Sh13.2 milioni zatumika kujenga vimbweta chuo kikuu cha Kikatoliki Mwenge
Meneja wa NMB kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus na baadhi viongozi wa chuo kikuu cha kikatoliki cha Mwenge, wakikata utepe kwenye vimbweta vilivyojengwa na benki hiyo.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Ujenzi wa vimbweta hivyo, uliogharimu zaidi ya Sh13.2 milioni, utaboresha mazingira ya kujisomea na kujifunzia kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Moshi. Katika jitihada za kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini, Benki ya NMB imefadhili ujenzi wa vimbweta vinne kwa gharama ya zaidi ya Sh13.2 milioni katika Chuo kikuu cha kikatoliki Mwenge, mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya mchango wake wa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo leo, Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuboresha huduma za kijamii, hususan elimu, kwa kuwa ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Amesema vimbweta hivyo vitawawezesha wanafunzi kupata sehemu salama na rafiki kwa ajili ya kujisomea, kufanya mijadala ya kitaaluma na kazi za vikundi nje ya madarasa.
"Leo tupo Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge kuungana na wanafunzi na uongozi wa chuo kukabidhi vimbweta hivi. Tunaamini wanafunzi wanapopata mazingira mazuri ya kujisomea na kufanya mijadala ya kitaaluma, huongeza uelewa wao na kuboresha matokeo ya masomo," amesema Meneja huyo
Aidha, ameongeza kuwa NMB ina ushirikiano wa muda mrefu na taasisi mbalimbali za elimu nchini na imekuwa ikiwekeza katika miradi inayoboresha mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa maeneo ya kujisomea na kuunga mkono ubunifu wa wanafunzi kupitia programu mbalimbali za kiteknolojia.
Pamoja na mambo mengine, amesema kupitia NMB Foundation, benki hiyo pia inatekeleza programu ya Nuru Yangu, inayowezesha wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kupata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha kikatoliki Mwenge, mkoani Kilimanjaro wakijisomea kwenye vimbweta ambavyo vimejengwa na Benki ya NMB.
"Programu hii huwasaidia wanafunzi wenye ufaulu mzuri kwa kulipiwa ada, kupewa fedha za kujikimu pamoja na vifaa vya kujifunzia katika kipindi chote cha masomo yao chuoni," amesema
Kwa upande wake, Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Johnviane Nyikizeha, ameishukuru NMB kwa ufadhili huo, akisema umeongeza fursa za wanafunzi kupata mazingira bora ya kujisomea na kujifunzia.
"Idadi ya wanafunzi inaendelea kuongezeka hapa chuoni, hivyo vimbweta hivi vitasaidia wanafunzi wengi zaidi kupata sehemu tulivu ya kujisomea na kufanya kazi za vikundi. Vile vilivyokuwepo havikuwa na paa, hivyo vilikuwa haviwafai wanafunzi wakati wa jua au mvua," amesema Nyikizeha
Naye, mwanafunzi wa chuo hicho, Viviance Konga, amesema mradi huo utaboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ari ya wanafunzi katika masomo yao kwa kuwa awali walikuwa wakisomea juani.
"Tunaishukuru Benki ya NMB kwa kutuwezesha kupata sehemu tulivu na salama ya kujisomea. Mazingira haya yatatusaidia kuongeza maarifa na kufanya vizuri zaidi katika masomo yetu," amesema.
Mwanafunzi mwingine, Neema Lazaro, amesema hapo awali walikuwa wakitumia vimbweta vilivyochakaa na visivyo na paa, hali iliyowalazimu kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.
"Vimbweta hivi vipya vina ubora mkubwa. Sasa tunaweza kujisomea bila kuathiriwa na jua au mvua, jambo ambalo litatuongezea utulivu na ufanisi katika masomo yetu," amesema.