Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sura mpya washindi viti maalumu vyuo vikuu

Muktasari:

  • Sura mpya zimeibuka kidedea katika matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa viti maalumu kwa kundi la vyuo vikuu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Dar es Salaam. Uchaguzi wa watiania wa ubunge wa viti maalumu kwa makundi mbalimbali ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) umekamilika, huku sura mpya zikiibuka kidedea katika matokeo ya awali.

Katika kundi la viti maalumu vyuo vikuu, washindi ni Selina Kingalame aliyepata kura 562, akifuatiwa na Asha Feruzi kura 495, kisha Dk Regina Malima aliyepata kura 268, huku Zeyana Abdallah Hamid akishinda upande wa Zanzibar kwa kura 426.

Wanne hao wote ni sura mpya katika nafasi hiyo, ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na Dk Pauline Nahato, Dk Christine Ishengoma na Dk Tea Ntala.

Kwa matokeo hayo, makada hao wanasubiri vikao vya juu vya CCM kuwathibitisha katika nafasi hizo, ili wapate uhalali wa kuingia bungeni pale litakapoanza.

Matokeo hayo yametangazwa leo, Jumapili Agosti 3, 2025, baada ya kufanyika uchaguzi wa makundi hayo jijini Dodoma jana.

Kundi hilo la vyuo vikuu, lililokuwa na wagombea 10, wengine ni Dk Sarah Chiwambwa aliyepata kura 227, Dk Siriel Mchembe (208), Profesa Neema Kumburu (150), Dk Benadetha Rushahu (127), Dk Agnetha Mhenga 9110), Vaileth Lusana (94) na Dk Philipina Shayo (39).

Kwa upande wa kundi la wafanyakazi, washindi ni Halima Nassor aliyepata kura 566 na Mariam Mungula kura 290, huku Tunu Juma Kondo akishinda upande wa Zanzibar kwa kura 556.

Katika kundi hilo lililokuwa na wagombea wanane, wengine ni Rizik Kingwale aliyepata kura 280, Janeth Mnyaga (210), Beng’I Issa (198), Marry Mbagata kura (122), Silpha Kapinga (99) na Alice Kaijage (81).

Magreth Ezekiel na Rahma Kisuo wameshinda viti maalumu kwa kundi la taasisi zisizo za kiserikali kwa kura 668 na 350, huku Mgeni Hassan Juma akishinda upande wa Zanzibar kwa kura 302.

Kundi hilo lilikuwa na wagombea wanane na wengine ni Asha Baraka (205), Neema Lugangira (129), Halima Mpinge (82), Pili Missanah (31), Irene Ishengoma (28) na Marcelline Mbogo nane.