Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usiri watawala jina la mgombea urais Chaumma

Muktasari:

  • Vikao vya juu vya Chaumma vinaendelea kwa usiri mkubwa jijini Dar es Salaam kujadili majina ya watiania kwa nafasi ya urais sambamba na maandalizi ya mkutano mkuu utakaofanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Usiri umegubika kikao maalum vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kinachoendelea katika Hoteli ya Golden Tulip, Masaki, jijini Dar es Salaam.

Inaelezwa kuwa miongoni mwa agenda wanazozijadili mbali ya maandalizi ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho, ni kujadili majina ya walioomba kugombea urais wa Tanzania na Zanzibar.

Kikao hicho kilichoanza leo mchana, kinatajwa kuwa ni cha hatua ya mwisho ya maandalizi kuelekea Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chaumma, utakaofanyika kesho Agosti 7, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na viongozi wa ndani wa chama hicho, vikao vya leo vinapokea na kujadili majina hayo ya watiania, mbele ya Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuchujwa na kujadiliwa kwa kina kabla ya kupitishwa rasmi kesho kwenye Mkutano Mkuu.

“Hili ni tukio muhimu sana kwa chama chetu. Kikao hiki kinaangalia kwa undani sifa na uwezo wa kila mmoja aliyejitokeza, tukilenga kumpata mgombea bora mwenye dira na maono ya kweli kwa Taifa,” amesema msemaji wa chama hicho, John Mrema, alipozungumza na Mwananchi akiwa eneo la mkutano huo.

Amesema kikao hicho kinaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chaumma, Hashim Rungwe ambaye ameshiriki mara tatu katika mbio za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi wengine wanaoshiriki kikao hicho ni pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Benson Kigaila.

Pamoja na viongozi hao, wapo pia wajumbe kutoka Zanzibar na mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

“Ninachoweza kusema ni kwamba, chama chetu kina watu makini. Tumevutia watu wa kada tofauti wapo waliowahi kugombea nafasi mbalimbali ikiwamo ya ubunge na udiwani, vijana wapya, lakini wote wameonesha ari ya kuliongoza taifa hili kwa misingi ya haki, uhuru na maendeleo ya kweli,” amesema  mjumbe mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake akisema si msemaji wa chama.

"Vikao hivi vinapitia sifa na vigezo vya watiania na kesho majina yatawasilishwa katika Mkutano Mkuu, pale Mlimani City kwa ajili ya uteuzi wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar," amesema Mrema bila kutaja majina wala idadi ya wagombea.

Uteuzi wa wagombea hao, utahitimisha hatua ya ndani ya chama na kutoa nafasi kwa wagombea kuchukua fomu za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kupata ridhaa rasmi ya kugombea nafasi hizo.