuharibu zaidi ya majengo 130, katika kile kinachotajwa kuwa shambulizi baya zaidi kulikumba jiji hilo mwaka huu.
Milipuko ilisikika katika maeneo mbalimbali ya Kyiv huku maelfu ya wakazi wakikimbilia kwenye maeneo ya kujikinga na mashambulizi, ikiwamo vituo vya treni ya chini ya ardhi. Vikosi vya uokoaji vya Ukraine vimesema idadi ya vifo imeendelea kuongezeka baada ya miili zaidi kupatikana chini ya vifusi, huku operesheni za utafutaji wa manusura zikiendelea.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alikatisha ziara yake nchini Ireland na kurejea Kyiv, ambako alitembelea moja ya majengo ya makazi yaliyoharibiwa.
Alisema kuchelewa kwa washirika wa Ukraine kutekeleza ahadi zao za kuipatia nchi hiyo mifumo ya ulinzi wa anga kumechangia ukubwa wa uharibifu uliotokea.
"Kama washirika wetu wangetekeleza ahadi zao kwa wakati, naamini tungeweza kuokoa nyumba na maisha zaidi. Tunachowaomba ni kutekeleza tulichokubaliana, si zaidi ya hapo," alisema Zelenskiy.
Rais huyo alisema pia kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga kutakuwa miongoni mwa ajenda muhimu katika mkutano ujao wa Nato, akisisitiza kuwa Ulaya inapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora ya balestiki.
Jeshi la Anga la Ukraine limesema Urusi ilirusha makombora 74 na droni 496 katika mashambulizi hayo ya usiku mmoja. Kwa mujibu wa jeshi hilo, idadi kubwa ya makombora ya balestiki pamoja na upungufu wa makombora ya mfumo wa Patriot uliifanya iwe vigumu kuyazuia mashambulizi hayo.
Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema operesheni hiyo ililenga viwanda vya kijeshi na miundombinu ya sekta ya ulinzi katika mji wa Kyiv na Mkoa wa Kyiv.
Moscow imedai maeneo yaliyolengwa ni pamoja na Kiwanda cha Redio cha Kyiv, Kampuni ya Radiyoniks na maghala yanayodaiwa kuhifadhi ndege zisizo na rubani pamoja na vipuri vyake. Aidha, imesema mashambulizi hayo yamevuruga uzalishaji wa mifumo ya makombora inayotumiwa na Jeshi la Ukraine.
Urusi imeeleza kuwa operesheni hiyo ilifanyika kujibu mashambulizi ambayo Ukraine imekuwa ikifanya dhidi ya miundombinu ya kiraia ndani ya eneo lake, ikidai baadhi ya makombora yaliyokuwa yakitengenezwa katika viwanda hivyo yalikuwa yakitumika kushambulia malengo ndani ya Russia.
Kuhusu uharibifu wa majengo ya makazi mjini Kyiv, Moscow imekanusha kuyashambulia moja kwa moja na kudai sehemu ya uharibifu huo ulisababishwa na makombora ya ulinzi wa anga ya Ukraine yaliyoshindwa kufikia malengo yake na kulipuka angani.
Hata hivyo, Ukraine na washirika wake wa Magharibi wameendelea kusisitiza kuwa mashambulizi ya Urusi yamelenga na kuathiri maeneo ya kiraia, huku pande hizo zikiendelea kutoa maelezo yanayokinzana kuhusu chanzo na athari za mashambulizi hayo.