Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh600 milioni kuondoa msongamano wa shule na zahanati Geita

Geita.Kampuni ya Buckreef Gold imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Halmashauri ya Wilaya ya Geita baada ya kusaini makubaliano ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) yenye thamani ya Sh600 milioni, yakilenga kuboresha huduma za afya, elimu, maji na usafi wa mazingira kwa jamii zinazoishi maeneo yanayozunguka mgodi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, ameipongeza Buckreef Gold kwa kutekeleza miradi ya jamii kwa kuzingatia sheria na mipango ya Serikali. Alisema kampuni hiyo imekuwa ikipanga, kutenga bajeti na kutekeleza miradi ya CSR kwa nidhamu, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuona matokeo ya moja kwa moja kupitia maboresho ya shule, vituo vya afya na huduma za maji.

Shigella amesema mkoa wa Geita, hususan maeneo ya uchimbaji madini, unaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya watu kutokana na shughuli za kiuchumi, hali inayoongeza shinikizo kwa huduma za umma. Alitaja kata ya Rwamgasa yenye zaidi ya wakazi 60,000 kuwa miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya zahanati kuzidiwa na wagonjwa, uhaba wa madarasa, miundombinu ya vyoo na upatikanaji wa maji safi.

Amesema miradi mipya ya CSR imebuniwa kujibu changamoto hizo, ambapo katika sekta ya elimu, ujenzi wa madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Isunganghoro na uboreshaji wa miundombinu Shule ya Msingi Lubanda unalenga kupunguza msongamano, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi.

Katika sekta ya afya, Buckreef Gold itawekeza katika ujenzi na uboreshaji wa zahanati za Rwamgasa, Lubanda na Ibisabageni, ikiwemo wodi, nyumba za watumishi, mifumo ya maji na vyoo. Hatua hiyo inalenga kuboresha huduma kwa wagonjwa na kuimarisha mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya, huku makazi ya watumishi yakiongeza uendelevu wa huduma na mwitikio wa dharura.

Miradi ya maji na usafi wa mazingira, ikiwemo ujenzi wa kisima cha maji safi katika Zahanati ya Lubanda, inalenga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji, hususan wakati wa kiangazi, na kusaidia kudhibiti maambukizi pamoja na kuboresha huduma za mama na mtoto.

Meneja Mkuu wa Buckreef Gold, Isaac Bisansaba, amesema kampuni inaona uwekezaji wa kijamii kuwa sehemu ya wajibu wake wa msingi. “Shughuli zetu zinafanyika ndani ya jamii. Kadri uzalishaji unavyoongezeka, ndivyo wajibu wetu kwa jamii unavyoongezeka. Miradi hii inalenga maeneo yenye athari ya moja kwa moja kwa familia—afya, elimu na maji,” amesema.

Mbali na miradi ya CSR, Buckreef Gold pia imekuwa ikichangia uchumi wa Geita kupitia ajira na ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wazawa. Ajira mgodini, alisema Bisansaba, huziwezesha familia kukidhi mahitaji ya msingi na kuimarisha ustawi wa kaya, huku manunuzi ya ndani yakichochea ukuaji wa biashara na ajira zaidi.

Mwaka uliopita, kampuni hiyo iliwekeza Sh420 milioni katika miradi ya CSR ikiwemo ujenzi wa madarasa, ukamilishaji wa vituo vya afya na uboreshaji wa barabara zilizorahisisha usafiri wakati wa msimu wa mvua. Tangu kuanza kwa shughuli za mgodi, jumla ya Sh1.86 bilioni zimewekezwa katika miradi ya maendeleo ya jamii mkoani Geita.

Buckreef Gold inaendeshwa kupitia ubia kati ya TRX Gold Corporation na Shirika la Madini la Serikali (STAMICO), muundo unaochanganya utaalamu wa kimataifa na ushiriki wa Serikali ili kuhakikisha uwekezaji wa jamii unaendana na vipaumbele vya kitaifa na mipango ya maendeleo ya wilaya.