Prime
Wajumbe wawatwisha kero lukuki wagombea
Muktasari:
Ubovu wa barabara, ukosefu wa ajira, migogoro ya ardhi, kukosekana kwa miundombinu ya madaraja na vivuko pamoja na malisho ya mifugo ni baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wakati watiania wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakijitambulisha.
Dar/mikoani. Ubovu wa barabara, ukosefu wa ajira, migogoro ya ardhi, kukosekana kwa miundombinu ya madaraja na vivuko pamoja na malisho ya mifugo ni baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wakati watiania wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakijitambulisha.
Watiania hao wa nafasi za ubunge na udiwani wamezunguka kwenye majimbo na kata wanazotaka kuziongoza wakijitambulisha na kuwaomba wajumbe wawachague ili wakiwakilishe chama chao kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Katika mikutano iliyofanyika kwenye ngazi ya kata, wajumbe walipata nafasi ya kutoa maoni yao na kuuliza maswali ambapo katika maeneo mengi, changamoto hizo zimeibuliwa na wajumbe katika maeneo husika.
Hata hivyo, watinia hao walipata fursa ya kujibu hoja hizo na kueleza namna watakavyokabiliana na changamoto hizo endapo watapewa nafasi ya kugombea ubunge na udiwani katika maeneo wanayotaka kuyawakilisha.
Katika maeneo mbalimbali nchini, wajumbe wamewabana wagombea hao wakitaka kupata undani wa jinsi watakavyozishughulikia ili kuboresha maisha yao. Kujitambulisha huko kuanzia Julai 30, 2025.
Kesho, Agosti 3, 2025 ndiyo mwisho wa watiania hao kujitambulisha kwa wajumbe na siku itakayofuata, Agosti 4, 2025, wajumbe watapiga kura kumchagua mwakilishi mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye jimbo na kata.
Baada ya kukamilika kwa mchakato huo, washindi watakaopatikana kwenye kura ya maoni, watakwenda kushindana na vyma vingine kwenye uchaguzi baada ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo itaanza mchakato huo Agosti 14 – 27, 2025.
Huduma za afya Iringa
Wajumbe katika Jimbo la Iringa Mjini wamewahoji watiania kuhusu namna watakavyotatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku hususan kero za afya, migogoro ya ardhi, ukosefu wa ajira na ubovu wa barabara.
Wajumbe pamoja na wananchi wamehoji hayo kwenye mkutano wa watiania hao kujitambulisha iliyofanyika katika kata za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kuomba kura kwa nafasi ya ubunge na udiwani.
Mkazi wa Kata ya Makorongoni mkoani humo, Asifiwe Chang’a amelalamikia uhaba wa dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Iringa huku akihoji kwa msisitizo ni kwa namna gani wagombea hao watahakikisha huduma za afya zinaboreshwa ikiwa watachaguliwa.
”Kwa sasa tunahitaji mbunge atakayegusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa vitendo, si maneno,” amesema Moses Lazaro kutoka Kata ya Mkwawa, huku akisisitiza wana kero nyingi ambazo hazijatatuliwa.
Pia, amesema changamoto ya migogoro ya ardhi imekuwa kero katika kata yao huku akisisitiza kwamba hivi sasa kero hiyo imezidi na inawagharimu.
Pamoja na hayo, wajumbe wamehoji kuhusu ukosefu wa ajira kwa vijana, wakitaka mbunge mpya awe na dira ya kuwasaidia kupitia miradi ya kiuchumi, fursa za mafunzo ya ufundi na ujasiriamali.
Ardhi, kivuko Kigamboni
Kwingineko katika Jimbo la Temeke, mkoani Dar es Salaam mjumbe kutoka Kata ya Tungi, Marco Macha amesema wanahitaji mwwakilishi jasiri atakayekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wananchi na siyo maslahi yake binafsi.
“Umeona Kigamboni uwekezaji kila kona, sehemu za wazi zinachukuliwa na wawekezaji, hatuna sehemu ambazo hata vijana wetu wanaweza kusema wakacheze mpira, hakuna sehemu ya kwenda kupunga upepo ukichoka.
“Wanajenga vituo vya mafuta kila kona, hakuna kiongozi anayefikiria ikiwa ajali ya moto ikitokea usalama wetu utakuwaje! Tunataka mbunge atakayekuja kuweka ukomo katika hili,” amesema Macha.
Kwa upande wake, Evalister Mbando, mjumbe kutoka Vijibweni, amesema wanahitaji mtu atakayeenda bungeni kupaza sauti walitumie Daraja la Nyerere bila kutozwa tozo kama ilivyo katika Daraja la Tanzanite na mengine.
“Wenzetu hawatozwi chochote, kwani Kigamboni tunaishi watu gani? Tunatamani Serikali iondoe jambo hili, bado hatujapata ufumbuzi; magari, bajaji na pikipiki zinatozwa utafikiri unaingia nchi zingine,” amesema Mbando.
Ilipofikia hatua ya watiania sita kujinadi, kila mmoja alikuwa anajenga hoja kuwashawishi wajumbe ikiwa atachaguliwa atafanyaje ili kuwa mwakilishi bora.
"Niwakati wa wananchi wa Kigamboni kuamua kupata kiongozi bora au mwakilishi, binafsi nastahili kuliko wengine wote kwakuwa nazijua shida za wananchi wa Kigamboni kwa kuwa tangu mdogo naishi huku najua kuna shida ya ardhi nichague nikawe muwakilishi bora," anasema Habib Mchange mgombea.
Cynthia Henjewele, amesema iwapo atapewa nafasi atakubali kuwa mtumwa wa wananchi kwa kusemea changamoto zao ili hatua zichukuliwe na Serikali.
"Kigamboni changamoto tunazo nyingi pamoja na kwa Serikali inajitahidi kuzitatua lakini nahitaji kura zenu ili niende bungeni nikaendeleze tulipoishia," amesema.
Mikopo ya asilimia 10
Suala la mikopo ya asilimia 10 lilibuliwa na Hadija Kiponga, aliyesema wananchi wa Temeke wamekuwa wakikopa vifaa mbalimbali na kutakiwa kulipa haraka, ikitokea wamechelewesha malipo, mali zao hupigwa mnada.
Kutokana na changamoto hiyo, Hadija ametaka mikakati ya watiania itakayowezesha wananchi kuondokana na mikopo inayowarudisha nyuma kiuchumi na kimaendeleo.
Mjumbe mwingine, Eva Mwenda alitaka kujua mikakati ya watiania hao kusaidia vijana ambao wanahangaika bila ajira kwa kipindi kirefu.
Wakati Said Masai alihoji namna watiania watakavyotatua tatizo la umasikini jimboni humo, akisisitiza Mfuko wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) umewatambua wananchi wenye vipato duni lakini hawajapata fedha hizo za Serikali.
Akijibu baadhi ya kero hizo, mgombea ubunge Temeke, Mariam Kisangi amesema alikuwa mbunge wa viti maalumu na ameacha nafasi hiyo kwa sababu anataka kutafuta maendeleo kwa wananchi.
“Nikiwa UWT sina eneo maalumu la kupeleka maendeleo, nikipata nafasi, nitatatua changamoto ya wafanyabiashara sokoni na miundombinu ya barabara.
Watu wanadhani ubunge ni rahisi, ubunge unahitaji uzoefu, nina uzoefu, naweza kuibua hoja na kutetea watu wangu wapate maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, Mussa Mtullya amesema sababu iliyomshawishi kugombea ubunge ni fursa zilizopo Temeke, hivyo anataka ridhaa hiyo kuwaonyesha wananchi fursa kwenye elimu na mikopo ya halmashauri.
“Changamoto ya bima ya afya kwa wazee na wajawazito pamoja na ukosefu wa fedha za Tasaf zote nitazifanyia kazi, barabara na maji nazo ni kero nitahakikisha tunaziondoa,” amesema.
Ajira, miundombinu
Kwingineko mkoani Kilimanjaro, changamoto za miundombinu ya barabara na ukosefu wa ajira kwa vijana vimetajwa kuwaathiri wananchi katika majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini mkoani hapa.
Changamoto nyingine zilizotajwa na wajumbe ni miundombinu chakavu kwa baadhi ya shule za msingi, upungufu wa walimu, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama baadhi ya maeneo, kushuka kwa uzalishaji wa kahawa, kukosekana masoko ya uhakika ya zao la ndizi na changamoto ya mikopo umiza kwa wananchi.
