Samia ageukia uzalishaji umeme akiutaja ushirika
Muktasari:
- Hadi sasa Tanzania inazalisha umeme wa megawati 4,000 kutokana na vyanzo vya maji na gesi huku Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ukiongeza sehemu kubwa ya umeme baada ya ujenzi wake kukamilika na mitambo kuwashwa
Iringa. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuongeza uzalishaji wa umeme nchini hadi kufikia megawati 8,000 ili kuchechea maendeleo ya Taifa.
Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Septemba 7, 2025 alipozungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Iringa Mjini, ukiwa ni mkutano wake wa mwisho katika Mkoa wa Iringa.
Ahadi hiyo imetolewa na mgombea huyo baada ya wagombea ubunge katika mkoa huo kueleza kazi zilizofanywa na Serikali ya kuunganisha umeme kwenye vijiji vyote katika majimbo yao huku vikiwa vimebakia vitongoji vichache ambavyo havijafikishiwa umeme.
Hadi sasa Tanzania inazalisha umeme wa megawati 4,000 kutokana na vyanzo vya maji na gesi huku Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ukiongeza sehemu kubwa ya umeme baada ya ujenzi wake kukamilika na mitambo kuwashwa.
Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni, Samia amesema wanajipanga kuhakikisha umeme unakuwa kichocheo cha maendeleo ya Taifa na unasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
"Pamoja na kuunganisha umeme mijini, vijijini na vitongojini, tuna kazi ya kuongeza uzalishaji wa umeme ili uweze kutosha. Tumetoka megawati 1,600, tumefikisha megawati 4,000, na sasa tunajipanga kufikisha megawati 8,000 tukitumia vyanzo mbalimbali anuai ikiwamo upepo na joto ardhi.
"Tunategemea kupata umeme mwingi wa upepo na joto ardhi katika ukanda huu (nyanda za juu kusini). Kwa hiyo, tumejipanga vema ili umeme uwe msingi au kichocheo cha maendeleo ya nchi yetu," amesema Samia wakati akiomba kura kwa wananchi wa Iringa.
Nafasi ya ushirika nchini
Samia amesema Serikali imechukua hatua ya kufufua ushirika nchini, lengo likiwa ni kuwezesha kuifikia mikopo na kuwatafutia wakulima wao pembejeo za kilimo.
"Tumejipanga kuvilea vyama vya ushirika katika nchi yetu, lengo ni kumwinua mkulima na kuhakikisha wakulima wanafaidi jasho lao," amesema mgombea huyo.
Amesisitiza ushirika unahitaji watu wenye weledi na uwazi watakaouendesha kwa kutumia teknolojia, ukilenga kuondoa mianya ya ubadhirifu wa mali zake.
"Tunataka kujenga Tanzania yenye uchumi jumuishi na ustawi kwa watu wote," amesema Samia.
Ujenzi Machinga Complex
Samia amesema aliahidi kujenga soko la machinga Iringa, sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga Machinga Complex mjini Iringa ili mamalishe na wafanyabaiashara wadogo maarufu wamachinga, wafanye shughuli zao katika mazingira mazuri.
Wagombea ubunge wampongeza
Mgombea ubunge wa viti maalumu, Nancy Nyalusi amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo na kubalidisha maisha yao.
"Tumepokea fedha nyingi hapa Iringa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile maji, barabara na afya, tunakupokeza kwa kazi hiyo nasi tutakulipa kwa kura nyingi za ushindi," amesema.
Rose Tweve, mgombea ubunge wa viti maalumu katika mkoa huo, amesema Iringa imepokea Sh13 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu na hadi sasa fedha hizo zimevinufaisha vikundi 380.
Amesema mkoa huo pia umepokea mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, jambo ambalo litamfanya apate kura nyingi kutoka kwa wananchi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mgombea ubunge katika Jimbo la Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe amesema barabara nyingi zimejengwa katika jimbo lake, huduma za afya zimeboreshwa na shule zimejengwa katika kata zote kwenye jimbo lake.
Rita Kabati ambaye ni mgombea ubunge katika Jimbo la Kilolo, amesema wanatambua jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya CCM katika kupunguza vifo vya mama na mtoto; na Kilolo wamejengewa hospitali mbili na vituo vya afya vinne.
"Kwenye suala la maji, Kilolo sasa inapata maji kwa asilimia 80, imeokoa ndoa zetu...nitakwenda kusimamia miradi inayoendelea ili tuhakikishe tunamalizia asilimia 20 zilizosalia," amesema Kabati.
Ameomba kuwe na barabara ya mchepuko kwenye eneo la Kitonga ili kufungua na maeneo mengine ya Kilolo na kuunganisha Mkoa wa Iringa na Morogoro.
Mgombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo amesema kwenye sekta ya afya, Serikali imeimarisha upatikanaji wa matibabu ya kibingwa na kwamba hadi sasa huduma za usafishaji wa figo unafanyika mkoani humo.
"Umetujengea uwanja wa ndege wa Iringa, uwanja huu umerahisisha usafiri kwa wananchi wa Iringa, sasa mashirika ya ndege yanatua katika uwanja huu," amesema mgombea huyo.