Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UNDP, Finland watambua biashara 14 ndogondogo na za kati nchini

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dk Linda Salekwa (katikati) na wageni wengine wakipiga makofi wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP ) pamoja na Serikali ya Finland wakitambulisha biashara bunifu 14 ndogo ndogo na za kati (MSMES) kupitia mpango wa #GreenCatalyst.  Hafla hiyo ilifanyika Mjini Njombe leo Jumanne Aprili 14, 2026.

Muktasari:

  • Hatua hiyo inaashiria mafanikio muhimu ya  kukuza ujasiriamali endelevu na uzalishaji wa ajira ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu nchini Tanzania

Njombe. Jumla ya biashara bunifu 14 ndogo ndogo na za kati (MSMEs)  zilizopo chini ya mpango wa #GreenCatalyst unaoungwa mkono na Serikali ya Finland, zimetambuliwa ili kukuza ujasiriamali endelevu na uzalishaji wa ajira ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu nchini Tanzania.          

Bashara hizo zimefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania kupitia programu yake ya ubunifu ya Funguo kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) na Serikali ya Finland.

Hatua hiyo inaashiria mafanikio muhimu ya kukuza ujasiriamali endelevu na uzalishaji wa ajira ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu nchini Tanzania.

Uzinduzi huo wenye  kaulimbiu ya:“Kuchochea Ubunifu na Ujasiriamali katika Mnyororo wa Thamani wa Misitu,” umewakutanisha wadau kutoka Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine ili kuonesha biashara zilizochaguliwa.

Pia, awamu ya pili ya maombi ya ufadhili wa ruzuku ya kuchochea ukuaji kwa wabunifu wa biashara endelevu zinazozingatia mustakabali wa mazingira imezinduliwa huku wabunifu wakitakiwa kuwasilisha maombi yao.

Katika awamu ya kwanza ya ufadhili, #GreenCatalyst iliwezesha biashara ndogo, ndogo na za kati bunifu katika mnyororo wa thamani wa misitu, hususani zile zinazoongozwa au kunufaisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi.

Kutokana na maombi 160 yaliyopokewa mwaka 2025, biashara 14 zilichaguliwa kupitia mchakato makini uliopitia tathmini za hatua mbalimbali ulioongozwa na kamati huru ya uwekezaji, zilizopokea zaidi ya Sh1  bilioni kama ruzuku, pamoja na msaada endelevu wa kiufundi.

Akizungumza leo Jumanne Aprili 14, 2026, Meneja wa Programu ya Funguo wa UNDP, Joseph Manirakiza amesema  maombi hayo yatakuwa wazi mpaka Mei 31, 2026 ili kusaidia biashara ndogondogo na za kati za Kitanzania zilizo katika hatua za awali au zinazokua ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu kupitia ufadhili chochezi, kufungua fursa za biashara endelevu na rafiki kwa mazingira, kuzalisha ajira na kubadilisha uchumi wa vijijini.

Amesema kipaumbele kimewekwa kwa biashara bunifu zinazojumuisha vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na zinazofanya shughuli zake au kujumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi.

Manirakiza amesema zinazolengwa ni  uchakataji wa mbao, bidhaa rafiki kwa mazingira, mbadala wa mkaa, useremala, samani, ufugaji nyuki, ubunifu wa mianzi, mafuta kwa matumizi tofauti, na huduma za kidijitali za misitu.

Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa UNDP, John Rutere akielezea dira ya mpango huo amesema: "Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususani misitu. Rasilimali hizi si muhimu tu kwa mustakabali uendelevu wa mazingira bali pia zinatoa fursa kubwa za ukuaji wa uchumi, ubunifu na ajira.

“Changamoto kubwa inayotukabili ni  kunufaika na rasilimali hizi kwa uwajibikaji ili kutengeneza ajira zenye staha, hasa kwa vijana, huku tukilinda mazingira kwa vizazi vijavyo. Hili ndilo lengo kuu la #GreenCatalyst,"amesema Rutere.

Amesema katika kuunganisha ubunifu na upatikanaji wa fedha, ujuzi na masoko, mpango huo utasaidia kubadilisha mawazo endelevu rafiki kwa mazingira na kuwa biashara halisi zinazozalisha kipato na ajira katika jamii na kutoa shukrani kwa Serikali ya Finland kwa ushirikiano wake endelevu.

 Mratibu wa Ushirikiano wa Maendeleo, William Nambiza amesema: "Finland itaendelea kujizatiti katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa misitu endelevu nchini Tanzania. Kupitia miradi kama #GreenCatalyst, tunasaidia kufungua fursa kwa vijana na wanawake; na kuhakikisha sekta hii inachangia kikamilifu ajira, ubunifu na ukuaji wa uchumi shirikishi, husasani katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini."

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa amepongeza kuwapo  kwa mradi huo na kuahidi ushirikiano wa Serikali.

"Tunaipongeza Serikali ya Finland na UNDP kwa mpango huu wenye manufaa kubwa. Kama Serikali, tunaendelea kujenga mazingira wezeshi yatakayoruhusu biashara hizi kukua, kustawi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa ndani pamoja na uhifadhi wa mazingira, hasa katika Nyanda za Juu Kusini."

Amesema ni jambo la kutia moyo kuona vijana na wanawake kupewa kipaumbele kupitia ujasiriamali, makundi ambayo Serikali inaendelea kuyainua kwa jitihada kubwa.

Biashara bunifu zinazofanya shughuli zake katika mnyororo wa thamani wa misitu katika mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma na Lindi zinahimizwa kuwasilisha maombi ya ufadhili wa ruzuku wa #GreenCatalyst kabla ya Mei 31, 2026.