Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhakiki wa taarifa kupunguza malalamiko ya wastaafu

Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ( PSSSF) Kanda ya Kaskazini Magharibi,Yesaya Mwakifulefule,akizungumza jijini Arusha leo Alhamisi Julai 2, 2026 katika mafunzo kwa waajiri na maofisa wanaoshughulikka wanachama wa mfuko huo. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Maofisa utumishi wametakiwa kuhakikisha taarifa za watumishi zinahakikiwa na kukamilishwa kwa usahihi tangu wanapoajiriwa ili kupunguza malalamiko ya wastaafu kuhusu ucheleweshaji wa mafao.

Arusha. Ili kupunguza malalamiko ya wastaafu kuhusu ucheleweshaji wa mafao yao, maofisa utumishi wameagizwa kuhakikisha taarifa za watumishi zinahakikiwa na kukamilishwa kwa usahihi tangu wanapoajiriwa, ili kuondoa dosari katika nyaraka na taarifa ambazo zimekuwa zikichangia kuchelewa kwa malipo ya mafao.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Dk Jacob Rombo amesema hayo leo Alhamisi Julai 2, 2026, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha wakati akifungua mafunzo kwa waajiri na maafisa wanaoshughulikia masuala ya wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Amesema maofisa utumishi wana nafasi muhimu katika kuhakikisha kumbukumbu za watumishi zinakuwa sahihi, ikiwemo majina, tarehe za kuzaliwa, taarifa za ajira na michango ya hifadhi ya jamii, ili watumishi wanapostaafu wasilazimike kutumia muda mrefu kufuatilia mafao yao.

Amesema imeendelea kusisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo taasisi zote zinapaswa kuhakikisha zinaitumia ipasavyo katika kusimamia taarifa za watumishi.

Ameongeza kuwa maofisa utumishi wanapaswa kuhakikisha watumishi wote wanasajiliwa kwenye mfumo wa PSSSF mara wanapoanza kazi, badala ya kuchelewesha usajili, jambo ambalo linaweza kusababisha changamoto za michango na ucheleweshaji wa mafao wanapostaafu.

“Sisi wote ni wastaafu watarajiwa. Elimu tunayopata leo si kwa ajili ya watu wengine pekee, bali ni kwa manufaa yetu pia. Tukisimamia vizuri taarifa za watumishi leo, kesho tutakapostaafu tutapunguza usumbufu tunaouona kwa baadhi ya wastaafu,” amesema.

“Usumbufu wanaoupata wastaafu wa sasa tuuepuke tusije tukapata na sisi kesho tukistaafu. Ni kama tunaweka akiba ya kesho. Ndugu zangu, utumishi wa umma una mwisho, tuweke rekodi sawasawa tusaidie Serikali ili kupunguza manung’uniko ya wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa PSSSF Kanda ya Kaskazini Magharibi, Yesaya Mwakifulefule amesema mfuko huo umeanza kutekeleza mpango wa kuhakikisha wanachama wanalipwa mafao yao ya mkupuo siku moja kabla ya tarehe rasmi ya kustaafu.

Amesema lengo la mpango huo ni kuondoa malalamiko ya muda mrefu ya wastaafu kusubiri mafao kwa miezi kadhaa baada ya kuondoka kazini.

“Tayari tuna wanachama ambao wamelipwa mafao yao siku moja kabla ya tarehe yao ya kustaafu. Hili linawezekana pale taarifa zote za mtumishi zinapokuwa zimekamilika mapema na michango yake imewasilishwa ipasavyo,” amesema.

Ameeleza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya PSSSF na waajiri, hususan maofisa utumishi wanaohusika na kuandaa na kuhakiki taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu.

Amebainisha kuwa baadhi ya changamoto zinazosababisha ucheleweshaji wa mafao ni tofauti za majina kwenye nyaraka, mapengo ya michango na taarifa zisizokamilika pamoja na kuchelewa kuwasilishwa kwa nyaraka muhimu.

“Ndio maana tunawataka waajiri waanze kufuatilia taarifa za watumishi wao mapema kabla ya kufikia umri wa kustaafu ili dosari zote zirekebishwe kwa wakati,” amesema.

Naye Ofisa Tawala kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Shedrack Kengese amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa mpana kuhusu wajibu wa maofisa utumishi katika kuhakikisha kumbukumbu za watumishi zinakuwa sahihi.

Amesema maafisa utumishi wana jukumu la kuhakikisha taarifa zote za watumishi zinaendana na zilizopo kwenye mfumo wa PSSSF ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kudai mafao.

Ameongeza kuwa mapengo ya michango ni miongoni mwa changamoto zinazopaswa kushughulikiwa mapema ili mtumishi anapostaafu aweze kupata stahiki zake kwa wakati.

“Tukisimamia vizuri mifumo ya PSSSF na kuhakikisha taarifa za watumishi ni sahihi, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ambazo zimekuwa zikiwasumbua baadhi ya wastaafu kupata mafao yao kwa wakati,” amesema.