Ubunifu wa taka za plastiki wafungua milango ya ajira kwa vijana 120
Diwani wa Kata ya Vingunguti, Omary Kumbilamoto, akisikiliza maelezo kutoka kwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibasila kuhusu ubunifu wa kutengeneza bidhaa kwa kutumia taka za plastiki, unaolenga kuhifadhi mazingira, kukuza ujuzi wa vijana na kufungua fursa za ajira na ujasiriamali.
Muktasari:
- Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Mabadiliko ya Tabia Nchi Tanzania (FORUMCC) umesema ubunifu wa kutengeneza bidhaa kwa kutumia taka za plastiki unawajengea vijana uwezo wa kujiajiri huku ukichangia kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka hizo.
Dar es Salaam. Wanafunzi 120 kutoka shule nane za mikoa ya Dar es Salaam na Lindi wameonyesha namna taka za plastiki zinavyoweza kubadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani ya kiuchumi, hatua iliyotajwa kufungua fursa za ajira na ujasiriamali kwa vijana, sambamba na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Ubunifu huo umefanyika kupitia mashindano ya michoro, kazi za sanaa na bidhaa zilizotengenezwa kwa kutumia taka za plastiki yaliyoandaliwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Mabadiliko ya Tabia Nchi Tanzania (FORUMCC).
Akizungumza leo Julai 17, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa mashindano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa FORUMCC, Sarah Ngoy amesema lengo la mpango huo si kuwafundisha vijana kutunza mazingira pekee, bali kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia ubunifu.
Amesema taka za plastiki ambazo mara nyingi hutupwa ovyo na kuchafua mazingira zinaweza kubadilishwa kuwa bidhaa zenye matumizi na thamani ya kiuchumi.
"Hatukuwa tunalenga tu kuwafundisha vijana kutunza mazingira. Tunataka ubunifu huu uwe fursa ya kujiajiri baada ya kuhitimu masomo na hata shule ziweze kuanzisha miradi ya kiuchumi kupitia kazi hizi," amesema Sarah.
Amesema kabla ya mashindano hayo, wanafunzi walipatiwa mafunzo kuhusu athari za taka za plastiki kwa mazingira, hususan katika mito na bahari, jambo lililowasaidia kubuni bidhaa mbalimbali zinazotokana na urejelezaji wa taka hizo.
Kwa mujibu wa Sarah, mradi huo unalenga kuwabadilisha vijana kutoka kuwa watazamaji wa changamoto za mazingira na kuwa sehemu ya suluhisho kupitia ubunifu na ujasiriamali.
Mashindano hayo yamefanyika kupitia mradi wa Bahari Yetu, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na kuratibiwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), kwa kushirikiana na WWF, TNC na WCS.
Wawakilishi wa Shule ya Msingi Kilindoni wakipokea hundi ya Sh1 milioni baada ya kuibuka washindi wa kwanza katika mashindano ya ubunifu wa kutengeneza bidhaa kwa kutumia taka za plastiki, yaliyolenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuibua fursa za ajira kwa vijana.
Amesema mradi huo unalenga kuboresha uhifadhi wa mazingira ya ukanda wa pwani na bahari kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari, kuongeza ushiriki wa jamii katika shughuli za uhifadhi na kupunguza uchafuzi unaosababishwa na taka za plastiki.
Aidha, amesema FORUMCC kupitia mradi huo imekuwa ikitoa elimu kwa umma na kusaidia kuandaa mikakati ya usimamizi wa taka za plastiki katika wilaya za Kinondoni, Ilala, Temeke na Mafia.
Diwani wa Vingunguti na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto, amesema ubunifu ulioonyeshwa na wanafunzi hao unathibitisha kuwa taka za plastiki zinaweza kuwa rasilimali badala ya kuwa uchafu.
"Mmetuthibitishia kwamba taka za plastiki si uchafu tu, bali zinaweza kuwa bidhaa zenye thamani na fursa ya kujiongezea kipato. Huu ndio mwanzo wa kujenga kizazi kinacholinda mazingira na kujitegemea," amesema.
Amewataka wanafunzi kuendelea kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira katika shule, familia na jamii kwa kuhamasisha ukusanyaji na urejelezaji wa taka za plastiki.
Kwa upande wake, Meneja wa Ubia wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Uchafuzi wa Mazingira kupitia Taka za Plastiki kutoka UNDP Tanzania, Flavian Mgeni, amesema Shule ya Msingi Kilindoni ya Mafia iliibuka mshindi wa kwanza kati ya shule nane zilizoshiriki mashindano hayo.
Amesema nafasi ya pili ilichukuliwa na Shule ya Sekondari Kitomondo, ikifuatiwa na Shule ya Msingi Ilala katika nafasi ya tatu, huku Shule ya Sekondari Mtongani ikishika nafasi ya nne.
Shule nyingine zilizofanya vizuri ni Juhudi Sekondari, Kibasila, Mbweni Teta Sekondari na Kitomondo Sekondari.
Washiriki hao walionesha bidhaa mbalimbali zikiwemo viti, mapambo na vifaa vingine vilivyotengenezwa kwa kutumia taka za plastiki na maboksi, wakionesha namna urejelezaji unavyoweza kuwa suluhisho la uchafuzi wa mazingira na chanzo cha ajira kwa vijana.