Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Selcom yazindua suluhisho la miamala nafuu kwa biashara

Dar es Salaam. Wakati wafanyabiashara wengi nchini wakilalamikia gharama kubwa za miamala zinazopunguza faida na kuongeza gharama za uendeshaji wa biashara, Selcom Microfinance Bank imekuja na suluhisho jipya ikizindua mfumo wa kidijitali unaolenga kushusha gharama hizo hadi kufikia Sh100 kwa muamala mmoja.

Mfumo huo unaoitwa Selcom Business umeundwa kuwahudumia wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), kampuni pamoja na watengenezaji wa mifumo ya kidijitali (developers), ukiwawezesha kufanya miamala kwa gharama nafuu, kusimamia fedha zao kwa wakati halisi na kuunganisha mifumo yao moja kwa moja na benki kupitia API bila gharama za ziada.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam leo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Selcom Microfinance Bank, Aloyse Maro, alisema gharama za kufanya miamala zimekuwa moja ya changamoto zinazopunguza ufanisi na faida ya biashara nyingi nchini.

"Muda na gharama za kufanya miamala zina athari kubwa kwa ufanisi na faida ya biashara. Kupitia Selcom Business, wateja wanaweza kujisajili kwenye bando la kila mwezi na kufanya miamala kwa gharama ya kuanzia Sh100 kwa muamala, bila kikomo cha idadi ya miamala," alisema Maro.

Alisema mfumo huo unatoa mabando matatu ya matumizi ambayo ni Bando Poa, Bando Bomba na Bando Max, ambapo kadri mfanyabiashara anavyochagua bando kubwa zaidi ndivyo gharama ya kila muamala inavyopungua.

Kwa mujibu wa benki hiyo, wateja wa Bando Max watakuwa wakilipa Sh100 kwa kila uhamisho wa fedha kwenda benki zote za ndani, mitandao ya simu na wafanyabiashara wanaotumia TanQR kwa miamala ya hadi Sh20 milioni, huku idadi ya miamala inayoweza kufanywa ikiwa haina kikomo ndani ya kipindi cha usajili.

Mbali na kupunguza gharama za miamala, Selcom Business pia inalenga kuondoa changamoto ya muda mrefu ambayo biashara zimekuwa zikikumbana nayo ya kuunganisha mifumo yao na taasisi za kifedha.

Maro alisema tofauti na utaratibu wa awali uliokuwa ukihitaji makubaliano mbalimbali, ada za uunganishaji na kusubiri kwa muda mrefu, sasa biashara zinaweza kujisajili zenyewe, kupata API credentials kupitia dashboard na kuanza kufanya miamala ndani ya saa chache bila kulipa ada ya matumizi ya API.

"Tumerahisisha uunganishaji wa API kwa mfumo wa kujihudumia, unaowezesha biashara kuunganisha mifumo yao na benki kwa haraka, kwa urahisi na bila vikwazo," alisema.

Aidha, mfumo huo unawezesha waajiri kulipa mishahara ya wafanyakazi na kufanya malipo ya makundi kwa hatua chache, huku ukitoa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha kwa wakati halisi, stakabadhi za kidijitali na viwango tofauti vya ruhusa kwa watumiaji kulingana na majukumu yao ndani ya biashara.

Benki hiyo inaeleza kuwa huduma hiyo inalenga kusaidia biashara kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza uwazi katika usimamizi wa fedha na kuharakisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika shughuli za kila siku za biashara nchini.