Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Salum Mwalimu: Chagua kiongozi anayefaa, msipige kura kwa mazoea

Muktasari:

  • Katika kampeni yake Babati, amewataka wananchi wajitathmini juu ya utekelezaji wa ahadi za viongozi wa sasa, ikiwemo elimu, huduma za msingi na maendeleo.

Manyara. Wakati Watanzania wakijiandaa kufanya uamuzi Oktoba 29, 2025, kuchagua viongozi wanaowataka, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amewataka Watanzania kuachana na tabia ya kupiga kura kwa ushabiki na mazoea, badala yake wachague viongozi wenye maono ya kweli ya kuwakomboa kutoka kwenye umaskini.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Magugu, Wilaya ya Babati Vijijini, akitokea Babati Mjini kuelekea Karatu, Mwalimu amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa ya uchaguzi mkuu huo kufanya uamuzi wa busara kwa kutathmini ahadi zilizotolewa miaka mitano iliyopita na utekelezaji wake.

“Unapigiwa kura ili uboreshe elimu, huduma za maji, umeme, pembejeo na masoko ya mazao, lakini miaka mitano inaisha hakuna kilichofanyika. Watu wanabaki maskini, viongozi wanabaki ofisini,” amesema Mwalimu.

Amesisitiza kuwa kura ni mkataba rasmi kati ya wananchi na Serikali, hivyo kabla ya kupiga kura kila mmoja ajitathmini kiwango ambacho viongozi waliopo madarakani wamejibu changamoto zao, ikiwemo hali ya elimu, huduma za msingi na maendeleo ya kiuchumi.

Akiendelea na ziara yake ya kampeni kutoka Babati Mjini kuelekea Karatu, Mwalimu amesema Chaumma kimejipanga kuleta mageuzi makubwa ya kiutawala kwa kubadili sera na sheria kwa manufaa ya wananchi.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema, amesema hoja zinazotolewa dhidi ya mgombea huyo kuhusu umri wake hazina mashiko na kuwataka wananchi wampime kwa sera na ahadi zake.

“Kuna nchi zimepiga hatua kubwa kwa kuwaamini vijana. Tunachowaomba Watanzania ni kumpima Mwalimu kwa sera zake. Ameshajipanga, ana dira, na anaifahamu Tanzania na changamoto zake,” amesema Mrema.

Kwa mujibu wa viongozi hao, endapo Chaumma kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitaweka misingi ya utawala bora, uwajibikaji na maendeleo kwa wote, kikilenga kubadilisha hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida.