Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana 800 wawezeshwa ufundi stadi, 400 wajiajiri

Wahitimu wa awamu ya tatu wa mradi wa VEMA waliohitimu katika chuo cha VETA Mwanza.

Muktasari:

  • Vijana hao wamepata mafunzo katika fani za ufundi magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi bomba, umeme wa majumbani, ushonaji, uashi pamoja na upishi.

Mwanza. Vijana 800 wamenufaika na mafunzo ya stadi za ufundi kupitia mradi wa Vijana, Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) unaotekelezwa mkoani Mwanza, huku sehemu kubwa wakianzisha biashara na wengine kuajiriwa baada ya kupata ujuzi na vifaa vya kuanzia.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa mradi wa utekelezaji wa Plan International Tanzania, Martha Lazaro katika mahafali ya kuhitimisha awamu ya tatu ya mradi huo yaliyofanyika Juni 26 jijini Mwanza.

Katika awamu ya tatu, vijana 183 kutoka halmashauri za Ilemela na Nyamagana wamehitimu mafunzo ya ufundi stadi katika chuo cha VETA mkoani Mwanza.

Amesema wahitimu wa awamu ya tatu wamekabidhiwa vifaa vya kuanzia 44 ili kuwawezesha kuanza kutumia ujuzi wao kujiajiri na kujipatia kipato kupitia shughuli mbalimbali za kiufundi.

Mradi huo unaotekelezwa na Plan International kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (DGD) unalenga kuwawezesha vijana wa kati ya miaka 10 hadi 24 kiuchumi na kijamii.

Ofisa Elimu Watu Wazima na Nje ya Mfumo Usio Rasmi, Maeda Chambuko (kushoto) akimkabidhi vifaa vya kuanzia muhitimu (katikati) katika mahafali ya awamu ya tatu katika chuo cha Veta Mkoani mwanza. Kulia ni Mkuu wa mradi wa utekelezaji wa Plan International Tanzania, Martha Lazaro.

Kwa mujibu wa Martha, jumla ya vijana 800 wamepata mafunzo kupitia awamu zote za mradi huo, ambapo 88 tayari wamepata ajira rasmi, 400 wamejiajiri na zaidi ya biashara 809 zimeanzishwa katika Mkoa wa Mwanza kupitia ujuzi walioupata.

Hatahivyo, Martha amesema baadhi ya vijana baada ya kuhitimu na kukabidhiwa vifaa vya kuanzia kazi, wanavihifadhi bila kuvifanyia kazi kama ilivyokusudiwa, huku wengine wakidaiwa kuviuza.

“Leo hii unaweza ukagawa vifaa kwa vijana lakini katika ufuatiliaji utakuta baadhi ya vifaa vimewekwa ndani kwa miezi kadhaa bila kutumika, au mhusika anasubiri mradi uishe ndipo aviuze,” amesema Martha.

Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Ofisa Elimu Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi, Maeda Chambuko amezitaka Serikali za Mitaa na Halmashauri kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa vifaa vinavyotolewa kwa vijana ili kuhakikisha vinatumika kama ilivyokusudiwa.

Amesema kuna taarifa zinazoonesha baadhi ya vijana kuuza vifaa hivyo au kuvihifadhi bila matumizi, jambo ambalo linahitaji udhibiti wa karibu ili kuhakikisha malengo ya miradi ya uwezeshaji yanatimia.

“Nawaelekeza viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kusimamia na kufuatilia matumizi ya vifaa vinavyotolewa na wadau ili kuhakikisha vinatumika kama ilivyokusudiwa,” amesema.

Baadhi ya vifaa walivyokabidhiwa wahitimu wa  ufundi kupitia mradi wa VEMA.

Ameongeza kuwa vifaa hivyo vinapaswa kuwa chachu ya mabadiliko kwa vijana na si mali ya muda mfupi ya kuuza au kuhifadhi, bali mtaji wa kuanzia maisha.

Naye, Mkuu wa Chuo cha VETA Mwanza, Henry Kasele amesema vijana waliohitimu wamepata mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo umeme wa magari, ufundi magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi bomba, umeme wa majumbani, ushonaji, uashi pamoja na upishi.

Amesema katika awamu hiyo ya tatu pekee, vijana 200 walidahiliwa, kati yao wanawake 98 na wanaume 102, huku wahitimu wakiwa 183 sawa na asilimia 91.5 ya walioanza mafunzo.

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza namna wanavyotarajia kutumia ujuzi walioupata kuboresha maisha yao na kusaidia familia zao.

Emmanuel John, mmoja wa wanufaika, amesema vijana wanapaswa kutumia vifaa wanavyopewa kama mtaji wa kuanzia badala ya kuvigeuza kuwa bidhaa ya kuuza.

Amesema vifaa hivyo ni msingi muhimu wa kuanzisha maisha ya kujitegemea, na vinapaswa kutunzwa ili viweze kuleta matokeo chanya ya kiuchumi kwa muda mrefu.

Naye Tamasha Jumanne amesema ujuzi alioupata atautumia si tu kwa manufaa yake binafsi bali pia kuwasaidia vijana wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo.

Amesema kupitia ujuzi huo, ataweza kuchangia maendeleo ya jamii na kuwa mfano kwa vijana wengine katika eneo lake.