Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yataka mapinduzi ya kisayansi tiba asili

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), uliofanyika leo Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema simulizi za watu wanaodai kupona baada ya kutumia dawa za asili zinapaswa kufanyiwa utafiti wa kisayansi.

Dar es Salaam. Serikali imetaka kuanzishwa kwa mapinduzi ya kisayansi katika sekta ya tiba asili ili kuthibitisha ufanisi wa dawa za mitishamba zinazotumiwa na mamilioni ya Watanzania, hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa afya na kuchangia upatikanaji wa huduma jumuishi za matibabu nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ulioanza Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam.

Profesa Mkenda amesema Tanzania haiwezi kuendelea kupuuza au kukubali moja kwa moja madai kuhusu ufanisi wa tiba asili bila kuyapima kwa mizania ya kisayansi, akisisitiza kuwa utafiti ndio njia pekee ya kubaini ukweli wa tiba hizo.

Amesema simulizi za wananchi wanaodai kupona baada ya kutumia dawa za asili zinapaswa kuwa chachu ya utafiti wa kina wa maabara, badala ya kubaki kama ushuhuda wa mdomo.

“Watu husema nilitumia mmea huu nikapona. Hapo ndipo sayansi inapohitajika. Ni lazima tuhakiki kwa mbinu za kisayansi,” amesema Profesa Mkenda.

Washiriki wa Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), uliofanyika leo Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam, wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa kuhusu tafiti za afya, ubunifu wa kisayansi na mwelekeo wa kuimarisha huduma za tiba nchini.

Amefafanua kuwa utafiti wa kisayansi utasaidia kubaini viambato halisi vya dawa za asili, dozi sahihi, pamoja na madhara yake, kabla ya kuingizwa katika mfumo rasmi wa tiba.

Profesa Mkenda amesema Serikali inaona fursa kubwa ya kuunganisha tiba asili na tiba ya kisasa kupitia tafiti, akisema hatua hiyo inaweza kupanua wigo wa huduma za afya na kupunguza gharama za matibabu.

“Nawapa changamoto msukume mbele mipaka ya maarifa ya kisayansi. Sayansi ndiyo daraja la kuunganisha tiba asili na tiba ya kisasa,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya dawa za kisasa zinazotumika duniani zilianzia katika mimea, lakini zilipitia uchunguzi wa kina wa kisayansi kabla ya kutumika kwa binadamu.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema vyuo vikuu vinapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika tafiti zenye kutatua changamoto za jamii badala ya kujikita kwenye machapisho pekee.

Amesema maendeleo ya teknolojia kama akili bandia (AI), jenomiki na afya kidijitali yanatoa fursa mpya za kuboresha huduma za afya, hivyo Tanzania inapaswa kuendana na mabadiliko hayo huku ikitumia rasilimali zake za ndani.

Wataalamu wa afya waliohudhuria mkutano huo wamesema endapo tiba asili itathibitishwa kisayansi, inaweza kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa afya nchini, hasa vijijini ambako upatikanaji wa dawa za kisasa bado ni changamoto.

Mjadala huo unafanyika wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha mpango wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC).

Serikali imesisitiza kuwa mustakabali wa afya nchini haupo katika kuchagua kati ya tiba asili na tiba ya kisasa, bali katika kutumia sayansi kuzichuja, kuzithibitisha na kuziunganisha kwa manufaa ya wananchi.