Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TRA Pwani yajipanga kwa Dira ya Taifa ikihimiza kulipa kodi kwa huari

Muktasari:

  • Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo na ustawi wa uchumi wa Tanzania yatategemea kiwango cha uaminifu wa wananchi katika kulipa kodi.

Kibaha. Wakati Tanzania ikiendelea kuweka msingi wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo, wakazi wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kuanza safari ya miaka 30 ijayo kwa kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari na kwa uaminifu, hatua ambayo imeelezwa kuwa ndiyo nguzo ya maendeleo endelevu na uchumi imara wa taifa.

Wito huo umetolewa leo Julai 1, 2026 mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa maendeleo, Mnyema amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 30 ya TRA yanapaswa kuwa chachu ya kujenga mfumo imara zaidi wa ukusanyaji wa mapato katika miongo ijayo.

"Tunapoadhimisha miaka 30 ya TRA, hatupaswi kuangalia tulikotoka pekee, bali tujiulize tunaelekea wapi. Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo yaanze kwa kila mwananchi kutambua kuwa kulipa kodi si adhabu, bali ni mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya nchi yetu," amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji, huku akisisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo inayobeba sehemu kubwa ya uchumi wa nchi kupitia uzalishaji, ajira na mchango wake katika mapato ya Serikali.

"Sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi. Kadiri biashara zinavyokua na wananchi wanavyoendelea kulipa kodi kwa uaminifu, ndivyo Serikali inavyopata uwezo mkubwa wa kuboresha huduma za afya, elimu, miundombinu na huduma nyingine za kijamii," alisema.

Mnyema aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na TRA kwa kufuata sheria za kodi na kutumia huduma za kidijitali zinazorahisisha utekelezaji wa wajibu wao.

Akizungumzia maadhimisho hayo, mkazi wa Mkoa wa Pwani, Samweli Mwanga, amesema TRA imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa walipa kodi, jambo lililoongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika kulipa kodi.

"Tunapongeza hatua zilizofikiwa na TRA katika kipindi cha miaka 30. Tunaiomba iendelee kujenga mahusiano mazuri na walipa kodi kwa kutoa elimu ya mara kwa mara, kusikiliza changamoto zetu na kutatua kwa wakati. Hilo litajenga imani na kuongeza mapato ya Serikali," amesema.

Naye mkazi mwingine wa Pwani, Dominick Michael, amesema maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu kati ya TRA na walipa kodi.

"TRA iendelee kuwahudumia walipa kodi kwa heshima, uwazi na weledi. Mahusiano mazuri yanajenga uaminifu, na uaminifu ndiyo unaochochea ulipaji wa kodi kwa hiari. Tukishirikiana, tutakuwa na taifa lenye uchumi imara na maendeleo endelevu," amesema.

Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA Mkoa wa Pwani yamekuwa fursa ya kutafakari mchango wa mamlaka hiyo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuimarisha huduma kwa walipa kodi na kuweka mikakati ya kuongeza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kujenga uchumi wenye ushindani kwa miaka ijayo.