Prime
Shughuli imeiva urais Tanzania 2025
Muktasari:
- Mchakamchaka wa kuchukua fomu za uteuzi waanza kuelekea Oktoba 29, 2025 ambapo wapigakura milioni 37.6 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura watatumia haki yao ya kuchagua Rais, wabunge na madiwani.
Dar/Dodoma. Mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 umefikia patamu baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupuliza kipenga cha uchukuaji fomu za uteuzi kwa wagombea.
Dimba limefunguliwa leo Agosti 9, likianzia na wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kuwa cha kwanza kuchukua fomu, kikifuatiwa na NRA.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi ya INEC, kuanzia leo Agosti 9 hadi Agosti 27, 2025 ni uchukuaji fomu za uteuzi kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, wakati Agosti 14 – 27, 2025 itakuwa ni uchukuaji fomu za uteuzi kwa wagombea ubunge na udiwani.
Baada ya kujaza fomu na kuzirejesha, Agosti 27, 2025 saa 10 jioni itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais, Makamu wa Rais, wabunge na madiwani, tayari kwa kuanza kampeni Agosti 28. Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba 29, 2025.
Baadhi ya vyama vya siasa tayari vimekamilisha mchakato wa ndani wa kuwapata wagombea urais, hivyo wagombea wake wako kwenye foleni ya kwenda kuchukua fomu za uteuzi kwenye ofisi za INEC jijini Dodoma.
Wagombea urais na wagombea wenza waliopitishwa mtawalia pamoja na vyama vyao kwenye mabano ni Samia Suluhu Hassan na Dk Emmanuel Nchimbi (CCM), Salum Mwalimu na Devotha Minja (Chaumma), Luhaga Mpina na Fatma Alhabib Ferej (ACT Wazalendo).
Wengine wanaogombea urais Hassan Almas (NRA), Kunje Ngombale-Mwiru (AAFP), Yustus Rwamugira (TLP), Hassan Doyo (NLD), Wilson Elias (ADC), Georges Busungu (Ada Tadea), Haji Khamisi (NCCR-Mageuzi) na Majaliwa Kyara (SAU).
Vilevile, wamo David Mwaijolele (CCK), Mwajuma Mirambo (UMD), Coaster Kibonde (Demokrasia Makini) na Twalib Kadege (UPDP).
Ratiba INEC
Tume jana ilitoa ratiba ya awali ya mchakato wa uchukuaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea urais wa vyama vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima ilisema hadi sasa vyama vya siasa 14 ndivyo vilivyopeleka barua na kuainisha tarehe na muda, ambao wanachama wao wanaowania kiti cha Rais na Makamu wa Rais wamependekeza kuchukua fomu.
“Tume imeviandikia barua vyama vya siasa husika kuvijulisha kuhusu ratiba ya utoaji wa fomu za uteuzi. Ni Muhimu tukumbuke ratiba hii inahusu vyama 14 pekee vilivyowasilisha taarifa hadi leo Agosti 8, hivyo iwapo vyama vingine vitajitokeza tutaandaa ratiba husika,” amesema Kailima.
Amesema vyama ambavyo watiania wake watafika ofisi za Tume zilizopo Njedengwa jijini Dodoma leo Agosti 9, 2025 kuchukua fomu za uteuzi ni CCM saa 5:00 asubuhi na NRA saa 8:00 mchana.
“Agosti 9 saa 10:00 jioni itakuwa zamu ya Chama cha AAFP na kesho Agosti 10 saa 3:00 asubuhi Demokrasia Makini; saa 6:00 mchana NLD na saa 9:00 alasiri UPDP.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Jumatatu Agosti 11 saa 3:00 asubuhi itakuwa Ada Tadea, saa 6:00 mchana UMD na saa 9:00 alasiri ni TLP,” ameeleza.
Kailima amesema Jumanne Agosti 12 saa 3:00 asubuhi itakuwa zamu ya Chama cha CCK, saa 9:00 alasiri ADC, Agosti 13 saa 3:00 asubuhi itakuwa zamu ya DP wakati Agosti 15, itakuwa zamu ya NCCR-Mageuzi ambayo wagombea wake watachukua fomu saa 6:00 mchana.
Fungua dimba
Wakati INEC ikieleza hayo, CCM imesema Rais Samia, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho atachukua fomu kutetea kiti hicho leo kisha kuzungumza na makada wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema Rais Samia ataambatana na mgombea mwenza wake, Dk Nchimbi.
“Baada ya kuchukua fomu, atarejea kwenye ofisi za chama hapa makao makuu Dodoma na atapata fursa ya kusaini kitabu na kusalimiana na wana-CCM ambao tumewakaribisha kwa ajili ya tukio hilo,” alisema.
Makalla alisema ratiba ya kuchukua fomu kwa wagombea ubunge itaanza Agosti 14, baada ya mchakato wa ndani ya chama kukamilika kwa wale watakaoteuliwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Nje ya jengo la makao makuu ya CCM, shughuli mbalimbali zinaendelea, ikiwemo ujenzi wa jukwaa maalumu litakalotumiwa baada ya uchukuaji fomu za urais.
Vyama vingine
Baadhi ya viongozi na watiania wa Urais na makamu wa Rais waliozungumza na Mwananchi jana, walisema wapo mguu sawa kwa ajili ya mchakato huo wa kuanza safari ya kushika baada ya Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa ADC, Shaban Itutu amesema kila kitu kinakwenda vizuri na siku moja kabla ya kuchukua fomu wataanza safari kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
“Tutaanzia safari Dar es Salaam tukiambatana na mgombea wetu, tutakuwa tukisimama sehemu mbalimbali kumtambulisha mgombea,” amesema.
Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai amesema: “Maandalizi yote yanakwenda vizuri, tunasubiri tarehe husika tukachukue fomu.”
Mgombea urais wa NLD, Doyo Hassan Doyo amesema yeye na mgombea mwenza wake, Chausiku Khatib Mohamed, watakwenda kuchukua fomu Agosti 9.
“Ratiba iko vizuri kwa sababu uteuzi ni Agosti 27, kwa hiyo kuanzia Agosti 10 hadi Agosti 27 kuna siku 17, zinatosha kutafuta wadhamini,” amesema Doyo akiongeza kuwa tayari yuko Dodoma kwa ajili ya shughuli hiyo.
CUF mguu sawa
Wakati vyama hivyo vikijiandaa kuchukua fomu za urais za INEC, Chama cha Wananchi (CUF) kimewateua makada wawili watakaopigiwa kura kwenye mkutano mkuu Agosti 9, 2025 ili kumpata mmoja wa kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya Rais.
Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza majina ya watiania waliojitokeza katika chama hicho jana, kuwa ni Mkunyutila Siwale na Samandito Gombo.
Kwa urais wa Zanzibar, amesema Kamati ya Uongozi ya chama hicho imewapitisha Habib Mohammed, Masoud Hamad na Mohamed Khatib.
Amesema wagombea wawili wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watatu wa urais wa Zanzibar, watapigiwa kura katika mkutano mkuu kesho jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba amesema katika mkutano huo mkuu, chama hicho kitazindua ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030, sambamba na kupitisha majina ya watiania wa nafasi ya ubunge.