Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaimarisha utalii, yavuta wageni zaidi duniani

Mkurugenzi wa Utalii nchini, Dk Theresa Nkobi (kulia), akiongozana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo, wakitembelea mabanda mbalimbali katika Maonyesho ya Utalii ya Karibu Kilifair yanayoendelea katika Viwanja vya Magereza, jijini Arusha.

Muktasari:

  • Tanzania imeendelea kuvutia watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani kutokana na juhudi za Serikali kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii, kuboresha miundombinu na kuendeleza uhifadhi wa rasilimali za asili, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Arusha. Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika soko la utalii duniani baada ya kuongeza ushirikiano wa kibiashara na kuvutia idadi kubwa ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa, maeneo ya kihistoria na vivutio vingine vya asili.

Mkurugenzi wa Utalii nchini, Dk Thereza Nkobi amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali katika kuitangaza Tanzania kimataifa, kuboresha miundombinu na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za utalii.

Akizungumza jana wakati akifungua Maonyesho ya Kimataifa ya Karibu Kilifair jijini Arusha, Dk Nkobi amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika sekta ya utalii ikilinganishwa na baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki.

"Maonyesho haya yameendelea kukuza ushindani wa Tanzania katika ramani ya utalii duniani huku sekta ya utalii ikiendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa na mapato ya fedha za kigeni," amesema.

Amesema Karibu Kilifair imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii, utamaduni na huduma mbalimbali zinazotolewa na wadau wa sekta hiyo, jambo linaloifanya Tanzania kuendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Dk Nkobi, maonyesho hayo pia yanatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani kuonyesha bidhaa na huduma zao, hali inayochochea ajira, uwekezaji na ukuaji wa biashara zinazotegemea sekta ya utalii.

Amesema maonyesho hayo yanatarajiwa kuchangia juhudi za Serikali kufikia lengo la kupokea watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.

Kwa sasa, amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP) na kutoa ajira zaidi ya milioni 2.5, huku mapato yatokanayo na shughuli za utalii yakiendelea kuongezeka.

Dk Nkobi amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika uhifadhi wa rasilimali za utalii, uboreshaji wa miundombinu, utoaji wa huduma bora na kuongeza kampeni za kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema maonyesho hayo yanaendelea kuwa jukwaa la kuwaunganisha wadau wa sekta ya utalii, wawekezaji, wanunuzi wa huduma za utalii na washirika wa biashara kutoka mataifa mbalimbali.

Awali, Mkurugenzi wa Kilifair Promotion, Dominic Shoo alisema maonyesho hayo yameendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara zinazohusiana na sekta ya utalii.

Alisema mataifa 50 yanashiriki maonyesho hayo ya siku tatu na kwamba wanatarajia kupokea wageni zaidi ya 20,000 watakaotembelea maonyesho hayo kutafuta fursa za uwekezaji na kubadilishana uzoefu wa kibiashara.

"Hii ni fursa ya kipekee kwa wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi kuimarisha biashara zao. Pia wafanyabiashara wanaochipukia wanapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao wenye uzoefu mkubwa katika sekta hii," alisema Shoo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Wilbroad Chambulo alisema maonyesho hayo yana mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Hata hivyo, aliiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya utalii ili kurahisisha usafiri wa watalii na wadau wa sekta hiyo.

"Miundombinu ya usafiri wa anga imeimarika kwa kiwango kikubwa, lakini bado kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha mtandao wa barabara katika maeneo ya utalii. Pia wadau wanapaswa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo," alisema Chambulo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii Zanzibar, Dk Tabia Mwita alisema sekta ya utalii imeendelea kuimarika visiwani Zanzibar kutokana na ongezeko la watalii na juhudi za kuitangaza Zanzibar katika masoko ya kimataifa.

Alisema ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kuzaa matunda, hali inayoongeza mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya kiuchumi ya pande zote mbili za Muungano.