Mmoja wa wajumbe katika Jimbo la Vunjo, Joseph Shayo amesema changamoto ya barabara imekuwa ni tatizo la muda mrefu katika baadhi ya maeneo na wamekuwa wakiahidiwa kila wakati wa uchaguzi bila mafanikio.
Kwa upande wake, Amadea Mushi, mkazi wa Mbokomu ameeleza changamoto ya upatikanaji wa maji na uchakavu wa miundombinu ya shule na afya na kuomba kujua mpango mkakati wa kukabiliana na changamoto hizo kwa mbunge atakayeshinda.
Wakizungumza wagombea hao walijipambanua namna ambavyo watashughulika na changamoto hizo huku kila mmoja akielezea uwezo wake wa kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka na kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora.
Kilio cha malisho Manyara
Kwa upande wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wafugaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo wamelia na maeneo ya malisho ya mifugo yao kwa wagombea ubunge wa CCM waliokwenda kujitambulisha kwa wajumbe.
Mkazi wa Kijiji cha Shambarai, Marko Loishiye amesema wafugaji wa eneo hilo wanakabiliwa na maeneo machache ya kufugia, hivyo wagombea hao mmoja wao akipata nafasi ahakikishe anawapa kipaumbele.
Mfugaji wa Kijiji cha Lengasiti, Elibariki Laizer amesema mbunge ajaye wa Simanjiro ahakikishe makundi ya wafugaji yanapewa kipaumbele kwani ndiyo wapo wengi ili wasiwe wanahamahama tena kufuata malisho ya mifugo yao.
Mkazi wa Kijiji cha Naisinyai, Simon Mollel amewauliza swali wagombea katika kura ya maoni kuhusu namna watakavyojali maslahi ya mifugo yao pindi wakichaguliwa.
“Sasa hivi, wafugaji kwenye eneo la ukuta unazunguka migodi ya madini ya Tanzanite, tunaambiwa tukae umbali wa mita 200 wakati miaka iliyopita tulikuwa tunachunga mifugo baada ya mita 50 pekee, mtatusaidiaje?” amehoji.
Kupanuka kwa mto
Athari za Mto Gide kwa makazi ya binadamu, uhaba wa ajira na masoko ni miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa CCM wakati watiania wa udiwani na ubunge wakijitambulisha kuelekea kura za maoni Agosti 4, 2025.
Wajumbe wametoa hoja kuhusu Mto Gide ikiwa ni miezi miwili imepita tangu Mwananchi lilipochapisha ripoti maalumu kuhusu kutanuka kwa mito ikiwamo Gide, kunavyoathiri makazi ya wananchi wa Ubungo na maeneo ya jirani.
Wakiwa Kata ya Kimara, Dar es Salaam wajumbe walihoji kwa nini kingo za Mto Gide hazijajengwa licha ya kuwa ni miongoni mwa ahadi kuu za Profesa Kitila katika kipindi cha uongozi wake jimboni humo.
Akijibu hoja hiyo, Profesa Kitila ameeleza kuwa tayari alichukua hatua kwa kutumia Sh5 milioni kutoka mfuko wa maendeleo ya jimbo kwa kila kata inayopakana na mto huo, ikiwemo Kimara.
Amesema fedha hizo zilielekezwa katika juhudi za muda mfupi kupunguza athari za mto huo wakati Serikali ikiendelea na taratibu za utekelezaji wa mradi mkubwa wa kudhibiti mafuriko.
Profesa Kitila ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, amesisitiza akipewa ridhaa tena, atalifuatilia kwa ukaribu zaidi suala hilo hadi lifikie mwisho.
Mgombea Elizabeth Jackson amesema endapo watampa ridhaa atahakikisha anaboresha miundombinu ili kupunguza mafuriko na ajira kwa vijana. Kuhusu huduma za afya, ameahidi atapigania kupatikana kwa hospitali kwa ajili ya wakazi wa Manzese.
Naye Dk John Kahemela amesema magumu yanayoikumba Ubungo ni mengi, likiwamo suala la ukosefu wa maji na elimu duni.